Geita. Malalamiko ya madereva wa bodaboda kutekwa na kuporwa pikipiki zao, mauaji ya watoto wakiwamo walemavu ndiyo vilivyotawala kwenye ziara ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi mkoani Geita.
Kiongozi huyo wa chama akiwa anahitimisha ziara yake mkoani Geita alikutana na kero mbalimbali zikiwamo za mauaji ya watoto wakiwamo wenye ulemavu kwa imani za kishirikina.
Dk Nchimbi aliingia Geita Agosti 12, 2024 akitokea mkoani Kagera ambapo amefanya mikutano ya hadhara, kusikiliza kero za wananchi pamoja na kutoa maelekezo kwa watendaji na viongozi wa Serikali katika kuzitafutia ufumbuzi.
Wakizungumza mbele ya kiongozi huyo waendesha bodaboda walisema wanatekwa wanapotekeleza majukumu yao na kuporwa pikipiki zao, jambo linalowatia hofu hasa nyakati za usiku.
Mwendesha bodaboda mjini Geita, Linus Masanja amesema wenzake wawili walijeruhiwa na kuporwa pikipiki zao. Amesema matukio hayo na mengine yaliyotokea Geita yamewajaza hofu katika kazi yao hiyo, hivyo wanalazimika kuepuka kwenda baadhi ya maeneo.
“Tunaomba Serikali itusaidie kukabiliana na changamoto hii. Bodaboda ndiyo ajira yetu, tukiacha kuendesha tutaishi vipi na kazi huku mtaani hakuna? Tunaomba Serikali itulinde ili tufanye kazi zetu kwa usalama,” amesema Masanja.
Kwa upande wake, Emmanuel Mashaka amesema wanahitaji kupatiwa ofisi ili waendeshe kazi zao kisasa kwa kutambuana na kukabiliana na matukio ya utekaji wa bodaboda.
“Rais Samia alituahidi kutujengea ofisi ya chama, hata hivyo bado hilo halijatekelezwa. Naomba Serikali ilione jambo hili kwa jicho la pekee na kulipatia ufumbuzi,” amesema.
Dk Nchimbi alimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela kuelezea kuhusu kero hiyo ya vijana wanaoendesha bodaboda, huku akisisitiza kwamba chama kinatambua umuhimu wa usalama wa kila Mtanzania wakiwemo bodaboda.
Shigela ameahidi kufanya kikao na bodaboda wa Geita wiki ijayo ili kuzungumzia kwa kina madai yao ya kutekwa na kuporwa pikipiki zao, jambo ambalo ni kinyume cha sheria za nchi.
“Ndugu Katibu Mkuu, wiki ijayo nitafanya kikao na bodaboda ili kuona kama kuna mtu anafanya hujuma ya kuteka watu na kama yupo, kiama chake kimefika,” amesema Shigela.
Hata hivyo, amesema walipokea maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwataka kutengeneza mazingira mazuri kwa wamachinga na bodaboda na aliwapatia Sh10 milioni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa ofisi yao.
“Ujenzi wa ofisi hiyo itakayotumiwa na wamachinga na bodaboda umekamilika na muda wowote watakabishiwa jengo hilo.”
“Septemba 15 tutakuwa na sherehe ya kuwakabidhi jengo wahusika. Ili wasibughudhiwe, tulikubaliana kuwatafutia maeneo kwa ajili ya kuendesha shughuli zao,” amesema Shigela.
Mauaji ya walemavu, watoto
Akizungumza kwenye mkutano uliofanyika Geita mjini, Dk Nchimbi amesema moja ya kero walizozipokea ni pamoja na vitendo vya kikatili dhidi ya watu wenye ulemavu na watoto kwa imani za kishirikina.
Amesema baadhi ya watu wamekuwa wakiwafanyia ukatili watoto na wenye ulemavu kwa imani kujipatia madini kwenye migodi. Amesema Taifa likikubali kuacha maadili yake linakuwa mfu.
“Ni lazima tukubali kushirikiana na Mkuu wa Mkoa kuhakikisha tunakomesha vitendo vyote vya kikatili dhidi ya watu wenye ulemavu na watoto. Tuwapende watu wenye ulemavu, tuwahudumie, tuwalinde. Tuwapende watoto wetu, tuwahudumie, tuwalinde,” amesema Dk Nchimbi.
Wakati huohuo, Dk Nchimbi ameitaka Serikali kuongeza kasi ya kuwalea wachimbaji wadogo ili nao wawe wakubwa wachangie katika Pato la Taifa.
