Gamondi apewa ramani kwa Pacome mjipange

IKIWA imebaki siku moja tu kabla ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025 kuanza, kiungo mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua amesema ajipanga kivingine kulinda kibarua alichokianza tangu msimu uliopita na kwamba ubora wa mastaa unavyoleta presha mpya ya nafasi naye yupo tayari kupambana kuendeleza moto.

Staa huyo, aliyetua Yanga msimu uliopita akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast kwa mkataba wa miaka miwili unaomalizika msimu huu, aliliambia Mwanaspoti ana kiu ya kufanya makubwa zaidi akiwa na Yanga hjususani katika mechi za kimataifa atakazoshiriki kwa msimu wa tatu mfululizo moja akiwa na Asec.

Awali, Mwanaspoti iliwahi kuhabarisha umma kwamba, Yanga ilikuwa na mazungumzo ya kumuongeza mkataba mpya baada ya kuonyesha kiwango bora ila dili hilo halikufika tamati, ingawa hadi sasa bado hakijaeleweka, lakini Pacome alisema, msimu huu iwapo hatapata majeraha anataka kufanya makubwa zaidi.

Alisema msimu uliopita ukiwa ni wa kwanza Yangam hakuitumikia timu hiyo ipasavyo baada ya kuumia mwishoni mwa msimu, lakini ubora wa kikosi hicho msimu huu unampa msukumo mkubwa kujituma zaidi.

“Kila mchezaji wa kikosi chetu hataki kufanya makosa anapopewa nafasi kwani wote ni bora, jambo ambalo linaongeza ushindani mkubwa zaidi,” alisema Pacome na kuongeza; “Sioni kama kuna jambo litatushinda msimu ujao, kwani mipango yetu sio kubeba makombe tu kama tulivyoanza na Ngao ya Jamii tuliyoikosa mwaka jana, pia kuwafurahisha mashabiki na viongozi kwa ujumla.”

Pacome aliyemaliza na mabao saba na asisti nne katika Ligi Kuu na mengine matatu katika Ligi ya Mabingwa Afrika, alishindwa kumaliza msimu vizuri kwa kusumbuliwa na majeraha ya muda mrefu yaliyomfanya kukosa mechi za ligi na ile ya robo fainali ya CAF dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Kwa msimu mpya wa Ligi ya CAF, Yanga itaanza na dhidi ya Vital’O ya Burundi , wikiendi hii na kwa Ligi Kuu Bara itashuka baada ya mechi hizo za kimataifa Agosti 29 dhidi ya Kagera Sugar ikiwa ugenini.

Related Posts