Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kinakusudia kuwafikisha mahakamani Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadhi Haji na Naibu Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza kwa madai ya kusababisha viongozi wakuu na wanachama wa chama hicho kukamatwa na kuumizwa.
Hata hivyo, Chadema imesema itawashtaki kwa majina yao na si kwa vyeo vyao.
Kwa mujibu wa Chadema, Awadhi na Nyahoza ndio waliokuwa mstari wa mbele kuratibu mchakato wa kukwamisha kongamano la Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), lililopangwa kufanyika Jumatatu ya Agosti 12, 2024 katika uwanja wa Ruanda-Nzovwe, jijini Mbeya.
Alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia hilo, Nyahoza amesema uamuzi wao wa kumpeleka mahakamani uendelee, lakini yeye alikuwa akitekeleza wajibu wake.
“Wao waendelee tu, sisi tunaendelea kutekeleza wajibu wetu kwa hiyo tunafanya kile tulichopaswa kukifanya, lakini njoo ofisini tutaongea kwa kina,” amesema Nyahoza.
Alipotafutwa Awadhi, simu yake ilipokewa na mtu aliyejitambulisha kuwa ni msaidizi wake na kudai kuwa bosi wake yuko kikaoni na kwamba, hivyo hana majibu ya swali lolote linalomuhusu kiongozi huyo.
“Afande yupo kikaoni. Swali lolote mimi siwezi kuwa na majibu yake hadi mwenyewe, kwa sasa yupo kikaoni,” ameeleza.
Akizungumza na waandishi wa habati leo Jumatano Agosti 14, 2024, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kutokana na hilo, Chadema kitawachukulia hatua za kisheria Awadhi na Nyahoza.
“Katika Jeshi la Polisi wapo watu wema wanaoyaona wanashindwa kuongea, hivyo hatuwezi kulishushia lawama Jeshi lote la polisi, lakini hawa wawili tunawataka wanasheria wetu wakutane kutengeneza mashtaka ya madai dhidi ya Nyahoza na Awadhi.
“Tunamburuza mahakamani kama Nyahoza, tutamburuza mahakamani Awadh Haji, jopo hili litaongozwa na Makamu Mwenyekiti (Tundu Lissu). Kwa muda mrefu Lissu hajaonekana mahakamani sasa mtamuona,” amesema.
Mbowe amesema tangu Serikali irejeshe mikutano ya hadhara, (Januari 6, 2023) Chadema imekuwa ikitekeleza jukumu hilo sambamba na kufanya maandamano, akisema hawakuwahi kumdhuru mtu au kuharibu mali zozote akisisitiza chama hicho, si cha kigaidi.
Mbowe amesisitiza akisema, “tutawashtaki wao kama wao, hatutaki mawakili wa Serikali waje kuingilia, tunataka tushughulike na wao, watuambie matendo yao yalikuwa halali kiasi gani, kama siyo halali, watueleze nani aliyewatuma,” amesema.
Mbowe amesema wanamshtaki Nyahoza kwa sababu barua aliyoiandikia Chadema Agosti 8, ndiyo chimbuko la sintofahamu iliyosababisha viongozi na makada wa chama hicho, kukamatwa na kuumizwa.
Barua hiyo iliyosainiwa na Nyahoza ilisema kilichoelezwa na Mwaipaya katika tangazo la kuelekea shughuli hiyo kinakiuka matakwa ya kifungu cha 6A na 9(2) vya Sheria ya Vyama vya Siasa.
Katika barua hiyo, yalinukuliwa maneno ya Mwaipaya yaliyoelezwa kuvunja sheria hiyo: “Siku ya Agosti 12, waje washuhudie vijana wote nchi nzima tunakutana Mbeya, siku hiyo ni siku ya kwenda kuweka hatima ya Tanzania… tupo ‘serious’ sana na jambo hili.
“Vijana wa Chadema kama ambavyo vijana wa Kenya wamejitambua, tunakwenda kuacha uteja wa Serikali na kuweka maazimio makubwa ya uchaguzi wa Serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2025,” imeeleza sehemu ya barua hiyo ikimnukuu Twaha Mwaipaya, ambaye ni mratibu wa uhamasishaji wa Bavicha Taifa.
Hata hivyo, Mbowe amesema si kweli Bavicha walikuwa na nia kama ilivyoelezwa na Nyahoza, akidai suala hilo lilitangazwa hadharani na Mwaipaya si kwa kificho ili mamlaka husika kusikia na kujirekebisha.
Kwa mujibu wa Mbowe, si mara ya kwanza kwa Bavicha kukutana kama ilivyokuwa miaka iliyopita na kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu.
Kuhusu Awadhi, Mbowe amedai kiongozi huyo ndiye aliyekuwa mstari wa mbele katika kukamatwa na kuumizwa kwa makada na viongozi wa Chadema kutokana na maelekezo kwa askari wa chini yake walioyatekeleza na kusababisha maumivu kwa Chadema.
“Mnyika na Sugu wamepigwa na polisi, baada ya kukamatwa, kawaida polisi inatumia nguvu pale mtu anapolizuia Jeshi la Polisi kutekeleza wajibu wake, lakini hawa viongozi wetu hakuna aliyepinga, bali walijikabidhi na kupigwa ndani ya magari ya polisi,” amedai Mbowe.
Katika hatua nyingine, Mbowe amesema viongozi wote waliofunguliwa mashtaka hewa hawataenda kuripoti kituo cha Polisi.
“Viongozi wote tuliofunguliwa mashtaka hewa hatutakwenda polisi kuripoti, sasa wakitaka kuchukua hatua nyingine wachukue, sisi tunasema hatutakwenda polisi kufuata mashtaka hayo,” amesema.
