Dar es Salaam. Kampeni maalumu ya kuvutia wawekezaji mikoa ya kusini imeanza kufanyika wakati ambao tafiti zinaonyesha kuwapo kwa uwekezaji hafifu unaofanywa katika maeneo hayo.
Lengo la kampeni hiyo ni kuzitangaza fursa zinazoweza kutumiwa na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi zinazoweza kugusa maisha ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Kampeni hii inaanza wakati ambao takwimu zinaonyesha mikoa ya Pwani na Dar es Salaam ndiyo imekuwa kimbilio la wawekezaji wengi, huku wataalamu wa uchumi wakitaka jitihada zifanyike zaidi ili kuvutia wawekezaji kwenye maeneo yenye fursa nyingi ambazo hazijafikiwa.
Taarifa iliyotolewa na kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa vyombo vya habari, inaeleza kuwa kampeni hiyo itagusa mikoa ya Lindi, Ruvuma na Rukwa, na baadaye Katavi na Kigoma ikiwa ni awamu ya pili ya Kampeni hii iliyoanza Januari.
Meneja wa Uhamasishaji, Uwekezaji wa Ndani wa TIC, Felix John amesema lengo la kampeni hiyo ni kuchochea mabadiliko na kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.
“Hatua hizi zitasaidia Watanzania katika kuanzisha na kukuza miradi yao. Lengo mojawapo la kampeni ni kueleza mabadiliko yaliyofanywa katika sheria ya uwekezaji ya mwaka 2022, ambayo imeweka kipaumbele kwa Watanzania katika uwekezaji wa ndani,” amesema John.
TIC ilitenga mwaka 2024 kuwa maalumu kwa ajili ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani ikilenga kuwavutia Watanzania wengi zaidi kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini.
Kwenye uwekezaji huo, wazawa wanaweza kusimama wao wenyewe au kuingia ubia na kampuni za kigeni ili kutimiza malengo yao.
“Miongoni mwa vitu vilivyofanywa katika mabadiliko ya sheria ni kupunguza thamani ya mtaji kwa wanaotaka kuwekeza kutoka dola laki 1 hadi dola elfu 50, hivyo kurahisisha uwekezaji kwa Mtanzania,” amesema.
Awali waratibu wa kampeni hiyo ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani walipokuwa Lindi, walitembelea mradi Sheby Mix Investment, uliosajiliwa TIC unaofanya shughuli za uchimbaji madini mkoani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga aliwataka wananchi wa Lindi na Watanzania kwa ujumla kutumia fursa hiyo kwa kupata elimu na kuchukua hatua sasa kwa ajili ya kufanya uwekezaji.
“Nitoe wito kwa wana Lindi na Tanzania kwa ujumla kutumia fursa hii kupata elimu, lakini pia kuchukua hatua sasa, kwani Serikali ya ina lengo la kuwasaidia Watanzania si tu kusajili miradi, bali pia kuona jinsi miradi hii inavyosaidia Watanzania, hasa katika suala zima la ajira,” amesema Ndemanga.
Mradu wa Sheby Mix Investment mpaka sasa unazalisha tani 80 hadi 90 za gypsum kwa mwezi ambayo inauzwa katika viwanda vingine, kikiwemo cha Dangote kilichopo Mtwara huku kikiwa kimeajiri Watanzania 40.