Kaka, dada jela miaka 30 kwa kosa la kuoana

Simiyu. Mahakama ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imemuhukumu Mussa Shija (32) kifungo cha miaka 20 jela na dada yake Hollo Shija (35) kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia ya kosa la kujamiiana na maharimu (ndugu wa damu).

Hukumu hiyo ilitolewa Agosti 14, 2024 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Enos Misana katika kesi ya jinai namba 26634/2024 baada ya washtakiwa kukiri makosa yao.

Awali, Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mashitaka ya Taifa Wilaya ya Maswa, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Vedastus Wajanga aliielezea Mahakama kuwa washtakiwa hao ni ndugu wa damu kwa maana ya kaka na dada, waliokuwa wakiishi kama mke na mme na mwaka 2022 walipata mtoto mmoja wa kike.

Alisema ndugu hao wakazi wa Kijiji cha Mandang’ombe wilayani humo walitenda makosa hayo tarehe na miezi tofauti kati mwaka 2018 hadi Julai 31, 2024 katika kijiji hicho.

Alieleza makosa waliyotenda ni mwanamme kujamiiana na maharimu kinyume na  kifungu cha 158 (1) (b) na mwanamke kujamiiana na maharimu kinyume na kifungu 160 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2022.

Wajanga alisema taarifa zilifika kituo cha polisi wilayani Maswa ambapo washtakiwa walikamatwa na walipohojiwa katika kituo hicho kwa kuandikwa maelezo yao ya onyo, walikubali kutenda makosa hayo na baada ya upelelezi kukamilika walifikishwa mahakamani Agosti 14, mwaka huu.

Hata baada ya kukiri makosa yao mahakamani, ndugu hao walitiwa hatiani, huku mwendesha mashtaka akiiomba Mahakama kuwapa adhabu kali ili iwe funzo kwao na kwa jamii.

Alidai makosa  waliyofanya ni kinyume na maadili ya nchi, mila, desturi ya Mtanzania na kitendo hicho hakikubaliki katika jamii iliyostaarabika.

Washtakiwa waliomba Mahakama iwapunguzie adhabu kwani ni wakosaji wa mara ya kwanza na wana familia inawategemea na kwamba kitendo hicho walikifanya wakiwa hawajui kuwa ni kosa.

Walisema kuwa waliambiwa na babu yao mzaa baba, kuwa ili wadumishe mila za ukoo wake wanatakiwa wao waoane.

Ndipo Mahakama ikamuhukumu mshtakiwa wa kwanza (Mussa) kwenda jela miaka 20 na mshtakiwa wa pili (Hollo) kwenda jela miaka 30.

Related Posts