WATENDAJI VILABU VYA LIGI KUU WANUFAIKA NA ELIMU YA HIFADHI YA JAMII KUTOKA NSSF

*Karia avitaka vilabu vyote ligi kuu kuchangamkia fursa ya kujiwekea akiba

*NSSF waeleza namna  watakavyonufaika kupata mafao, matibabu

Na MWANDISHI WETU,
Dar es Salaam. Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bw. Wallace Karia amevitaka vilabu vinavyoshiriki ligi kuu Tanzania Bara kuwaandikisha wachezaji, makocha na wafanyakazi wao katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili waweze kunufaika na mafao mbalimbali yanayotolewa na Mfuko huo ikiwemo matibabu.

Bw. Karia amesema hayo tarehe 14 Agosti 2024 wakati akifungua semina kwa watendaji wakuu wa vilabu vinavyoshiriki ligi kuu, ambayo imeandaliwa na TFF, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPBL) pamoja na NSSF, iliyofanyika katika ukumbi wa Mafao House Ilala, Dar es Salaam.

Amesema zipo faida nyingi za wachezaji na wadau wengine wa mpira kujiunga na kuchangia NSSF ikiwemo kupata mafao pamoja na huduma za matibabu na wategemezi wao na kuwa jambo hilo litawasaidia kipindi ambacho hawana nguvu za kucheza mpira.

Bw. Karia amevitaka vilabu vyote kuchangamkia fursa hiyo yenye manufaa kwa wachezaji, na kuwa vielekeze nguvu zaidi ya kuandikisha NSSF wachezaji vijana walio chini ya umri wa miaka 20 ili wanapostaafu mpira wanufaike na pensheni ya uzeeni inayotolewa na NSSF.

“Tunawashukuru wenzetu wa NSSF kwa kuja na jambo hili kwetu sisi litatuepusha na zile lawama tulizokuwa tunatupiwa ambazo hazituhusu za wachezaji wa zamani kuishi maisha magumu kwa kukosa kukidhi gharama za matibabu na gharama za maisha, angalau sisi tunaosimamia mpira tutahakikisha wachezaji wanaocheza kipindi hiki wasipate changamoto ambazo wanazipata wenzao,” amesema Bw. Karia.

Naye, Bw. Cosmasi Sasi, Meneja Uandikishaji, Ukaguzi na Michango wa NSSF, amesema kwa mujibu wa mabadiliko ya sheria ya hifadhi ya jamii sura ya 50 ya mwaka 2018, NSSF ndio Mfuko pekee uliopewa jukumu la kuandikisha wanachama waliopo katika sekta rasmi na sekta isiyo rasmi wakiwemo wachezaji wa mpira pamoja na wajasiriamali wengine wote.

“Lengo la NSSF ni kuwafikia wafanyakazi waliopo katika sekta binafsi na tayari kazi hiyo tunaifanya kwa njia mbalimbali, lakini ili tuweze kumfikia kila mmoja tuna jukumu la kutoa elimu ya hifadhi ya jamii, mafao tunayotoa na faida zake. Tunashukuru kupata fursa hii ya kujumuika na wenzetu TFF, TPBL pamoja na watendaji wakuu wa vilabu vinavyoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kwa lengo la kutoa elimu hii ili waweze kujiunga na kuchangia,” amesema Bw. Sasi.

Amesema wachezaji na watendaji wa vilabu vya mpira ni wadau muhimu ambao wanatakiwa wapate kinga ya hifadhi ya jamii ili waweze kunufaika moja kwa moja kipindi ambacho hawana uwezo wa kucheza mpira kwa kupata mafao yatakayowasaidia kuishi maisha bora uzeeni.

Bw. Sasi amesema sheria ya NSSF imezungumzia mahususi wanaopaswa kujiunga na Mfuko kuwa ni wafanyakazi wote walioajiriwa katika sekta binafsi, raia wa kigeni wanaofanya kazi Tanzania bara, watumishi wa taasisi za kimataifa zinazofanya kazi Tanzania bara na watu waliojiajiri katika sekta isiyo rasmi.

“Tutahakikisha elimu ya hifadhi ya jamii inawafikia wana michezo wote hata waliopo vilabu vya chini, lengo waweze kujiunga na kujiwekea akiba kwa ajili ya kesho yao iliyokuwa njema,” amesema Bw. Sasi.

Naye, Meneja wa NSSF Mkoa wa Temeke, Bw. Ferouz Mtika ameishukuru Bodi ya Ligi, TFF na vilabu vya mpira wa miguu kwa kushiriki semina hiyo yenye lengo la kupata elimu ya hifadhi ya jamii.

Related Posts