Simba, Yanga kuoga manoti CAF

Dar es Salaam. Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) limetangaza kutoa kiasi cha Dola 50,000 kwa kila timu inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika kuanzia msimu huu.

Uamuzi huo unalenga kuzisaidia timu ziweze kumudu mechi za raundi mbili za awali za mashindano hayo kabla ya ile ya makundi.

Taarifa iliyotolewa na Caf leo imebainisha kwamba mgawo huo utazihusu timu zitakazoanzia raundi ya kwanza na zile zitakazoanzia raundi ya pili.

Mechi za raundi ya kwanza zinachezwa kuanzia jana Agosti 16 hadi kesho Agosti 18 na marudiano yake yatakuwa ni mwishoni mwa wiki ijayo.

Mechi za raundi ya pili zitachezwa Septemba mwaka huu na timu zitakazofanya vizuri hapo zitafuzu hatua ya makundi.

Hii ni mara ya kwanza kwa Caf kutoa sapoti ya fedha kwa klabu zinazoshiriki mashindano hayo kuanzia raundi ya mwanzo na hapo awali ilikuwa inatoa kuanzia hatua ya makundi tu.

Na ni utekelezaji wa ahadi iliyowahi kutolewa na Rais wa Caf, Patrice Motsepe ambaye alisema moja ya malengo yake ni kuzipa timu usaidizi wa kifedha ili kuimarisha mvuto na ushindani wa mashindano hayo.

Katika kipindi cha miaka miwili, Caf imeonekana kukuza thamani ya mashindano yake ya klabu kwa kupandisha viwango vya fedha ambavyo inatoa kwa timu.

Mfano kwa sasa, bingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika anapata kiasi cha Dola 4 milioni (Sh 10.8 bilioni) wakati mwaka 2022 alikuwa anapata kiasi cha Dola 2 milioni (Sh 5.4 bilioni).

Bingwa wa Kombe la Shirikisho anapata kiasi cha Dola 2 milioni wakati mwaka 2022 alikuwa anapata kiasi cha Dola 1.2 milioni (Sh 3.3 bilioni.

Kwa sasa timu inayotinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika inapata kiasi cha Dola 700,000 (Sh 1.9 bilioni) wakati mwaka 2022 ilikuwa inapata Dola 550,000 (Sh 1.5 bilioni).

Katika Kombe la Shirikisho Afrika, timu inayotinga hatua ya makundi kwa sasa inapata Dola 400,000 (Sh 1.1 bilioni) na mwaka 2022 ilikuwa inapata Dola 275,000 (Sh 746 milioni).

Katika mashindano hayo msimu huu, Tanzania inawakilishwa na timu sita ambapo Yanga, Azam na JKU zinacheza Ligi ya Mabingwa Afrika na Simba, Coastal Union na Uhamiaji zinacheza Kombe la Shirikisho Afrika.

Related Posts