Mbeya kukomesha biashara ya dawa asili kwenye mabasi

Mbeya. Wakati uuzaji wa dawa za asili ndani ya vyombo vya usafiri wa umma, hususan mabasi, ikishika kasi mkoani Mbeya, Serikali mkoani humo imesema itaongeza nguvu za kudhibiti na kuwachukulia hatua watakaobainika kujihusisha na biashara hiyo.

Biashara hiyo imekuwa maarufu mkoani hapa, ambapo wajasiriamali hupanda magari kutangaza biashara zao kwa abiria na wakati mwingine hugeuka kero ndani ya usafiri.

Hata hivyo, kinachoibua hofu na sitofahamu kwa abiria na wananchi kwa ujumla juu ya afya zao ni kutokana na bidhaa hizo kutokuwa na nembo ya mamlaka yoyote inayotambua au kuthibitisha ubora wa dawa hizo.

Uchunguizo mwananchi umebaini baadhi ya dawa hizo zinakuwa hazina anuani wala maelekezo ya kitaalamu, zaidi ya kuchorwa mti au picha za matunda.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wameeleza hofu juu ya dawa hizo huku wengine wakishauri kuwapo utaratibu wa kuwabana wanaoziuza kienyeji.

Sarah Mgeja, mkazi wa jijini Mbeya, amesema si kila anayesafiri anakuwa na magonjwa lakini kwa kutumia dawa za asili kiholela anaweza kuambulia matatizo kiafya.

“Biashara hii imeshamiri sana, sijajua Mikoa mingine nayo kama iko hivyo, lakini pamoja na kwamba wanatafuta riziki, ila Serikali iwape utaratibu namna ya kufanya biashara hii,” amesema Sarah.

Naye Benson James amesema wanaopaswa kuwajibika ni madereva wanaowapakia wauzaji hao kwenye gari na huduma hiyo bila kujiridhisha na ubora wa madawa hayo.

“Ukifika kituo fulani unaona wanapanda na kuanza kutangaza bidhaa zao, kinachotia hofu na mashaka ni bidhaa hizo kutokuwa na nembo inayotambulisha dawa hizo, hazioneshi muda wa matengenezo wala wa mwisho kuzitumia, na hazielekezi kiwango gani mtu atumie” amesema James.

Mmoja wa madereva wa magari yaendayo Tunduma mkoani Songwe ambaye amesema hutoa nafasi kwa wafanyabiashara hao kuhudumia abiria lengo likiwa ni kuwasaidia wenye shida mbalimbali na kwa njia hiyo, abiria huweza kununua mahitaji yao na wengine hufurahishwa na dawa hizo.

“Abiria ni mwanadamu, tunafanya hivyo ili kama kuna mwenye matatizo kiafya anaweza kupata dawa na muda mwingine zinawasaidia kwa sababu binafsi sijawahi kusikia zimewadhuru” amesema dereva huyo.

Naye dereva wa gari zinazofanya safari za Mbeya, Chunya, amesema wanaouza dawa hizo huomba kutoa huduma wakieleza kuwa wanakibali cha kufanya hivyo.

Anasema pamoja na hali hiyo, huridhishwa na mwitikio wa wananchi (abiria) namna wanavyojitokeza kununua bidhaa hizo kwa faida ya afya zao na hawajahi kupata changamoto yoyote.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Elizabeth Nyema amesema licha ya kwamba hawajapata kesi yoyote ya athari katika matumizi ya dawa hizo, amepiga marufuku uuzwaji holela wa bidhaa hizo.

Amesema zipo taratibu za kufuata kabla ya biashara hiyo ikiwa ni kupata vibali na kujisajili katika mamlaka inayotambuliwa na Wizara ya Afya kupitia Baraza la Tiba Asili na Tiba mbadala.

“Kabla ya kuanza biashara hizi lazima wajisajili na kupata kibali na hadi sasa  wapo 510 waliosajiliwa, lakini baraza lazima likague dawa hizo na kuthibitisha, vinginevyo hairuhusiwi kufanyika biashara hiyo.”

“Tunao wataalamu kutoka Baraza kila Wilaya, ambapo tunahitaji kuona huduma hiyo inafuata utaratibu kwa miongozo ya serikali, tutachukua hatua kwa watakaobainika” amesema Dk Elizabeth.

Mratibu Mkuu wa shughuli za Tiba Asili na Tiba Mbadala Mkoa wa Mbeya, Dk Abel Asilia, amesema Serikali haitambui wanaouza na kusambaza dawa hizo kutumia njia za panya ikiwemo kwenye vyombo vya usafiri.

Amesema hatua kali zitachukuliwa kwa wale wanaofanya biashara hiyo bila kufuata kanuni, sheria na utaratibu akieleza kuwa watashirikiana na Latra kudhibiti shughuli hiyo kwenye mabasi.

“Kwanza lazima mtoa huduma awe na kituo chake siyo kutumia mabasi au kutembeza barabarani, Serikali haiwatambui wanaofanya hivyo na tutachukua hatua za haraka kukomesha biashara hiyo”

“Tutaongeza nguvu ikiwamo mipakani kudhibiti uingizwaji wa dawa hizo na waliopo ndani kwa kushirikiana na Latra ili kupiga marufuku, haiwezekani kwenye gari igeuzwe kliniki” amesema Dk Asilia.

DaktaRI huyo amesema kabla ya kutoa huduma lazima mhusika ajisajili kuanzia ngazi ya mtaa, wilaya hadi mkoa ili kupewa kibali na leseni na Baraza la Tiba Asili na Tiba mbadala, lakini dawa zake zithibitishwe na Mkemia Mkuu wa Serikali.

Katibu Mkuu wa Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira (Tramepro), Boniventura Mwalongo amesema wanaofanya biashara hizo kupitia vyombo vya usafiri ni kinyume na sheria namba 23 ya mwaka 2002.

Anasema kufanya biashara kwenye vyombo vya usafiri siyo eneo rasmi na kwamba wataendelea kutoa elimu kwa wananchi, madereva, vyama vya usafiri na usafirishaji ili kukomesha changamoto hiyo.

“Kwa kufanya hivyo si kuimarisha bali ni kudhofisha tiba hii na siyo mwongozo wa Serikali kama inavyotaka kwa sheria namba 23 ya mwaka 2002, kila anayefanya biashara hii lazima awe na kibali,” amesema Mwalongo.

Katibu huyo amewataka wananchi kupuuza biashara ya dawa za asili zinazouzwa bila mpangilio, haswa katika vyombo vya usafiri na kwamba Shirika litatumia wiki ya tiba za asili itakayofanyika jijini Mwanza kutoa elimu.

“Sheria pia itekelezwe kwa wanaofanya biashara hiyo bila kuzingatia sheria wachukuliwe hatua, yote wanayofanya ni makosa, tunaenda kuadhimisha wiki ya tiba za asili kitaifa jijini Mwanza na tutatoa elimu,” amesema Mwalongo.

Related Posts