WAAANDISHI wa habari zaidi ya 50 ambao ni wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) kutoka Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wamepatiwa mafunzo mbalimbali kwa lengo la kujengewa uelewa kuhusu usalama mahala pa kazi huku wakihamasishwa kuwa daraja la kufikisha elimu waliyoipata Kwa wananchi.
Mafunzo hayo yametolewa na Wakala wa Usalama wa Afya Mahala pa Kazi (OSHA) ambapo katika mafunzo hayo wameelezwa namna ya kutambua vihatarishi vya mahala pa kazi sambamba na Sheria ambazo OSHA wanazifuata katika kuteekeleza majukumu yao yakiwemo ya kuhakikisha Afya na usalama wa wafanyakazi unakuwepo.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam,Mkurugenzi Mkuu wa OSHA Hadija Mwenda amesema wameona ni vema wakakutana na JOWUTA wa ajili ya kupeana elimu kuhusu mahala pa kazi.
“Tathimini yetu tumebaini uelewa Kwa jamii kuhusu usalama mahala pa kazi ni mdogo,hivyo tumeona tuwashirikishe waaandishi wa habari.Sisi na ninyi ni wafanyakazi hivyo lazima mjue yanayofanywa na OSHA, kupitia mafunzo haya waaandishi watakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu vihatarishi mahala pa kazi
“Ni lazima ujue OSHA ina nafasi gani katika maisha yetu lakini niwaambie tu hakuna mazingira ya kazi ambayo hayana vihatarishi, tunataka mtu akistaafu asione ndio anakwenda kufa.Kumekuwa na magonjwa ya misuli,shingo ,mgongo ambayo ndio yanatafuna Dunia na ili tuondoe magonjwa lazima tutoe elimu kuhusu mtindo wa maisha sehemu za kazi.”
Ametoa mfano kuwa kuna viti ambavyo vinatakiwa kutumika wakati wa kazi kwani unapofanya kazi lazima ukae mkao sahihi lakini pia mwanga uliopo mahala pa kazi lazima uwe unaokubalika ili kuepuka madhara huku akifafanua ili waaandishi waendelee kutoa taarifa endelevu lazima wawe salama.
“Matarajio yetu elimu ambayo mtaipata mtaifikisha kwa Watanzania. Watu lazima wajilinde na kujilinda ni pamoja na watu kupata elimu, tunafahanu Tanzania ina watu milioni 60 lakini tukiwafikisha waaandishi 400 ambao ni wanachama wa JOWUTA maana yake nao watawafikia mamilioni ya Watanzania.
“OSHA ni jukumu letu kuhakikisha wananchi wanakuwa salama ili nchi isonge mbele maana watu wakiwa na Afya njema maana yake tutaendelea kujenga uchumi wa nchi yetu .Niwaombe yote ambayo tutafundishwa yakawe chachu ya mabadiliko na tukaisemee Serikali ambayo muda wote iko kazini,”amesema Mwenda.
Aisha amesema waaandishi wa habari wamekuwa wanakwenda maneno mbalimbali na mengine ni hatarishi kama maneno ya migodini na viwandani ambako kuna vihatarishi hivyo lazima wajue na kupitia mafunzo hayo yatasaidia kutambua vihatarishi wanapokwenda kuteekeleza majukumu yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa JOWUTA Mussa Juma amesema wanaishukuru OSHA Kwa kukubali kutoa mafunzo hayo wa waaandishi wa habari ambao ni wanachama wao na matarajio yao ni kuona mafunzo hayo yanakuwa endelevu.
Amesema waaandishi wa habari wanakutana na changamoto nyingi katika kuteekeleza majukumu yao,hivyo ni Imani yao OSHA wakiendelea kuwajengea uelewa waaandishi itasaidia kupunguza baadhi ya changamoto hizo.
Awali Katibu Mkuu wa JOWUTA Suleiman Msuya amesema JOWUTA inafanya kazi kwa mujibu wa Sheria na inajumla ya wanachama 400 nchi nzima na leo wanachama wake 50 ndio wanapatiwa mafunzo hayo na maombi yao Kwa OSHA ni kuendelea kutoa mafunzo hayo Kwa wanachama wao walioko mikoani.
“Kwa Dar es Salaam tunaowanachama zaidi ya 80 lakini tuliona katika mafunzo hayo tuwe na washiriki 50 kutoka Dar na Pwani .Tunaamini mafunzo haya ni muhimu kwa waaandishi ambao ni wanachama wetu.Mkienda kufanya operesheni zenu tushirikisheni ili umma utambue mnachokifanya,”amesema Msuya.