Angalizo la uvuvi haramu latolewa Ziwa Tanganyika likifunguliwa kesho

Kigoma. Ikiwa imebaki siku moja kabla ya Ziwa Tanganyika kufunguliwa baada ya kufungwa kwa miezi mitatu tangu Mei 15, 2024, baadhi ya wavuvi mkoani Kigoma wameiomba Serikali kuendeleza hatua za kudhibiti uvuvi haramu kabla ya kuruhusu uvuvi kuanza.

Serikali ilisitisha shughuli za uvuvi katika ziwa hilo linalozunguka mikoa ya Kigoma, Katavi, na Rukwa hadi Agosti 15, 2024, ili kuruhusu samaki kuzaliana na kuongeza tija kwa wavuvi wanaofanya shughuli zao ziwani humo.

Akizungumza leo Jumatano, Agosti 14, 2024, mvuvi anayefanya kazi ndani ya ziwa hilo, Kasia Hamimu, alisema Serikali isifungue ziwa hilo bila kuweka utaratibu mzuri wa kuvua samaki.

Amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha zana za uvuvi zisizotakiwa zinadhibitiwa ndani ya Ziwa Tanganyika kwani zinasababisha kupungua kwa mazalia ya samaki.

“Kilichotufikisha hapa hadi ziwa likafungwa ni uvuvi haramu na kupungua kwa mazao ya uvuvi ziwani. Ziwa likifunguliwa, Serikali iweke utaratibu wa kudhibiti zana za uvuvi zitakazoingia ziwani. Sio kila mtu anaingia na kuvua, hii itasaidia kuvua kwa malengo na kukomesha uvuvi haramu,” alisema Hamimu.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amesema uamuzi wa Tanzania wa kusitisha shughuli za uvuvi ziwani humo ulitokana na makubaliano yaliyoazimiwa katika kikao kilichofanyika mwaka 2022, kikihusisha nchi zinazozunguka ziwa hilo ambazo ni Zambia, Tanzania, Burundi, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Ulega amesema uamuzi huo ni utekelezaji wa Mkataba wa Kikanda wa Nchi Wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika unaoweka hatua na taratibu za usimamizi endelevu wa shughuli za uvuvi katika ziwa hilo.

Waziri huyo amesema baada ya utafiti kubainisha upungufu mkubwa wa samaki na dagaa katika Ziwa Tanganyika, unaotokana na ongezeko la uvuvi usio endelevu, ulisababisha uharibifu wa mazalia ya samaki.

Mwenyekiti wa Wavuvi Mkoa wa Kigoma, Francis John, amesema walikuwa wanasubiri kwa hamu siku ya kufunguliwa ziwa hilo, akiamini Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi tayari ina mikakati ya kudhibiti uvuvi haramu.

“Tunafurahi siku tuliyokuwa tunaisubiria kwa muda mrefu imefika. Tunaamini Serikali itaweza kuwa na mikakati ya kukomesha uvuvi haramu katika ziwa letu, uvuvi ambao umetusababishia kuwa hapa na ziwa kufungwa. Na kama haitafanya hayo, basi itakuwa imefanya kazi bure kwa kipindi cha miezi hii yote,” alisema John.

Mchuuzi wa samaki na dagaa, Shaban Hamisi, amesema amefurahi kuona siku ya kufunguliwa ziwa hilo imefika, kwa sababu alikuwa hana biashara nyingine ya kufanya baada ya kufungwa na kusababisha maisha yake kuwa magumu hivyo kushindwa kuhudumia familia yake.

Amesema wamezoea kuvua na kuuza samaki na dagaa kwa maisha yote kwani tangu alipokuwa mdogo, aliwaona wazazi wake wakitumia ziwa hilo.

Amesema ilikuwa vigumu kukubaliana na hali halisi lakini sasa wamefarijika na kuwa na matumaini ya maisha kama awali.

Naye mlaji wa mazao ya uvuvi, Rusha Rashid, alisema alikuwa na wakati mgumu hadi kuzoea hali ya kukosa kula samaki na dagaa wa Kigoma kwa siku.

Alisema ni kitoweo walichozoea kukitumia na familia yake, hivyo kufunguliwa kwa ziwa hilo kesho ni ahueni kwake na familia yake.

Related Posts