Geita. Wafanyabiashara wa madini wanaonunua dhahabu katika Soko Kuu la dhahabu Geita wamesema sababu inayochangia utoroshwaji wa madini hayo ni kodi kubwa ya asilimia 9.2 inayotozwa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) huku nchi jirani zikitoza kodi kiduchu.
Akizungumza juzi kwenye kikao baina ya wafanyabiashara na TRA kilichokuwa kikijadili masuala mbalimbali na kusikiliza kero za wafanyabiashara, Mwenyekiti wa soko kuu la dhahabu Geita, George Paul amesema usafirishaji wa dhahabu kwa njia za panya hautamalizika kama TRA haitapunguza kodi.
Amesema TRA imekuwa ikipanga kodi bila kufanya utafiti wala kushirikisha wafanyabiashara na matokeo yake ni wauzaji hao wa madioni kutafuta mbinu za kukwepa kodi ili wapate faida.
“Kodi hii ya 9.3 ni kubwa mno, kwa wiki mtu akitorosha kilo 10 ya dhahabu amekwepa kodi ya Sh190 milioni na ukweli ni kwamba njiani hakuna mtu anayekataa hela, ukitenga milioni 50 zinakutosha kuvuka hadi Rwanda, ukifika huko unalipa asilimia moja tu mzigo wako unakuwa salama,” amesema Paul.
Mwenyekiti huyo wa Soko ameishauri TRA kukaa na watu wa madini kuona namna gani ya kupunguza kodi kwa kuwa kila wanavyoipandisha ndivyo utoroshaji unaongezeka.
“TRA kaeni chini na Wizara ya Madini, ukweli ni kuwa mali inapatikana nyingi lakini asilimia kubwa inatoroshwa. Soko la Madini Geita lina wanunuzi 70 wa dhahabu lakini si wote wanapata mali kwa sababu dhahabu nyingi inatoroshwa,” amesema Paul.
“Watu wanataka utajiri wa haraka mtu anawaza kwa nini nilipe Serikalini Sh200 milioni wakati nikitoa Sh50 milioni naweza kuvuka na mzigo wangu ukawa salama na nakwambia Kamishna, hakuna mtu asiyetaka pesa huko njiani wanapita vizuri tu hadi wanafika Rwanda lakini mkiboresha kodi hakuna atakayetorosha,” amesisitiza Paul.
Aidha, amesema Wizara ya Madini inatoza asilimia saba na Wafanyabiashara wanalipa kwa kuwa wizara ilikaa nao chini na kuwaelimisha pamoja na kujenga mahusiano mema, jambo ambalo TRA wameshindwa kulifanya na hivyo kuwa adui wa mfanyabiashara.
Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo mkoani Geita, Gabriel Luhumbi akizungumza kwenye kikao hicho amesema mazingira rafiki ya kufanya biashara yatawafanya wafanyabiashara kulipa kodi kwa moyo na kuondoa utoroshaji.
“Kamishna, taarifa nilizopata kwa wafanyabiashara wa dhahabu ni kuwa kodi inayotozwa Uganda kwenye dhahabu ni asilimia 2 jirani zetu Rwanda ni asilimia moja lakini hapa nyumbani ni asilimia 9.3, kwa hali hii lazima utoroshwaji uendelee,” amesema Luhumbi.
Kwa mujibu wa Luhumbi mwaka 2022 tani 430 za dhahabu zilitoroshwa Afrika na hii inatokana na wafanyabiashara kuangalia wapi penye unafuu, ambako hata akilipa bado atapata faida.
Mwenyekiti huyo wa TCCIA ameishauri TRA kukaa na wadau na kufanya utafiti wa namna gani ya kuzuia utoroshaji huku wakifanya jitihada za kuwavutia wafanyabiashara ili waone sababu ya kuchangia ukuaji wa uchumi badala ya kutorosha.
Akizungumza na wafanyabiashara hao, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amesema watashirikiana na tume iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kutathmini mifumo ya kodi ili kuona namna gani ya kuweka mazingira wezeshi kwao.
“Hili la asilimia 9.3 tume ikifika pia muwaeleze … kama kweli nchi jirani iko chini lazima kutakuwa na magendo, lazima tuone namna ya kuweka kodi shindani, ambayo haitapelekea utoroshwaji. Niwaahidi tunakokwenda TRA itakuwa rafiki sana kwenu na mifumo mingi ya kodi itabadilika,” amesema Mwenda.
Mwenda amesema wanachokifanya sasa ni kuimarisha mahusiano kati yao na wafanyabiashara na kazi kubwa ni kutoa elimu kwa mlipa kodi, kurahisisha mifumo, kujenga mfumo wa ndani na kuboresha ule wa kuingiza mzigo kutoka nje ili kuweka usawa kwa wote.
Hata hivyo, amesema TRA itapambana na wakwepa kodi kwa kuimarisha vitengo vya uchambuzi na ukaguzi ili kuhakikisha watu wote wenye sifa ya kulipa kodi wanalipa.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.