Changamoto uchakataji mkonge kupatiwa ufumbuzi

Na Mwandishi Wetu, Tanga

Changamoto za uhaba wa mashine za kuchakata Mkonge (korona) zinazowakabili wakulima katika maeneo yao zinatarajiwa kuwa historia na kuchochea ongezeko la uzalishaji wa zao hilo.

Hatua hiyo inafuatia baada Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB) kufanya ziara kutembelea miradi mbalimbali yakiwamo mashamba ya Vyama vya Ushirika na Masoko (Amcos) na viwanda vya uchakataji Mkonge mkoani Tanga na kubaini changamoto kubwa inayowakabili wakulima ni uchache wa mashine hizo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi, Theobald Sabi, amesema ililenga kujionea sekta ya mkonge kuanzia kwenye mashamba hadi uchakataji na kuelewa mnyororo mzima wa thamani wa sekta hiyo na changamoto zinazowakabili wakulima na wadau waliopo kwenye sekta hiyo.

“Nia yetu ni kuhakikisha kwamba tunapata suluhisho la changamoto ambazo zimekuwapo hasa kwenye eneo la uchakataji mkonge. Tumejionea mashine ambazo zinafanya vizuri na zile zenye changamoto, tutachukua hatua kama bodi kuhakikisha kwamba shughuli nzima za mkonge zinakwenda vizuri ili tujenge tija kwa wakulima, mamlaka, bodi, uchumi na pato la taifa kwa ujumla,” amesema Sabi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TSB, Saddy Kambona, amesema licha ya ziara hiyo ya kujifunza na kujenga uelewa lakini jambo kubwa ambalo walitaka kujionea ni kukosekana kwa mitambo ya uchakataji mkonge na kupata majawabu kwa wakulima juu ya kuondokana na changamoto hiyo.

“Tuliwapitisha maeneo mbalimbali lakini pia tukawaonesha jitihada ambazo tumezichukua kuondoa changamoto ya uchakataji, ukiondoa jitihada ambazo tunaendelea nazo kupitia wizara yetu ya kilimo, mipango ya serikali ni kununua mitambo ya uchakataji na kuiweka maeneo mbalimbali.

“Tunawakaribisha wawekezaji binafsi kuwekeza mitambo kwenye mashamba hapa Korogwe ili kupunguza changamoto za uchakataji ambazo zimekuwa zikilalamikiwa mara kwa mara.

“Wakurugenzi wamejionea tofauti iliyopo kati ya mitambo ambayo imekuwepo miaka yote ambayo imekuwa ikiendeshwa na Sisalana na mitambo mipya ambayo imewekezwa na wawekezaji binafsi ikiwamo Hale na Magunga. Hatua hiyo imesaidia kupunguza changamoto ya uchakataji kwa wakulima katika maeneo yao,” amesema Kambona.

Aidha, amesema baada ya ziara hiyo wanategemea watakapokutana kwenye kikao cha bodi watapokea maelekezo mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji.

“Tunategemea watatupa miongozo na maelekezo, kama menejimenti tunaahidi kutekeleza yale yote tutakayoelekezwa kutatua changamoto ili kufikia malengo ya kuzalisha tani 120 kwa mwaka ifikapo 2025,” amesema Kambona.

Mjumbe wa Bodi hiyo, Naweed Mullah, amesema wamejionea mazuri mengi na kutoa wito wadau wanaoshiriki kwenye biashara hiyo wajitahidi kutoa huduma bora na mashine ziwe zinahudumiwa kwa wakati ili wananchi wanufaike na miradi hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Magunga Amcos na Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Amcos za Mkonge Tanga, Shedrack Lugendo, ameishukuru bodi kuwatembelea na kujionea shughuli wanazofanya na kwamba mitambo ya uchakataji mkonge ya Kampuni ya Sisalana imepitwa na wakati na haina matengenezo mazuri ambapo mkonge mwingi unaishia kwenye mtaro mkulima anapata hasara.

“Tuna matarajio makubwa kwa Amcos tano kwa kuwa Bodi ya Wakurugenzi imepita na Amcos zimeomba kuwekeza viwanda, kila kitu tulishamaliza kwa hiyo tunawaomba waharakishe Amcos ipate korona zake ili iwe mkombozi kwa wakulima,” amesema Lugendo.

Related Posts