Dar es Salaam. Siku moja baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kubaini udanganyifu katika ulipaji nauli kwa safari za treni ya kisasa ya umeme (SGR), Shirika la Reli Tanzania (TRC), limesema limewakamata watu wanaolihujumu.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 15, 2024, Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Morogoro, Christopher Mwakajinga, amesema uchunguzi uliofanyika umethibitisha kuwa baadhi ya abiria wanaotoka Dar es Salaam, hususani wanaolipa nauli za kuishia vituo vya jirani, hawashuki kwenye vituo vyao, badala yake huendelea na safari ambayo hawajailipia.
Takukuru ilitaja vituo vilivyokithiri kwa abiria kupitiliza vituo kuwa ni wanaotoka Dar es Salaam kuishia vituo vya njiani kama vile Pugu wanaolipa Sh1,000, Soga (Sh4,000), Ruvu (Sh5,000) na Ngerengere (Sh9,000).
TRC kwa upande wake imesema imewakamata watu wanaohujumu usafiri wa SGR kwa kutolipa nauli sahihi kulingana na safari wanazofanya.
Shirika hilo limesema limewakamata pia wanaokata tiketi na kisha kuziuza kwa watu wengine kwa bei ya kulangua, likitaja hatua linazochukua kukabiliana na hali hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 16, 2024, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano wa TRC, Jamila Mbarouk, amesema ni kweli tatizo hilo lipo na hutokea kutokana na kutokuwapo umakini katika kufuatilia mienendo ya abiria wanapopanda na kushuka baada ya safari.
Mbarouk amesema tayari wameanza kuchukua hatua za kuwashughulikia watu hao kwa kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria, ikiwemo mahakamani.
Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja idadi ya waliokamatwa wala waliofikishwa mahakamani akieleza hilo limeshughulikiwa zaidi na vyombo vya usalama.
“Nikiri tatizo lililosemwa na chombo cha uchunguzi lipo, baada ya kupata taarifa tumechukua hatua na mpaka sasa kuna waliokamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” amesema.
Wakati Takukuru ikieleza wanaopitiliza vituo ni abiria waliopaswa kuishia Pugu, Soga, Ruvu na Ngerengere, TRC imesema wanaofanya hivyo ni abira wa Ngerengere na Ruvu kwa kuwa hakuna abiria wanaopanda kuanzia stesheni ya Dar es Salaam na kushuka Pugu.
Amefafanua kuwa stesheni ya Pugu ni kwa ajili ya kupandisha abiria wanaotoka pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam, yakiwamo maeneo ya Gongo la Mboto na viunga vyake, Chanika na Kigogo Sokoni.
Mbali ya hayo, Mbarouk amesema wamebaini kuna watu wanaotumia Vitambulisho vya Taifa (Nida) vya kughushi, hivyo kila abiria atakayekaguliwa wakati wa kuingia kwenye treni watamuangalia kwa kulinganisha na sura ya kwenye kitambulisho, jambo ambalo halikuwa likifanyika awali.
Hatua nyingine zilizochukuliwa na TRC amesema ni kuweka mkazo katika ukaguzi wa tiketi, akieleza kutakuwa na wakaguzi ndani ya treni watakaofanya ukaguzi wa mara kwa mara tofauti na awali mtu alikuwa akipanda treni hakaguliwi tena.
Amesema pia watakaoshuka kwenye treni watakaguliwa tiketi zao kama inavyofanyika wakati wa kupanda.
“Tunaamini kwa kukagua tiketi wakati wa kupanda na kushuka tutawabaini wahalifu, wakiwamo wanaopitiliza kwenye vituo walivyopaswa kushuka, kwani mashine yetu ina uwezo wa kuwabaini watu hao kwa kupiga kelele,” amesema.
Rais Samia Suluhu Hassan akizindua safari ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma Agosti mosi, 2024 aliwataka wafanyakazi wa TRC kulisimamia shirika kwa ubunifu, uadilifu, na waweke mikakati ya kuendesha treni kibiashara ili tija iliyokusudiwa ipatikane haraka.
“Haitapendeza Serikali ikaendelea kulipa deni la fedha zilizokopwa kwa ajili ya ujenzi wa reli na kununua vitendea kazi, wakati huku shirika haliendi kwa faida, ingependeza sana shirika lingefanya kazi kwa faida ili lichangie kulipa deni,” alisema
Rais Samia alimtaka Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu kukaa na bodi ya shirika hilo na kuweka vigezo vya vipimo vya utendaji kazi. Pia ahakikishe vinafuatiliwa kwa karibu.
Pia aliitaka Wizara ya Uchukuzi na Msajili wa Hazina kuhakikisha wakati wa uendeshaji wa reli za SGR na MGR kunakuwa na akaunti mbili tofauti za fedha na mifumo miwili ya uwajibikaji.
“Tukichanganya hatujui kipi kinatupa faida kipi kinanyonya mwenziwe. Lakini tukizitenganisha tutakuwa makini katika kuendesha kila mfumo, na kila mfumo utasimamiwa vema,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa alisema Sh25 trilioni zimeshatumika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa SGR kwa maeneo yote.
Pia alisema tangu kuanza kwa safari za treni ya umeme kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kufikia Julai 28, mwaka huu abiria 100,060 wamesafiri na kuingiza jumla ya Sh2.4 bilioni.
Baada ya kuanza kwa safari za Dar es Salaam hadi Dodoma Julai 25, alisema abiria 28,600 wamesafiri na kuingiza Sh744 milioni hadi ilipofika Agosti Mosi, 2024.
Mradi wa SGR ulianza kutekelezwa katika utawala wa hayati Rais John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021.
Rais Samia alipokea kijiti cha urais, Machi 19, 2021 kipindi ambacho utekelezaji wa mradi wa SGR ulikuwa asilimia 22.
Aprili 2024, alipoeleza mafanikio ya mradi wa SGR, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema mradi huo umehusisha ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (kilomita 52.69) ambao umekamilika, Makutupora – Tabora (kilomita 371) umefikia asilimia 13.86.
Kipande cha Tabora – Isaka (kilomita 165), alisema umefikia asilimia 5.38 na Tabora – Kigoma (kilomita 506) umefikia asilimia 1.81, huku Mwanza – Isaka (kilomita 341) usanifu umekamilika.