Leonel Ateba ana kibarua kigumu cha kuthibitisha kuwa Simba haijakosea kumsajili kwa gharama kubwa juzi akitokea USM Alger kutokana na takwimu zake za ufungaji kuonyesha hazijatofautiana sana na zile za Freddy Koublan na Steven Mukwala ambao kocha Fadlu Davids ameonyesha kutoridhishwa nao.
Simba ilikamilisha kwa haraka uhamisho wa Ateba kwa gharama zinazotajwa kufikia Dola 200,000 baada ya kufikia makubaliano na USM Alger ya Algeria ambayo mshambuliaji huyo wa Cameroon ameichezea kwa miezi sita tu tangu alipojiunga nayo kutokea Union Douala, Januari mwaka huu.
Katika kipindi cha nusu msimu alichoitumikia USM Alger, Ateba amecheza idadi ya mechi 19 za timu hiyo ya Algeria. Ameifungia mabao matatu tu huku akitoa pasi nane za mwisho katika mashindano tofauti ambayo imeshiriki.
Kabla ya hapo, katika nusu msimu aliochezea Douala, Ateba aliifungia mabao saba hivyo kiujumla msimu uliopita alipachika mabao 10.
Freddy Koublan, katika nusu msimu uliopita alipochezea Simba, aliifungia mabao nane, sita yakiwa kwenye ligi na mawili ya mashindano mengine lakini kabla ya hapo, katika ligi ya Zambia alikotoka, kwa nusu msimu alipachika mabao 11 na hivyo kwa msimu uliomalizika alifunga mabao 19, tisa zaidi ya yale ya Ateba.
Kwa msimu uliopita, Mukwala katika Ligi ya Ghana alifunga idadi ya mabao 14 katika michezo 28 na hivyo anamzidi Ateba kwa mabao manne.
Msimu ambao Ateba alikuwa moto wa kuotea mbali katika ufungaji ni 2020/2021 ambapo aliifungia Coton Sports mabao 13 na kupiga pasi saba za mwisho katika mechi 28 na baada ya hapo hajawahi kufunga zaidi ya mabao 10 kwa msimu mmoja.
Uamuzi wa Simba kumsajili Ateba umetokana na mapendekezo ya benchi lake la ufundi chini ya Fadlu Davids ambaye baada ya Simba kupoteza dhidi ya Yanga kwa bao 1-0 katika mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii, Alhamisi iliyopita alisema anahitaji mshambuliaji wa kati ili kuwaongezea nguvu waliopo.
“Kama ambavyo nilisema kwenye ‘interview’ (mahojiano) zangu zilizopita bado tuna shida kwenye eneo la ushambuliaji. Siridhishwi na hali ya sasa na klabu inapambana kupata mshambuliaji anayekidhi zaidi ila kama hatopatikana nitaendelea kupambana na hawa waliopo,” alisema Davids.
Lakini mbali na kuthibitisha kuwa Simba haikukosea kutumia kiasi kikubwa cha fedha kumsajili, Ateba anakabiliwa na kibarua kigumu cha kumaliza nuksi ya misimu mitatu mfululizo ambayo imewakumba washambuliaji wa kati wa Simba.
Kuanzia msimu wa 2021/2022 hadi uliopita wa 2023/2024, washambuliaji wa kati wa Simba wameonekana kuwa na ubutu jambo ambalo limeilazimisha timu hiyo kuingia sokoni kusajili mchezaji wa nafasi hiyo katika kila dirisha la usajili.
Kwa misimu mitatu iliyopita, hakuna mshambuliaji wa kati wa Simba ambaye alifanikiwa kufunga zaidi ya mabao 10 kwenye ligi.
Katika msimu uliopita, mshambuliaji wa kati wa Simba aliyepachika mabao mengi alikuwa ni Jean Baleke ambaye alifumania nyavu mara nane na alipoondoka katika dirisha dogo, aliletwa Koublan aliyefunga mabao sita.
Msimu wa 2022/2023, mshambuliaji wa kati wa Simba aliyefumania nyavu mara nyingi alikuwa ni Moses Phiri aliyemaliza akiwa na mabao 10 akifuatiwa na John Bocco aliyefunga mabao tisa.
Katika msimu wa 2021/2022, Meddie Kagere ndiye alimaliza akiwa kinara kwa upande wa washambuliaji wa kati ambapo alifunga mabao saba.
Msimu wa mwisho kwa washambuliaji wa kati wa Simba kutamba ulikuwa ni 2020/2021 ambao John Bocco alipachika mabao 16 na aliyemfuatia alikuwa ni Chris Mugalu aliyefunga mabao 15.
Ikumbukwe msimu huo, Bocco alimaliza akiwa kinara wa ufungaji kwenye Ligi Kuu kwa mabao hayo 16.
Mchambuzi wa soka, Geoffrey Lea alisema kuwa usajili wa Ateba unaonekana ni matokeo ya presha ambayo uongozi wa Simba umepata kutoka kwa mashabiki.
“Namba za Fredy zinaashiria ni mshambuliaji mzuri anayehitaji kuaminiwa. Shida ya viongozi wa Simba ni kucheza ngoma wanayopigiwa na watu wasiohusika kisha wao wanakubali kuicheza ngoma hiyo,” alisema Lea.