Robertinho alivyomuachia gundu Benchikha | Mwanaspoti

KOCHA wa Simba, Abdelhak Benchikha, anatarajiwa kuachana na klabu hiyo leo baada ya kusimamia mechi yake ya mwisho ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Azam FC katika fainali ya Kombe la Muungano jana akitwaa ubingwa wa michuano hiyo kwenye Uwanja New Amaan Complex, Zanzibar.

Taarifa za ndani zinasema Simba wakati wowote itatangaza kumuaga Benchikha anayeondoka ili kwenda kushughulikia mambo ya kifamilia ikisemekana anauguliwa na mkewe.

Benchikha anaondoka akiwa ameiongoza Simba katika mechi 12 za Ligi Kuu, lakini takwimu zinaonyesha mtangulizi wake, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyeachana na timu hiyo Novemba 7, 2023 baada ya kipigo cha 5-1 kutoka kwa Yanga, bado ana rekodi bora zaidi ya mwalimu huyo uraia wa Ubelgiji mwenye asili ya Algeria. 

Aprili 20, 2024, Yanga ilikuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Mkapa na kuifunga Simba 2-1, mabao yaliyofungwa na Aziz KI kwa mkwaju wa penalti dakika ya 20 na Joseph Guede dakika ya 38. Ushindi huo umepunguza kwa kiasi kikubwa matumaini ya Simba kwenye kuchukua ubingwa wa ligi msimu huu.

Mwanaspoti linakuchambulia mechi 12 za makocha wawili wa Simba, Robertinho na Benchikha, ambaye nafasi yake inatarajiwa kukaimiwa na Suleiman Matola wakati Wekundu wa Msimbazi wakisaka mrithi wake.

TAKWIMU ZA ROBERTINHO
Takwimu za makocha hawa wawili kwenye mechi 12 za mashindano ya ndani na kimataifa, yanaonekana kumbeba zaidi Robertinho.

Katika mechi 10 za Ligi Kuu Bara alizosimamia Robertinho, Simba ilishinda mechi saba, sare zikiwa mbili na alipoteza mchezo mmoja tu dhidi ya Yanga aliofungwa 5-1 na kufutwa kazi.

Alianza na Mtibwa Sugar 2-4, Dodoma Jiji 0-2, Coastal Union 0-3, Ihefu 0-2, Azam 1-1, Namungo 1-1.

Kwenye mashindano ya Kombe la ASFC, Robertinho aliishia hatua ya nusu fainali kwa kutolewa na Azam kwa jumla ya mabao 2-1, pia amechukua Ngao ya Jamii mbele ya Yanga, akiibwaga kwa mikwaju ya penalti 3-1 baada ya muda wa kawaida matokeo kuwa suluhu.

Wakati Robertinho anatua Simba Januari 03, 2023, aliikuta tayari timu hiyo imeingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuiongoza kutinga robo fainali ya michuano hiyo, wakitolewa na Wydad AC kwa mikwaju ya penalti 3-2 baada ya sare ya jumla kuwa 1-1.

Mechi nane za Ligi ya Mabingwa Afrika, alishinda tatu na kupoteza tatu hatua za makundi na kuweka rekodi ya aina yake kwa kuichapa Horoya mabao 7-0 kwenye Uwanja wa Mkapa, huku robo fainali akishinda moja na kupoteza moja.

TAKWIMU ZA BENCHIKHA
Ni kama Robertinho amemuachia gundu Benchikha kwani tangu ajiunge na Wekundu wa Msimbazi, Novemba 24, 2023, amecheza michezo 12 ya mashindano yote, ushindi saba, kapoteza mbili na sare tatu.

Sare tatu ilizopata Simba kwenye ligi ni ya 1-1 dhidi ya Azam Februari 09, 1-1 na Ihefu, Aprili 13 na 2-2 dhidi ya KMC Septemba 23 mwaka jana huku ikishinda dhidi ya Mashujaa 0-2, 1-0 na JKT, 3-1 Singida Big Stars, 1-0 na Geita Gold na kimataifa akishinda 6-0 vs Jwaneng Galaxy, 2-0 dhidi ya Wydad AC.

Alianza kwa kupoteza dhidi ya Tanzania Prisons kwa mabao 2-1, Machi 06, 2024, kisha Aprili 20, 2024 dhidi ya Yanga (2-1) na kurudisha rekodi ya Yanga kuifunga Simba nyumbani na ugenini ndani ya msimu mmoja wa ligi kama ilivyotokea mara ya mwisho msimu wa 2014-15.

Kimataifa alitolewa katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri, kwa jumla ya mabao 3-0, akifungwa 1-0 nyumbani na 2-0 ugenini, kisha kutolewa Kombe la ASFC hatua ya 16 bora na Mashujaa kwa penalti 6-5.

Tangu Robertinho aachane na Simba, timu hiyo imekuwa ikisuasua kupata matokeo mazuri na kuonekana dhaifu kuliko misimu miwili iliyopita ikiruhusu mabao 21 katika mechi 21 za Ligi Kuu Bara, rekodi ambayo mara ya mwisho ilitokea msimu wa 2019-20 tena kipindi hicho ligi ikiwa na timu 20 na mechi zilizochezwa ni 38.

KIKOSI
Kikosi cha kwanza cha Simba hivi sasa hakijatofautiana sana na kile alichokiacha Robertinho ambaye kwa asilimia kubwa wachezaji wanaotumika sasa ni walewale, Clatous Chama, Kibu Denis, Henock Inonga, Saido Ntibazonkiza na Che Malone.

Utofauti ulikuwa kwenye eneo la mastraika ambao Robertinho alikuwa akiwatumia Moses Phiri, John Bocco na Jean Baleke, wakati Benchikha anawatumia Pa Omar Jobe na Fredy Koublan kwani Phiri na Baleke wameondolewa moja kwa moja, huku Bocco akiwekwa kando.

Eneo jingine ni kiungo mkabaji ambapo kwa sasa Babacarr Sarr anacheza baada ya kusajiliwa katika dirisha dogo na kumuweka benchi Mzamiru Yassin aliyekuwa kipenzi cha Robertinho.

Baada ya Aishi Manula kuumia, kwa sasa chaguo namba moja la Benchikha golini ni Ayoub Lakred ambaye kwa Robertinho akimkosa Manula humchezesha Ally Salim.

Related Posts