Dodoma. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema licha mvua zinazoendelea kunyesha nchini, Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) lipo salama kwasababu limejengwa kisayansi.
Mbali na hilo, amesema bwawa hilo linaendelea kuzalisha umeme kupitia mtambo namba tisa huku mitambo mingine miwili ikiwa ukingoni kukamilika.
Amesema hayo leo Alhamisi Aprili 18, 2024 wakati akizungumza kwenye Maonesho ya Wiki ya Nishati 2024 yanayoendelea kwenye Viwanja vya Bunge jijini Dodoma.
Amesema ujazo wa bwawa hilo ni mita za ujazo 183 na kwamba takwimu za leo zinaonyesha kuwa lina mita za ujazo 183.4.
Amesema awali, maji yalikuwa yakiingia mengi kwa kiasi cha mita za ujazo 8,400 kwa sekunde na yalipaswa kupunguzwa ili kuendana na ujazo wa bwawa.
“Kama kusingekuwa na bwawa basi mafuriko yangekuwa yameshaanza tangu Oktoba mwaka jana lakini kwa sababu ya uwepo wa bwawa, limetumika kupunguza makali,” amesema Dk Biteko.
Amesema bwawa hilo limetoa mchango mkubwa katika kupunguza mafuriko katika maeneo ya Mkoa wa Pwani.
“Mimi kwa kweli inanisikitisha tumepoteza ndugu zetu, tumeharibiwa mali zao, mashamba yameharibiwa, watu wengi hawana mahali pa kulala na ndio maana Serikali inafanya kila jitihada kurejesha hali zao bila kuchelewa,”amesema.
Dk Biteko amesema wanavyoangalia ukuaji wa uchumi nchini unaenda kwa kasi kubwa, hivyo ni lazima kuwepo kwa vyanzo vingine vya umeme nchini mbali na bwawa la Mwalimu Nyerere.
Amesema kwa kubaki na vyanzo vilivyopo vya uzalishaji umeme ikiwamo bwawa hilo tu, itakuwa ni likizo ya miaka 10 tu kabla ya kurejea tena kwa mgawo wa umeme.
Dk Biteko amesema wanachotaka ni kuongeza vyanzo vingine vya umeme ili kuendana na kasi ya ukuaji wa uchumi na ongezeko la viwanda Tanzania.
Amesema viwanda vingi vinavyojengwa vinahitaji umeme na kwamba Reli ya Kisasa (SGR) yenyewe tu inahitaji Megawati 80 kujiendesha.
“Maana yake kuwa ni mtambo mzima wa Mtera (Bwawa la kuzalisha umeme kwa kutumia maji) unatoisha kuendesha SGR. Tunavyo viwanda ambavyo kiwanda kimoja kinahitaji Megawati nane na Megawati nane ni umeme unaotosha katika baadhi ya mikoa,”amesema.
Dk Biteko amesema watu wengi bado wanatumia nishati isiyo safi ya kupikia kama vile mkaa na kuni na wananchi wachache wanatumia gesi na nishati nyingine kama vile umeme.
Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa ndani ya miaka 10 asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.
Amesema Serikali imepitisha Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia ikiwa ni moja ya njia za utekelezaji wa ajenda hiyo ambayo inanadiwa na kinara wake, Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema katika kutekeleza mpango huo wa Nishati Safi ya Kupikia, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, imeshatoa waraka wa kutotumia kuni na mkaa kwa taasisi zinazolisha watu kuanzia 100 na zaidi kama vile shule na magereza.
Uboreshaji wa miundombinu
Dk Biteko amesema kuwa kwa sasa uzalishaji umezidi mahitaji hivyo kinachofanyika sasa ni kuboresha miundombinu ya umeme nchini.
Amesema miundombinu hiyo ni pamoja na usafirishaji wa umeme kwa kuwa baadhi ya sehemu laini za umeme ni ndefu sana hivyo vitajengwa vituo vya kupoza umeme takriban 83 nchini ili kuondoa athari za watu wengi kutopata umeme pale laini inapopata hitilafu.
Dk Biteko amekiri bei ni kubwa na kuwa Serikali inaangalia kwa karibu sana suala hilo ili kuweza kupunguza gharama.
Amesema suala hilo haliishii kwenye gesi pekee bali kwenye majiko banifu.
Dk Biteko amesema katika mwaka huu wa fedha Serikali itaanza kutengeneza majiko ya bayogesi kwenye nyumba za wananchi wanaofuga mifugo ili watumie nishati hiyo kwa ajili ya kupikia.