Dah! APR yaingiwa ubaridi kwa Azam

KOCHA msaidizi wa APR FC ya Rwanda, Thierry Hitimana amesema, baada ya kuwatazama wapinzani wao Azam FC katika michezo yao ya hivi karibuni kabla ya kukutana nao, amegundua wana timu nzuri ya ushindani hivyo wanaenda kupambana kwa heshima.

Kauli ya Thierry, inajiri wakati timu hizo zikijiandaa kushuka uwanjani Jumapili katika mchezo wa awali wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

“Tulipata nafasi nzuri ya kuiangalia katika michezo yao ya hivi karibuni ikiwemo ya Ngao ya Jamii na kugundua wana timu nzuri sana na yenye wachezaji wenye uwezo mkubwa, tutapambana nao kwa heshima ila kwa lengo la kupata matokeo chanya.”

Hitimana aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali hapa nchini zikiwemo Simba, Namungo na KMC, alisema wapinzani wao wana upungufu kadhaa katika eneo la kujilinda ingawa kila mchezo una aina yake ya uchezaji, hivyo hawazingatii hilo zaidi.

“Licha ya udhaifu iliyonayo, tumebaini pia ina wachezaji wazuri mmoja mmoja anayeweza kuamua matokeo ya timu, ukiangalia kitendo cha kupoteza mbele ya Yanga kwa mabao 4-1, katika fainali ya Ngao ya Jamii sio kigezo kwetu cha kuidharau.”

Azam iliyomaliza Ligi Kuu Bara nafasi ya pili msimu uliopita na kukata tiketi ya kimataifa baada ya miaka 10, tangu mara ya mwisho iliposhiriki 2015, inakutana na APR ambao ni mabingwa mara 22 wa Ligi Kuu ya Rwanda.

Related Posts