Arusha. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Arusha, imesema inawashikilia watu watatu wakiwamo watumishi wa Mkoa wa Arusha kwa tuhuma za ubadhirifu wa Sh428 milioni.
Fedha hizo zilitolewa kwa ajili ya utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).
Takukuru imesema inaendelea na taratibu ili kuwafikisha watuhumiwa hao mahakamani.
Jana Jumamosi Aprili 27, 2024 Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda aliagiza Takukuru baada ya kukamilisha uchunguzi wa suala hilo kuwafikisha mahakamani Jumatatu, Aprili 29, 2024 wote wanaohusika na suala hilo.
Makonda amedai kuna ubadhirifu wa Sh428 milioni za Tasaf.
Aliagiza kuchunguzwa kwa miradi saba ya Tasaf yenye thamani ya zaidi ya Sh1.8 bilioni iliyotekelezwa mkoani Arusha.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Aprili 28, 2024, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo, amesema ni kweli walikuwa wakichunguza tuhuma hizo.
Amesema hadi sasa wanawashikilia watu watatu na kati yao baadhi ni watumishi katika Mkoa wa Arusha, kwa ajili ya uchunguzi wa suala hilo.
Ngailo amesema wakikamilisha taratibu watawafikisha mahakamani.
“Kuna tuhuma tunachunguza kuhusu fedha hizo za Tasaf, hadi sasa tunawashikilia watu watatu na tunaendelea na taratibu ili tuweze kuwafikisha mahakamani,” amesema.
Amesema taarifa zaidi zitatolewa kwa kuwa uchunguzi bado unaendelea.
Makonda alieleza licha ya elimu na nasaha ambazo zimekuwa zikitolewa juu ya rushwa, bado kuna baadhi ya watendaji ndani ya mkoa huo wameendelea kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Amesema lengo la Tasaf ni kuhudumia wananchi hasa wa hali za chini kiuchumi kupitia miradi wanayoanzisha katika maeneo yao ila baadhi ya watumishi mkoani Arusha wameamua kutafuna fedha zilizolenga kuokoa na kuwasaidia wananchi hao.
Amesema hivi karibuni kuna video ilisambaa ikionyesha mtu ameingiziwa Sh428 milioni kwenye akaunti yake na wanaoumuingizia fedha wanazunguka upande wa pili wanaenda kuzichukua na wanagawana.
“Na yeye wanamuachia pesa kwenye akaunti yake kama kishika uchumba kwa kazi ya kupitisha fedha za wananchi hasa wa chini waliolengwa kujengewa miundombinu na kuboreshewa maisha yao, pesa ya Tasaf mnaifahamu inahudumia watu wa kada zote lakini ikiwemo wazee wetu wastaafu, wengine ni wazee wetu wanahitaji kwenda kwenye matibabu lakini bila haya watu wameamua kula hizo fedha kufanya ni miradi yao,” amesema.
“Nishukuru Takukuru mkoa kwa kazi waliyoikamilisha na nimeelekeza wahusika wote wapandishwe mahakamani Jumatatu. Nimeelekeza mtandao wote unaojihusisha na jambo hili iwe Tasaf, Tarura, Tanroads, maji, umeme, elimu, afya kwenye mradi wowote ule imefika wakati wa kufunga mkanda, hatutamuonea haya mtu kwa kuwa rushwa ni adui wa haki,” alisema.
Makonda amesema kwa sauti moja wamekubaliana kuhakikisha miradi saba ya Tasaf yenye thamani ya zaidi ya Sh1.8 bilioni inachunguzwa kwa madai kuwa huenda imejengwa chini ya kiwango, huku baadhi ya watu wakinufaika.
Amesema hatajali kiongozi wa taasisi yoyote, chama chochote wala cheo chochote ambaye atabainika kujihusisha na vitendo vya rushwa, sheria itachukua mkondo wake.
“Mimi sitajali kiongozi wa taasisi yoyote, sitajali wewe mwanachama wa chama chochote, wala wa cheo chochote ili mradi utabainika kujihusisha na kitendo cha rushwa sheria itachukua mkondo wake, siko tayari na sitakuwa tayari kumuumiza Mungu wangu,” amesema.
Amesema hatakuwa tayari kumkatisha tamaa Rais aliyemwamini kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, wala kuwaumiza wananchi kwa kutosimamia haki.
“Kwa mkoa wetu tuepuke rushwa na watendaji wote kama mnataka tuelewane vizuri na tufanye kazi kwa pamoja usijihusishe na rushwa, ukijihusisha na rushwa nitakula sahani moja na wewe, niombe wananchi kwa sauti moja tuseme rushwa hapana,” amesema.