Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Afya kuongeza vituo vya huduma za uchunguzi na utambuzi wa mapema wa ugonjwa wa usonji na matatizo mengine yanayoweza kubainika, watoto wanapohudhuria kliniki kila mwezi.
Wakati kati ya watoto 160 mmoja ana usonji, takwimu za kwenye vituo vya huduma za afya na shuleni zinaonyesha ni takribani watoto 2000 pekee, ndio wanaopatiwa huduma.
Ukilinganisha na hali ya uzazi nchini ambapo jumla ya wanawake milioni 2.4 hujifungua kila mwaka na kwa makadirio ya Shirika la Afya Duniani (WHO), kila mwaka watoto zaidi ya 15,000 huzaliwa na tatizo la usonji kwa viwango tofauti.
Majaliwa ametoa agizo hilo leo Jumapili, Aprili 28, 2024 alipokuwa akizungumza baada ya kushiriki mbio fupi za hisani za Run 4 Autism Tanzania, zilizofanyika katika viwanja vya The Green Ground Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Majaliwa amesema kwa kufanya hivyo wataweza kuwabaini watoto wenye changamoto mapema na hivyo kuwaanzishia matibabu.
“Wizara ya Afya na Tamisemi zihakikishe uwepo wa huduma jumuishi zinazoweza kuleta tija kwa kinamama na watoto, wanazaliwa na magonjwa ambayo yanaweza kubainika mapema,” amesema.
Ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, iendelee kongeza kasi ya upanuzi wa utoaji wa huduma za elimu jumuishi pamoja na kuongeza wigo wa mafunzo na vyumba vya madarasa katika shule ili watoto wenye ulemavu wasitembee umbali mrefu kwenda shule.
Majaliwa amewataka wazazi na walezi wenye watoto walio na changamoto za ukuaji au uelewa, watafute ushauri kwa wataalamu wa afya ili kufaidika na huduma zilizopo wakiwa katika umri mdogo.
“Wataalam wetu muendelee kuongeza juhudi katika kuelimisha jamii kuhusu magonjwa haya, ili watu wengi zaidi waweze kunufaika na huduma,” amesema.
Ameitaka jamii ya Watanzania kuacha kuwanyanyapaa watoto na watu wanaoishi na usonji, magonjwa ya mfumo wa fahamu pamoja na matatizo ya akili.
Pia amevitaka vyombo vya habari, wasanii na wanajamii kwa ujumla, kutumia kila fursa kuielimisha jamii kuhusu masuala mbalimbali ya afya.
“Wanahabari tumieni kalamu zenu kuelimisha jamii kuhusu afya na udhibiti wa magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya akili,” amesema Majaliwa.
Naye, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Muhimbili (MUHAS), imeanzisha shahada ya kwanza ya sayansi ya mazoezi tiba ya kusaidia mawasiliano, tiba kazi, tiba viungo na shahada ya kwanza ya sayansi ya saikolojia ya kitabibu kuanza mwaka huu 2024.
“Lengo la kuanzishwa kwa shahada hizi ni kuhakikisha, huduma za utengemao zinapewa kipaumbele cha juu na Serikali,” amesema.
Waziri Ummy amesema, Serikali inaendelea kufanya juhudi za kutatua changamoto za watu wenye usonji ambapo amebainisha miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na upungufu wa wataalamu wa mazoezi tiba pamoja na gharama za mazoezi tiba.
“Tunategemea pia kuanzisha fani hizi katika ngazi za diploma kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa kuwa nchi ni kubwa, ili tuweze kuwa na watalaam wengi zaidi wa masuala haya katika ngazi za vituo vya afya na hospitali za wilaya kote nchini,” amesema Waziri Ummy.
Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Lukiza Autism Foundation ambao ndio waandaaji wa mbio hizo, Hilda Nkabe amesema lengo la mbio hizo ni kuchangisha fedha kiasi cha Sh50 milioni kwa ajili ya kutekeleza mkakati wa miaka mitano kuanzia 2024 hadi 2028 wenye lengo la kukuza ustawi wa kila mtoto mwenye viashiria vya usonji.
“Mkakati huu ni kwa ajili ya kuongezea nguvu mipango ya Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Afya kwa kuboresha uwezo wa walimu wa shule za chekechea, katika kubaini viashiria vya usonji kwa watoto.”