KWA mara ya kwanza Ken Gold inatarajia kushiriki Ligi Kuu tangu ilipoanzishwa timu hiyo mwaka 2018 ilipobadilishwa jina kutoka Gipco FC iliyokuwa mkoani Geita.
Timu hiyo yenye makazi yake Wilayani Chunya mkoani Mbeya, inajiandaa na Ligi Kuu kwa mara ya kwanza baada ya kupanda daraja ikiwa na rekodi ya ubingwa wa Championship.
Ken Gold inayomilikiwa na mtu binafsi, inatarajia kuanza ligi hiyo kwa kuwakaribisha Singida Big Stars, mchezo utakaopigwa Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya kasha kuwavaa Yanga, Septemba 25 katika uwanja huo.
Pamoja na ugeni walionao, benchi la ufundi, wachezaji, uongozi na wadau wa soka jijini humo pamoja na mashabiki wake wameonyesha matarajio yao wakieleza timu ipo fiti na tayari kwa ligi.
Nahodha wa timu hiyo, Charles Masai amesema licha ya ugeni walionao kwenye ligi lakini hawana hofu kutokana na maandalizi waliyofanya na hamu waliyonayo ya kucheza Ligi Kuu,
Anasema timu imekuwa na muda mzuri wa maandalizi kwa kambi bora na ushirikiano walionao ndani na nje ya uwanja akieleza kwa sasa akili zote zipo kwenye mchezo wa Jumapili dhidi ya Singida BS.
“Tumekuwa na muda mzuri na wa kutosha kufanya maandalizi, tunawaheshimu wapinzani lakini kwa kuwa tupo nyumbani tunaamini tutashinda kwa sababu nia na uwezo tunao.”
“Ushirikiano ni mkubwa ndani na nje kwa mashabiki namna wanavyo tusapoti, hali inayotupa hamasa kubwa kutamba kuanza vyema msimu na hatuna hofu yoyote,” anasema Masai.
Kwa upande wake winga wa timu hiyo, Helbert Lukindo anasema licha ya wachezaji wengi kikosini kuwa chipukizi kwenye Ligi Kuu, lakini uwapo wao kama wazoefu itawaamsha.
Anasema wanafahamu ugumu wa ligi hiyo, lakini kwa kikosi walichonacho hawana hofu yoyote kutokana uwezo binafsi walionao na wanahitaji kuipambania Ken Gold kwa nguvu zote.
“Kwa kuwa bado wageni wa ligi tutapambania nafasi tano za juu, tunjua ugumu ulivyo kwenye michuano hii ila umejipanga kuipambania Ken Gold na hatuwezi kushuka,” anasema nyota huyo aliyekipiga Mbao na Biashara United.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Fikiri Elias anasema pamoja na ugeni katika ligi hiyo, lakini wasichukuliwe kinyonge kwani wapo fiti kupambana na yeyote watakayekutana naye na shughuli itaanza Jumamosi dhidi ya Singida BS.
Anasema jina ndilo geni lakini wapo wachezaji wenye uzoefu na uwezo wa kuamua mechi na kutamba kuwa watawaheshimu wapinzani ila siyo kuwaogopa akisema kila mechi kwao ni vita ya pointi tatu.
“Ugeni ni wa jina lakini timu ni wachezaji na wapo wenye uzoefu na uwezo wa kupambana kupata ushindi kila mechi, tumekuwa na maandalizi mazuri na kazi itaanza Jumapili dhidi ya Singida BS,” anasema Elias.
Elias anasema anafahamu ugumu wa ligi lakini kwa uzoefu na uwezo wake anaamini watafanya vizuri kwani wamekuwa na muda mwingi kujiandaa kwa ajili ya Ligi Kuu.
Katibu Mkuu wa timu hiyo, Benson Mkocha anasema uongozi umeweka mipango mizuri ikiwa ni kuwasapoti wachezaji na benchi la ufundi kwa ujumla kuhakikisha wanafikia malengo.
Anasema Ken Gold wanaoichukulia poa timu hiyo watajionea maajabu yao na kwamba licha ya usajili wao kutokuwa na wachezaji wenye majina makubwa, lakini kazi itaonekana uwanjani.
“Wanaotuchukulia poa waje uwanjani kuanzia Jumapili tutakaposhuka kazini dhidi ya Singida BS, kimsingi tumesajili kulingana na mahitaji ya timu, hatuna majina makubwa ila ukubwa wetu ni matokeo,” anasema Mkocha.
Kigogo huyo anaongeza msimu huu wanahitaji kucheza na kubaki Ligi Kuu, kisha baada ya misimu miwili mbele watapambania nafasi nne za juu na wamejipanga.
Mmoja wa wadau wa soka na mkereketwa wa timu hiyo wilayani chunya, Ayoub Omary anasema kwa heshima waliyoweka Ken Gold wataendelea kuipa sapoti.
Anasema kazi waliyofanya viongozi kwa kuiheshimisha Chunya na Mbeya kwa jumla, haipaswi kutengwa bali kuongozana nayo Ligi Kuu akiwataka wachezaji kutobweteka.
“Tumeenda Ligi Kuu, lazima tuendelee kushirikiana na sisi kama wadau tutakuwa na timu bega kwa bega, wachezaji wasibweteke kwa namna yoyote ili kutoshuka daraja,” anasema Omary.
Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mmbarack Batenga anasema kuhusu suala la uwanja uliopo wilayani humo, wanaenda kulifanyia kazi kuhakikisha Tanzania inahamia Chunya.
“Nipo na Mkurugenzi Tamimu Kambona, katika bajeti yam waka huu tutahakikisha uwanja unakamilika na timu inacheza mechi zake huko, tunataka Chunya kuiweka katika ramani za soka,” anasema Batenga.
Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoani Mbeya (Mrefa), Jumbe Sadick, anasema heshima waliyoiweka Ken Gold watahakikisha wanaisapoti timu hiyo na kushauri kutumia uwanja wa Sokoine kuliko kuhamia kwingine.
“Hatujawahi kupandisha timu na kuwa bingwa wa ligi, tunashauri waangalia wachezaji wanaofanya vizuri ambao wataachwa na zile timu kubwa kuweza kuwaleta kuongeza nguvu,” anasema Jumbe.
Castory Mwangabo, Mussa Malika, Mishamo Michael, Hamad Hamis, Bilali Abdi, Amukena Lubinda, Masoud Hamad, Ramadhan Salum, Adam Uled, Said Kitima, Emanuel Mpuka na Ambokise Mwaipopo.
Wengine ni; Tungu Robert, Kelvin Simon, Asanga Mwakalibule, Helbert Lukindo, James Msuva, Salum Idrisa, Paul Matelaz, Steven Mganga, Martin Kazila, Haji Ugando, Charles Masai Joshua Mwakasaba na George Sangija.