Dar es Salaam. Mahakamani hakujawahi kuisha vituko, ndivyo unavyoweza kusema. Basi sikia kisa hiki ambacho kimefanya watu waliokuwa ndani ya ukumbi namba mbili wa Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, kucheka na wengine kuduwaa.
Hii ilikuwa baada ya mmoja wa wadhamini aliyefika katika mahakama kumwekea dhamana mshtakiwa aliyedai ni mtoto wa dada yake, kuzua sitofahamu wakati anahojiwa kuhusu sehemu anapoishi.
Ilikuwa jana Agosti 15, 2024 baada ya wakazi wawili wa Goba akiwemo mfanyakazi wa ndani, Clemensia Milembe (19) kufikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni na kusomewa shtaka la kujaribu kuua.
Mbali na Milembe, mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo ya kujaribu kuua ni Elizabeth Makori(38) maarufu kama mama Brayannna mama wa nyumbani.
Washtakiwa hao walisomewa shtaka lao na wakili wa Serikali Rhoda Kamungu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemalila.
Baada ya Rugemalila kuwatajia masharti ya dhamana kuwa wadhamini wao wawe na barua za utambulisho kutoka Serikali za mitaa au kama wameajiriwa basi awe na barua kutoka kwa mwajiri, ndipo sintofahamu hiyo ilitokea.
Masharti mengine ilikuwa wawe na kitambulisho cha Taifa( Nida) na wasaini bondi ya Sh10milioni kila mdhamini.
Hata hivyo, mshtakiwa wa pili alikuwa na wadhamini wawili, mmojawapo, Grayson Anthony barua yake ya utambulisho ilitiliwa shaka na hakimu.
Hakimu alimtilia shaka baada ya kuuliza sehemu anayokaa na ifuatayo ni sehemu ya mahojiano baina ya hakimu na mdhamini huyo.
Hakimu: Mdhamini umeleta barua ya utambulisho wakati kwenye masharti ya dhamana niliyotoa nimesemaa uwe na kitambulisho cha Nida?
Mdhamini: Nimeandika namba ya kitambulisho cha Taifa cha Nida.
Hakimu: Mwanayamala sehemu gani?
Hakimu: Manyanya sehemu gani?
Mdhamini: Karibu na uwanja
Hakimu: Manyanya unapafahamu vizuri?
Hakimu: Hapa tulipo Manyanya ipo wapi? Au hupafahamu vizuri?
Hakimu: Hapa, barua yako ya utambulisho imeandikwa Mwananyamala na wewe umesema unakaa Manyanya.
Mdhamini: Sielewi hasa Mwanyanya.
Mdhamini: Ninapoishi ni karibu na Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala.
Mdhamini: Kwa kweli mheshimiwa Hakimu nimekosea mheshimiwa
Hakimu: Hebu zungumza vizuri, nitakupelea mahabusu.
Mdhamini: Nakaa karibu na mochwari ya Hospitali ya Mwananyamala.
Hakimu: Unafanya kazi gani?
Hakimu: Mshtakiwa unayemdhamini anaitwa nani?
Hakimu: Mtoto wake anaitwaa nini?
Mdhamini: anaitwa mama Brayan
Hakimu: Sasa wewe unaishi Mwananyamala au Manyanya?
Hakimu: Tukahakikishe unapoishi? Unaniruhusu nitume askari waende na wewe kujua hapo unapoishi?
Hakimu: Nikichukua hatua usinilaumu! Niambie ukweli unapoishi, nieleze unapoishi.
Mdhamini: Nisamehe Mheshimiwa Hakimu.
Mdhamini: Naishi Goba kwa Awadhi
Mdhamini: Nilichukua barua kule ila wakasema lazima niwe na barua ya Serikali za Mitaa, ndio nikaona nije huku Manyanya kuchukua, maana pia niliwahi kukaa hapo.
Hakimu: Huyu mjumbe Peter Hatibu umempataje? Wakati sio sehemu unayokaa?
Mdhamini: Mheshimiwa naomba unisamehe nilitaka tu kumdhamini dada yangu ndio maana nikaenda kuomba kule.
Baada ya mdhamini huyo ambaye alikuwa amevaa miwani nyeusi na tisheti nyeupe, suruali nyeusi ya jinsi na raba nyeupe kuomba msamaha, wakili Kamungu alisimama na kuieleza Mahakama kuwa mdhamini huyo hana sifa za kidhamini na haaminiki.
“Mheshimiwa hakimu, kwanza mdhamini huyu haaminiki na amefanya kosa, hivyo hana sifa,” alidai Wakili Kamungu.
Hakimu: Hivi huyu anaishia tu kuwa hana sifa? Hawa ndio wanaochafua Mahakama.
Hakimu: Ulishawahi kukaa Mwananyama?
Mdhamini: Kama miaka 19 hivi
Mdhamini: Mwananyama na Manyanya.
Hakimu: Kwa kosa la kuidanganya Mahakama huna sifa na askari mpeleke mahabusu kwanza.
Baada ya amri hiyo, Hakimu Rugemalila alisema mdhamini wa pili amefanikiwa kutimiza masharti ya dhamana lakini kwa kuwa mdhamini wa kwanza ameshindwa kutimiza masharti, mshtakiwa wa pili anatakiwa kupeleka mdhamini mwingine ili aweze kupata dhamana.
Baada ya kueleza hayo, kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 29, 2024 itakapotajwa na washtakiwa walirudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.