Dar es Salaam. Wizara ya Afya imesema hadi kufikia jana, Aprili 27 wasichana zaidi ya milioni 4 wenye umri wa miaka 9 hadi 14 wamechanjwa chanjo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi ( ‘HPV Vaccine’) Tanzania bara na visiwani.
Chanjo hiyo iliyotarajiwa kuwafikia wasichana 5,028,357 waliopo katika mikoa 31 na halmashauri 195 Tanzania bara na visiwani, kwa mujibu wa Wizara hiyo tayari asilimia 95 ya walengwa wamefikiwa, tangu kuanza kutolewa kwake Aprili 22, 2024.
Meneja Mpango wa Taifa wa Chanjo Dk Florian Tinuga amesema mpaka sasa uchanjaji umeonyesha mafanikio makubwa ikiwa ni wiki moja tu tangu kuanza kwake.
“Tulipoanza zoezi siku ya Jumatatu tulilenga kufikia watoto wenye umri wa miaka 9 hadi 14 takribani milioni tano, bara ni takribani milioni nne na laki nane na wengine waliobaki Zanzibar, ila hadi kufikia Aprili 27, 2023 tumefikia walengwa kwa asilimia 95,” amesema Dk Tinuga.
Dk Tinuga ameongeza kuwa kufanikiwa kwa lengo hilo, kumetoka na maamuzi ya kufanya mabadiliko ya kutoa dozi moja sahihi na kuweza kuwafikia mabinti wengi zaidi ambapo kwa siku ya kwanza pekee walichanja asilimia 27 huku lengo likiwa kila siku kuchanja asilimia 20.
Dk Tinuga ameongeza kuwa wasichana 4,841,298 wa Tanzania Bara na 187,059 wa Visiwani Zanzibar watafikiwa na chanjo hiyo kabla ya kufikia mwisho Desemba mwaka huu.
“Chanjo ni salama na hutolewa bure kwa walengwa kwa hiari na chanjo hiyo hupunguza uwezekano wa kupata saratani ya mlango wa kizazi, inapatikana katika vituo vya kutolea huduma za chanjo na hutolewa vituoni, kwenye jamii na shuleni na hutolewa wakati wa kampeni za kawaida,” amesisitiza Dk Tinuga.
Wataalamu wanaeleza kuwa chanjo ya kukinga inakusudiwa kuzuia msichana kupata maambukizi ya kirusi cha ‘human pappiloma virus HPV’ kinachombukizwa zaidi kupitia kujamiiana.
Hivi karibuni Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Hospitali ya Agakhan, Harrison Chuwa aliliambia Mwananchi sababu ya chanjo hiyo kupewa wasichana wenye umri mdogo;
“Katika jamii nyingi, wasichana hawatarajiwi kushiriki ngono kabla ya kuanza kwa hedhi ambayo ni karibu miaka tisa mpaka 13 kwa hivyo ni fursa nzuri zaidi ya kupata chanjo, yaani kabla ya kuwa na ari ya ngono,” alisema Dk Chuwa.
Alisema chanjo haitibu maambukizi ya virusi hivyo, kwa hivyo inahitajika msichana kuchanjwa kabla hajakabiliana na virusi hivyo.
“Hata msichana ambaye amepata kujamiiana anastahili chanjo, ingawa kwa kweli anatakiwa kupimwa kupitia kipimo cha HPV-DNA ili kuhakikisha kuwa hana maambukizi ndipo apewe chanjo,” alisema Dk Chuwa.
Licha ya mafanikio hayo, siku chache baada ya Serikali kuanza kutoa chanjo hiyo katika shule na vituo vya afya, baadhi ya maeneo kulikuwa na changamoto ya kukubali chanjo hiyo huku kukiwa na upotoshaji.
Baadhi ya walengwa, wazazi na jamii walionyesha wasiwasi juu ya watoto wao kupata chanjo hiyo wakidai kuwa zitawazuia kuzaa wakati utakapofika.
Wakizungumza na Mwananchi maeneo mbalimbali nchini, wengi waliitaka Serikali kuja na ufafanuzi wa kina kuhusu chanjo hiyo, ikiwemo kuhamasisha wazazi kuzungumza na binti zao kwani wengi hawana elimu.
Katika baadhi ya shule, watoto walikuwa wakikataa kuchanjwa, huku baadhi yao wakiomba ruhusa kuwasiliana na wazazi kabla.
Baadhi ya Watanzania ambao walitoa maoni yao katika mitandao ya kijamii walisema kuna ugumu kukubali chanjo ilhali hawajui manufaa yanayoweza kupatikana na iwapo chanjo hizo hazina madhara.
“Mfano chanjo hii ya saratani kuna taarifa kuwa mtoto akichanjwa hatakuwa na uwezo wa kuzaa, wanadai nchi zilizoendelea zina mpango wa kudhibiti idadi ya watu katika bara la Afrika hivyo wanatumia njia mbalimbali kuhakikisha idadi hiyo inapungua ikiwemo chanjo,” amesema Anna Maregesi mkazi wa Musoma mkoani Mara.