KLABU ya Simba muda wowote kuanzia sasa itatangaza kuachana na aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo Mualgeria, Abdelhak Benchikha ikiwa ni siku moja tangu atwae Kombe la Muungano lililohitimishwa jana visiwani Zanzibar.
Simba ilitwaa taji hilo baada ya kuifunga Azam FC bao 1-0, lililofungwa na kiungo wa kikosi hicho, Babacar Sarr katika dakika ya 77 na kuwapa Wekundu wa Msimbazi ubingwa wa sita wa michuano hiyo baada ya kulitwaa kuanzia mwaka 1993, 1994, 1995, 2001, 2002 na 2024.
Klabu hiyo inaachana na Benchikha kwa kile Mwanaspoti inachofahamu kwamba ni kutokana na matatizo yake ya kifamilia kwao Algeria na hivyo kudumu kwa siku 156 tangu alipotambulishwa Novemba 24, mwaka jana akichukua nafasi ya Robertinho Oliveira ‘Oliveira’.
Robertinho aliondoka Novemba 7, mwaka jana ikiwa ni muda mchache tangu timu hiyo ilipofungwa mabao 5-1 na Yanga na kuvunja rekodi ya kutopoteza tangu mara ya mwisho kikosi hicho kilipofungwa na Azam FC bao 1-0, Oktoba 27, 2022.
Tangu atambulishwe, Benchikha ameiongoza timu hiyo katika jumla ya michezo 21 katika mashindano mbalimbali ikiwemo ya Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ligi ya Muungano iliyorejea mwaka huu.
Katika Ligi Kuu Bara ameiongoza katika michezo 11 ambapo kati ya hiyo ameshinda sita, sare mitatu na kuchezea kichapo mara mbili huku akifunga jumla ya mabao 18 na kuruhusu nyavu za kikosi hicho kufungwa manane tu hadi sasa msimu huu.
Ni michezo miwili tu ya Ligi Kuu Bara ambayo Benchikha hakuiongoza Simba ambayo ni dhidi ya Coastal Union ambayo timu hiyo ilishinda mabao 2-1 (Machi 9, 2024) na ushindi wa 3-1 mbele ya Singida Fountain Gate uliopigwa Machi 12, mwaka huu.
Sababu za kukosekana kwake katika michezo hiyo ni kutokana na kwenda kwao Algeria kwa ajili ya kushiriki kozi ya ukocha ya siku tano.
Kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Afrika aliiongoza katika michezo saba ambapo kati ya hiyo alishinda miwili, sare miwili na kupoteza mitatu huku kiujumla ikifunga jumla ya mabao manane na kuruhusu nyavu zake kutikishwa mara nne tu.
Michuano mingine ni katika Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ambapo Benchikha alijikuta akitolewa mapema tu hatua ya 16 bora dhidi ya Mashujaa ya mkoani Kigoma baada ya timu hizo kufunga bao 1-1, kisha kuaga kwa changamoto ya penalti 6-5.
Katika Kombe la Muungano lililorejea mwaka huu baada ya kusimama kwa miaka 22, Benchikha aliiongoza timu hiyo katika michezo yote miwili na kushinda yote akianza na 2-0, dhidi ya KVZ kisha kuifunga Azam FC bao 1-0 kwenye fainali na kutwaa taji hilo.
Kiujumla katika michezo hiyo 21, Simba ikiwa chini ya Benchikha imefunga mabao 30 huku ikiruhusu kufungwa mabao 13.
Benchikha alijiunga na kikosi hicho Novemba 24, mwaka jana akitoka kuipa USM Alger ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuibwaga Yanga kwa faida ya mabao mengi ya ugenini kufuatia sare ya 2-2 na kubeba pia CAF Super Cup kwa kuifunga Al Ahly ya Misri.
Benchikha anatarajiwa kuondoka na benchi lake la ufundi lote na Simba inatarajiwa kuwa chini ya Suleiman Matola wakati ikimsaka kocha mpya.