Kada wa CCM Geita, Sophia Mayala amesema matukio ya mauaji ya watoto yanayohusishwa na imani za kishirikina yamekuwa yakiwatia hofu wazazi, jambo linalowafanya waongeze uangalizi wa watoto wao hasa wanapokuwa wakicheza mitaani.
“Wazazi tunaishi kwa hofu, tunasikia watoto wanaibiwa na kuuawa, tunaomba Serikali ikomeshe matukio haya ili tuishi kwa amani kama zamani, kwa sasa hatuna amani kabisa,” amesema Sophia.
Kuhusu changamoto ya barabara, Mbunge wa Geita Mjini, Constantine Kanyasu amesema wana changamoto ya barabara ambapo licha ya kuwa mkandarasi yuko kazini, lakini ujenzi hauendi kwa hasi iliyotarajiwa na wananchi wa Geita.
“Tuna uhitaji mkubwa wa barabara za ndani katika jimbo hili, tunaomba utusaidie kuweka msukumo ili mkandarasi aweze kumaliza kazi kwa haraka kama ilivyotarajiwa ifikapo Februari 2025,” amesema Kanyasu akimweleza Katibu Mkuu Dk Nchimbi.
Kutokana na hoja hiyo, Dk Nchimbi alimwita Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Zainabu Katimba kujibu hoja ya mbunge huyo ambapo amekiri kwamba Geita kuna mradi wa ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 17 utakaogharimu Sh22 bilioni, hata hivyo amesema mradi huo hauendi kwa kasi kama ilivyotarajiwa
Amesema mkandarasi katika mradi huo sasa amefikia asilimia 20 wakati alitakiwa kuwa amefikia asilimia 50 kufikia Julai. Amefafanua kuwa amewasiliana na Naibu Katibu Mkuu na wamekubaliana kwamba atakwenda Geita kusukuma ujenzi huo na kuona changamoto zilizopo.
“Nimeongea na Naibu Katibu Mkuu wa Tamisemi anayeshughulikia mambo ya miundombinu, amenieleza kwamba atakuja kuweka kambi hapa kumsimamia mkandarasi ili kuhakikisha kwamba anakwenda kwa kasi,” amesema Katimba huku akishangiliwa na wananchi kwenye mkutano huo.
Akiwa njiani kutoka Geita kuelekea Sengerema, Dk Nchimbi na msafara wake wamepita katika Jimbo la Geita Vijijini ambapo mbunge wa jimbo hilo, Joseph Kasheku, maarufu Msukuma alimwomba Katibu Mkuu kuzungumzia ujenzi wa barabara ya Nzela – Nkome ambapo mkandarasi alitarajiwa kukabidhiwa eneo la mradi jana, hata hivyo haikuwezekana.
Dk Nchimbi alimpa nafasi Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya kuzungumzia barabara hiyo, ambapo amekiri kuwa mchakato wa ujenzi huo umekamilika, mkataba umesainiwa na jana mkandarasi alitarajiwa kukabidhiwa eneo la mradi huo wenye thamani ya Sh42.8 bilioni.
“Niwahakikishie wananchi wa Geita Vijijini kwamba mbunge wenu aliomba ujenzi wa barabara hii, Rais wetu amekubali ombi lake, ametoa fedha na muda wowote ndani ya wiki hii, mkandarasi ataanza ujenzi,” amesema Kasekenya.
Uhitaji wa kituo cha afya
Akiwa Wilaya ya Chato, mbunge wa Chato (CCM), Dk Medard Kalemani amesema Kata ya Bwanga ina wakazi zaidi ya 60,000, hivyo inaongoza kwa idadi kubwa ya watu katika Wilaya ya Chato ikifuatiwa na Muganza.
Kwa sababu hiyo, ameeleza kuwa Kituo cha Afya Bwanga kwa wiki kinahudumia wastani wa wajawazito 150 hadi 200 huku wagonjwa wanaofika kupatiwa huduma wakiwa zaidi ya 200 kwa siku.
Dk Kalemani ameishukuru Serikali kwani licha ya kata hiyo kuwa na vijiji vinne, lakini ina shule 10 za msingi na tayari wamepatiwa Sh100 milioni za ujenzi wa kituo cha mabasi.
“Ombi letu kituo cha afya kilichopo kipande hadhi kuwe hospitali ya wilaya kwa kujengewa jengo la utawala, wodi ya watoto na kinamama,” amesisitiza.
Vilevile, ameomba eneo la Matebe lililopo hifadhini lipatiwe hadhi ya kuwa kijiji maalumu, kwani kuna idadi kubwa ya watu ambao wanahitaji huduma za afya, shule na umeme.