Na WILLIUM PAUL, SAME.
MKUU wa wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni ameagiza Halmashauri ya Same kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kufanya oparesheni maalum eneo la mjini kuondoa mifugo iliyoingia Same kinyume cha taratibu ambayo inadaiwa kuwa kero kwa wakazi wa maeneo hayo.
Ametoa agizo hilo akiwa kata ya Same na Kisima kwenye ziara yake ya kawaida ya kusikiliza na kutatua kero na malalamiko ya wakazi wa Wilaya hiyo ambapo amesisitiza kuwa wafugaji wanaotaka kufuga mjini lazima wafuate taratibu za ufugaji wa mjini ambapo mfugaji anapaswa kufungia mifugo yake kwenye banda na kuitafutia malisho na sio kuacha mifugo ikizurura ovyo au kuchungwa na mchungaji.
“Mifugo mjini Same siitaki, wanaofuga wafuge kwa mujibu wa taratibu za ufugaji wa mjini wafungie mifugo yao, wanaotaka kuchunga wakachunge huko kwenye maeneo yaliyoainishwa na Serikali kwaajili ya wafugaji lakini sio hapa mjini”, Alisema Kasilda.
Awali baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye mikutano hiyo miwili wamemueleza Mkuu huyo wa Wilaya adha wanayoipata ya kulishiwa mazao yao na wafugaji bila ya izini yao, hali ambayo ilimlazimu Mkuu huyo wa Wilaya kutoa maelekezo hayo kwa Halmashauri na Jeshi la Polisi.
Wilaya ya Same ni sehemu ambayo maeneo yake yamefanyiwa mpango wa matumizi bora ya ardhi ikiwemo kutenga sehemu ya Wakulima na Wafugaji kwa lengo la kuepusha migogoro isyo ya lazima baina ya makundi haya mawili, hivyo mamlaka za Serikali zilizopo zinasisita kila kundi kuheshimu eneo la mwenzake kwani zipo hatua ambazo zitachukuliwa kwamujibu wa sheria kwa atakaye bainika kuendelea kukiuka utaratibu huo.