Dar es Salaam. Mtandao wa Viongozi Wanawake Vijana umeungana na Mtandao wa Kupinga Rushwa ya Ngono Tanzania kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na vyombo vinavyohusika na mabadiliko ya sheria, ikiwemo Bunge, kuondoa kifungu cha 10(b) cha mapendekezo ya kuzuia na kupambana na rushwa ya ngono kinadaiwa kumhukumu mtu aliyetendewa udhalilishaji huo kwa kigezo cha kushawishi.
Ombi hilo linakuja siku moja tu baada ya Mtandao wa Kupinga Rushwa ya Ngono kutoa tamko lake la kutaka kuondolewa kwa kifungu hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 16, 2024, jijini Dar es Salaam, Hellen Sisya, ambaye ni mmoja kati ya wajumbe wa mtandao huo, amesema wao kama viongozi vijana wanawake wanapendekeza kuondolewa kabisa kwa kifungu hicho kwa kuwa kitawafanya waathirika kuogopa kutoa taarifa kwa mamlaka husika, pale wanapofanyiwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, ikiwemo rushwa ya ngono.
Pia amesema nyongeza ya kifungu hicho ni kinyume na sheria za kimataifa, sheria za kuzuia rushwa za SADC, Umoja wa Afrika, na kanuni zote zinazoongoza Muungano wa Afrika Mashariki zinazokataza rushwa ya ngono.
“Tunaviomba vyombo vinavyohusika na mabadiliko ya sheria, ikiwemo Bunge, kutobariki kifungu hicho kwani kitapelekea uwepo wa sheria itakayoendeleza utumiaji mbaya wa mamlaka na ambayo itanyamazisha sauti za wahanga (waathirika) katika kuleta uwajibikaji zaidi kwa wale wote wenye dhamana ya uongozi,” amesema.
Wanamtandao wa Kupinga Rushwa ya Ngono Tanzania, wakati wakitoa tamko lao juzi, walisema marekebisho yaliyobainishwa kwenye kifungu cha 10(b) ni kinyume na dhana nzima ya kifungu cha 25 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa kwa kuwa kinalenga kumlinda mhalifu badala ya kuwa msingi wa kuzuia uhalifu na kulinda haki.
Walibainisha kuwa hilo linaweza kuchochea kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii ambapo waathirika wakubwa ni wanawake na watoto.