Katika mkutano huo, Lissu na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika wamesimulia namna walivyopigwa na kusafirishwa kupelekwa maeneo tofauti kabla ya kufikishwa Dar es Salaam na kuachiwa huru na Jeshi la Polisi.
Mbali ya hao, imeelezwa mwingine aliyekumbwa na kadhia hiyo ni Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Nyasa, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Joseph Mbilinyi maarufu ‘Sugu’.
Inadaiwa Sugu ndiye aliyekuwa wa kwanza kukumbwa na msukosuko huo.
Hata hivyo, Agosti 13, 2024 Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi, Awadhi Haji alipoulizwa juu ya madai ya viongozi hao wa Chadema alieleza kuhusu tukio hilo alishazungumzia mbele ya vyombo vya habari.
“Siwezi kuzungumzia tena tukio hilo, yote nilishayazungumzia (Agosti 12) katika mkutano wangu na waandishi wa habari na kama kuna suala lingine basi wafuate utaratibu katika kuwasilisha,” alisema Awadhi.
Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara) na Mnyika wamesimulia yaliyowafika baada ya kukamatwa mkoani Mbeya na Jeshi la Polisi wakidaiwa kukaidi zuio la kutofanyika kongamano kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani inayosheherekewa Agosti 12 ya kila mwaka.
Lissu amedai baada ya kuzingirwa na polisi katika ofisi ya kanda na giza kuingia ndipo sintofahamu ilipoanza akidai Kamishna Haji alipowasili aliamuru wakamatwe.
“Ilikuwa ni unyanyasaji, kwa sababu walimvuta Sugu hadi kumchania fulana yake, sasa baada ya hapo kipigo kikaanza kwa kutumia marungu ya umeme, watu walipigwa sana ilikuwa vurumai. Kilichotokea kwangu RPC (Kamanda wa Polisi wa Mkoa) wa Mbeya- Benjamin Kuzaga), alinitoa nje na kunikabidhi kwa mkuu wa upelelezi wa mkoa.
“Sasa huku nyuma niliacha kipigo kikiendelea, watu walipigwa sana, lakini ghafla nilikuja kuondolewa katika gari la RCO na kuamriwa nipande gari aina ya Pick-up ambayo sikuweza kuipanda kwa namna nilivyo, lakini nikajibiwa kama sina mguu nimekuja kutafuta nini hapa,” amedai Lissu.
Lissu amedai kwa vile hakuweza kupanda, askari waliamriwa wambebe na kumtupa ndani ya gari hilo na kuwekwa katika uvungu wa viti vya gari hilo. Amedai baada ya hapo alipelekwa mkoani Songwe katika kituo cha polisi cha Vwawa.
“Nilipofika niliwekwa mahabasu, kesho yake saa tisa jioni nilisafirishwa kuletwa Dar es Salaam. Nilifika Dar es Salaam saa 11 alfajiri katika kituo kikuu, nikajaza karatasi ya kujidhamini mwenyewe kisha nikapelekwa moja kwa moja nyumbani kwangu,” amedai Lissu.
Mnyika ambaye wakati anasogea kwenye kipaza sauti, alionekana akitembea kwa kuchechemea, amedai alivuliwa miwani iliyovunjwa na kutupwa chini na Awadhi aliyemwambia viongozi hao wamekuwa wakisumbua.
“Kwa kauli hii ya Haji ilikuwa kama ishara kwa polisi kikosi cha kutuliza ghasia kunipiga, walinizunguka wakiwa na silaha nzito pamoja na kunishushia kipigo, kwa marungu na mabuti. Nilivyoona hali ile nikahisi hapa nitapata madhara makubwa kama si kifo.
“Kwa hiyo kujiokoa nikaamua kupiga kelele za mnaniua, mnaniua kwa sauti kubwa, wakaamua kunibeba na kunitupa katika gari ambapo pembeni yangu alikuwapo Sugu ambaye hakuwa katika hali nzuri baada ya kipigo,” amedai.
Mnyika amedai wakati wanasafirishwa kutoka Mbeya kwenda Njombe na Iringa walilazwa chali na hawakutakiwa kuinuka kwa jambo lolote, akidai wakati safari ikiendelea Sugu alizidiwa na kulia kutokana na maumivu.
“Niliwaambia askari kuwa Sugu hali siyo nzuri, wakaniambia ajikaze safari bado. Nilipofika Makambako nilitengenishwa na Sugu aliyepelekwa Iringa,” ameeleza.
Ilivyokuwa Ofisi za Chadema
Kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari, kulifanyika mkutano wa ndani uliodumu kwa nusu saa ukianza saa 8:40 mchana hadi saa 9:10 alasiri, uliojumuisha baadhi ya viongozi wa Kamati Kuu ya chama hicho, wakiwamo Mbowe, Lissu, Mnyika na Godbless Lema.
Wakati wakiendelea na mkutano wa ndani, wanachama na makada wa Chadema waliendelea kukusanyika katika ofisi hizo na kuketi makundi wakijadiliana.
Baadaye viongozi wa kamati kuu walitoka ndani ya ofisi waliyokuwa wakifanya mkutano huo wa ndani kwenda kuzungumza na waandishi wa habari pamoja na wanachama waliojitokeza kusikiliza ujumbe wa viongozi wao.
Mnyika alitoka akiwa anachechemea, mkono wa kulia ulikuwa umeshikwa na Mbowe aliyemsaidia kuruka kwenye ngazi na upande wa kushoto alikuwa Lissu.
Mnyika aliyekuwa amevaa viatu vya wazi, mguu wa kulia muda mwingi alikuwa akiuning’iniza juu.
Wakati viongozi hao wakizungumza na waandishi wa habari, makada wa chama hicho waliokuwepo muda mwingi walikuwa wakisikika wakiguna.