Ukuaji miji, upungufu wa nyumba unavyochochea uzalishaji vifaa vya ujenzi

Dar es Salaam. Ukuaji wa miji, uhitaji wa makazi na ujenzi wa miradi ya kimkakati unaofanywa na Serikali vimetajwa kuwa sababu ya kuwapo kwa ongezeko la uzalishaji wa vifaa vya ujenzi nchini.

Ongezeko hilo linachochewa na kuendelea kukua kwa mahitaji ya bidhaa hizo muhimu katika ujenzi na si ndani ya nchi pekee, hadi mataifa jirani, hasa ukanda wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Ripoti ya Takwimu Muhimu kwa mwaka 2023 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha kuwapo ongezeko katika uzalishaji saruji, nondo na rangi katika mwaka 2023 ukilinganisha na mwaka 2021.

Uchambuzi unaonyesha uzalishaji rangi ulipaa hadi kufikia lita milioni 75.4 mwaka 2023 kutoka lita milioni 62.7 mwaka 2021, uzalishaji saruji ukifika tani 7,673 kutoka tani 6,531, uzalishaji nondo ukifika tani 343,000 kutoka tani  294,000.

Akizungumza na Mwananchi, Mtaalamuu wa Uchumi, Dk Donath Olomi amesema miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini na Serikali ni moja ya sababu ya kuchochea uzalishaji wa bidhaa hizo za ujenzi.

“Ujenzi unafanywa kwa wingi na wadau mbalimbali ikiwemo Serikali, tumeona ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), madaraja, barabara vyote hivi vinatafuna nondo na saruji, hivyo ni lazima tutashuhudia ukuaji wake,” amesema Dk Olomi.

Mbali na miradi hiyo, amesema kumekuwa na ujenzi wa viwanda unaotekelezwa, uwekezaji wa aina mbalimbali ambao unaonyesha ukuaji wa sekta ya biashara na hata miji.

“Ukizungumzia ukuaji wa miji, Dodoma ya miaka mitatu iliyopita na leo ni tofauti, hata Dar es Salaam imekua lakini bado inaendelea kukua sana, wote hawa wanahitaji saruji,” amesema Dk Olomi.

Mbali na hilo, amesema ujenzi wa nyumba za makazi ni miongoni mwa sababu zinazochochea ukuaji wa uzalishaji wa bidhaa za ujenzi katika viwanda.

Mtaalamu huyo amesema si Tanzania pekee inayotumia bidhaa hizo kwa wingi, bali pia mahitaji yapo kwa mataifa ya jirani.

Kuhusu ujenzi wa viwanda kama inavyoelezwa na Dk Olomi, takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania zinaonyesha kati ya mwaka 2019 hadi 2024 imekuwa miongoni mwa sekta tano zilizofanya vizuri kwa kuleta mtaji na idadi kubwa ya miradi.

Bidhaa hizo hutumika katika maeneo mawili, ikiwamo kupitia sekta ya uzalishaji viwandani ambayo ili kufikia hatua ya uzalishaji bidhaa, huhusisha ujenzi wa miundombinu ikiwamo ujenzi wa viwanda lakini pia ipo sekta ya ujenzi wa majengo ya biashara.

Sekta hizo kwa pamoja kila inapotolewa ripoti ya usajili wa miradi huwa miongoni mwa sehemu tano ambazo wawekezaji huzikimbilia,

 Takwimu zinaonyesha kati ya mwaka 2019 hadi 2024 uzalishaji viwandani ilishika namba moja kwa kusajili miradi 608 katika kipindi hicho, huku majengo ya biashara ikiwa nafasi ya tatu kwa kusajili miradi 140.

Mbali na hilo, Serikali imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali nchini ukiwamo wa barabara za mabasi yaendayo haraka awamu ya tatu unaofanyika ndani ya Jiji la Dar es Salaam.

Katika ukuaji wa miji, ongezeko la nyumba linadhihirishwa si tu katika makazi mapya bali pia hata katika uboreshaji wa majengo unaofanywa maeneo tofauti.

Hili huenda sambamba na ongezeko la watu nchini linaloshuhudiwa kila mwaka ambalo pia linakuza mahitaji ya makazi.

Takwimu zinaonyesha Tanzania inahitaji nyumba 390,981 kila mwaka ili kufikia mahitaji halisi ya makazi kulingana na idadi ya watu.

Mtaalamu wa biashara, Oscar Mkude amesema ukuaji wa sekta ya ujenzi unachochewa na mahitaji ya makazi yaliyopo nchini kwa sasa.

“Hivi karibuni tulimsikia Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuwa uhitaji wa nyumba kwa upande wa Dar es Salaam pekee ni milioni tatu, zote hizi zinapojengwa zinahitaji saruji, nondo, rangi na bati hivyo uhitaji wake ndiyo ukuaji wa soko,” amesema.

Mkude amesema ukuaji wa viwanda vya sekta ya ujenzi ni tofauti na ule wa viwanda vya nguo ambavyo mtu ana chaguo katika matumizi ya fedha zake kwa kuamua kununua mtumba badala ya nguo mpya dukani.

Hata hivyo, ukuajii wa uzalishaji bidhaa za ujenzi zina uhusiano wa karibu na ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja ambao sasa watu wanakuwa na kipato kinachoweza kukidhi mahitaji yao muhimu ya siku na kutunza baadhi ya fedha kwa ajili ya kuandaa makazi.

“Wanaweza kutumia fedha walizonazo na baada ya kutimiza majukumu muhimu anabaki na fedha kidogo anayoweza kutumia kufanya uwekezaji katika sehemu mbalimbali. Hapa ndiyo mtu hutenga kiasi kidogo kwa ajili ya akiba itakayotumika katika ujenzi,” amesema Mkude.

Amesema kwa sasa ujenzi unaonekana kuwa muhimu, watu wanauweka kuwa moja ya kipaumbele chao.

Si nyumba kwa ajili ya wao kuishi pekee, Mkude amesema baadhi wanalazimika kujenga hata sehemu walizozaliwa.

“Baadhi wametoka kwenye familia za kawaida, wanapoweka vipaumbele katika kujenga wanaangalia na nyumbani kwao kwa sababu wao ndio wanajua maisha waliyopitia na hali ya makazi yao,” amesema.

Mbali na hayo, uwepo wa soko la jirani ni sababu nyingine inayotajwa kuchochea ukuaji wa uzalishaji vifaa vya ujenzi hasa katika kipindi hiki ambacho miundombinu rafiki ya usafirishaji ipo, ikiwamo barabara zilizojengwa na Serikali.

“Unaweza kupeleka bidhaa zako Kenya, Zambia uwepo wa masoko kama haya ni fursa inayofanya wawekezaji wa Tanzania kuitumia kuuza huko. Miundombinu ya kufikia masoko hayo kama barabara imewekwa na hivi sasa kuna reli ya kisasa inakuja vizuri, kama miundombinu ikiwa mizuri soko ni uhakika,” amesema.

Mkude amesema uwepo wa masoko hayo unachochewa kwa karibu na ukuaji wa uchumi wa nchi husika, unaoenda sambamba na miradi ya kimaendeleo wanayoitekeleza.

Related Posts