Dar es Salaam. Wakazi wawili wa Goba akiwemo mfanyakazi wa ndani, Clemensia Milembe (19) wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, wakikabiliwa na shitaka moja la kujaribu kuua.
Mbali na Milembe, mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo ya kujaribu kuua namba 22964/2024 ni Elizabeth Makori (38), maarufu Mama Brayannna ambaye ni mama wa nyumbani.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya kujaribu kuua kinyume na kifungo 211 kifungu kidogo (a) cha Sheria ya Adhabu, sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo Alhamisi Agosti 15, 2024 na kusomewa shtaka lao na wakili wa Serikali, Rhoda Kamungu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemalila.
Milembe ambaye alikuwa amevalia suruali ya rangi ya bluu na shati rangi ya kijivu ambalo alikuwa amelikunja hadi kwenye kiwiko, huku miguuni akivaa kavaa ndala rangi ya pinki, alifikishwa mahakamani hapo mchana akiwa na mwenzake.
Muda wote aliokuwa ndani ya mahakama ya wazi namba mbili iliyopo mahakamani hapo alikuwa mtulivu, akiangalia huku na kule na kuinama chini.
Kabla ya kusomewa shitaka lao, Hakimu Rugemalila aliwaeleza washtakiwa hao kuwa hawatakiwi kujibu chochote mahakamani hapo kutokana Mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji, isipokuwa Mahakama Kuu pekee.
Hakimu Rugemalila baada ya kueleza hayo, Wakili Kamungu aliwasomea shitaka lao.
Alidai washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo Julai 15, 2024 katika eneo la Goba Kizundi lililopo katika Wilaya ya Kinondoni.
Inadaiwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa kwa pamoja walijaribu kusababisha kifo kwa mtoto Maliki Kitumbi mwenye umri wa miaka sita.
Upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hata hivyo, wakili wa utetezi Benson Florence na Jerry Kalemwa wanaomtetea mshtakiwa Elizabeth waliomba mteja wao apewe dhamana.
Hakimu Rugemalila amesema nafasi ipo wazi kwa ajili ya washtakiwa wote kupata dhamana na kisha kutoa masharti matatu ya dhamana.
Hakimu Regemalila ameyataja masharti hayo kuwa kila mshtakiwa anatakiwa awe na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kutoka serikali za mitaa au kama wameajiriwa wawe na barua kutoka kwa mwajiri zinazoonyesha pia sehemu wanayoishi.
Pia wadhamini hao wanatakiwa kuwa na kitambulisho cha Taifa ( Nida), vilevile kusaini bondi ya Sh10 milioni.
Hata hivyo washtakiwa hao walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na hivyo kurudishwa rumande.
Hakimu Rugemalila ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 29, 2024 kwa ajili ya kutajwa.