Profesa Mkenda awakingia kifua wanaume Rombo kwa ulevi

Dar es Salaam. Mwaka 2015 iliripotiwa wanawake wilayani Rombo kulalamika kwenda nchi jirani ya Kenya kukodi wanaume kupata unyumba, baada ya waume wao kuishiwa nguvu kwa sababu ya ulevi uliopindukia.

Taarifa hiyo ilitangazwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Lembris Mchome.

Mwananchi  mwaka 2023 liliripoti habari kuwa wanaume wanaoishi pembezoni mwa Mto Mlembea, wilayani Rombo  walilalamika kuwa wake zao wanavamiwa na nyani wa kiume na wakati mwingine kuhatarisha usalama wao.

Wakati mikasa hiyo ikiripotiwa, Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda Jumamosi Aprili 27, 2024 akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa amesema ameitisha kikao na wanaume wote wa Rombo wanaoishi Mkoa wa Dar es Salaam.

Profesa Mkenda amesema atakutana na wanaume wa Rombo Mei 5, 2024.

Amesema wanaume wilayani humo ni wachapakazi na suala la ulevi si la wilaya hiyo pekee.

Profesa Mkenda amesema wanaume wa Rombo wamesambaa mataifa mbalimbali wakifanya kazi na wana mchango mkubwa kwa uchumi wa wilaya hiyo, akisema wanaokunywa ni baada ya kazi.

“Kuna aina ya pombe tunapaswa kuangalia kwa nchi mzima, kuna pombe zingine lazima tuangalie viwango,” amesema.

Profesa Mkenda amesema suala la wanaume kuwa walevi Rombo ni jambo linalokuzwa na halina uhalisia.

Kuhusu mkutano na Warombo wote, Profesa Mkenda amesema ajenda kubwa ni kujadili masuala ya maendeleo na watakuwapo madiwani wote.

Mkutano huo si wa kwanza ni mwendelezo wa aliyowahi kufanya aliyewahi kuwa Mbunge wa Rombo, Basil Mramba.

Profesa Mkenda amesema Wilaya ya Rombo inakabiliwa na shida ya maji ambayo inachangiwa na uhaba wa vyanzo vya maji, hivyo kupitia mkutano huo na wananchi watalizungumzia tatizo hilo na ufumbuzi wake.

“Mkutano huu utakaohusisha madiwani ni wa kuwajibika kujibu changamoto na kutafuta majibu,” amesema.

Related Posts