Baba ashikiliwa, kisa mwanaye aliyehukumiwa kifungo miaka 20 kutoroka

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu Ally Palupalu kifungo cha miaka 20 jela, lakini kutokana na yeye kutokuwepo mahakamani, baba yake aliyemdhamini ameshikiliwa mpaka atakapopatikana.

Uamuzi huo umetolewa leo, Agosti 16, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu, Fahamu Kibona, wakati kesi hiyo ya kusafirisha nyara za Serikali ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa hukumu.

Hata hivyo, Palupalu hakuwepo mahakamani hapo baada ya kuruka dhamana na hivyo mahakama imeamuru baba yake mzazi, Juma Palupalu akamatwe hadi mshtakiwa huyo atakapopatika.

Mbali na Palupalu, mshtakiwa namba moja katika kesi hiyo, Husein Seif maarufu kama Mzizima yeye amehukumiwa kifungo cha miaka 17 jela baada ya kupatikana na hati ya kusafirisha vipande vinane vya meno ya tembo, vyenye thamani ya Sh87 milioni, bila kuwa na kibali kutoka kwa mkurugenzi wanyamapori nchini.

Wakili wa Serikali Aaron Titus amedai kuwa shauri hilo limeitwa kwa ajili ya kutolewa hukumu na upande wa mashtaka upo tayari, ila mshtakiwa wa pili hayupo mahakamani hapa, hivyo tunaomba mdhamini wake atueleze alipo mshtakiwa,” alidai Wakili Titus.

Mdhamini huyo Juma Palupalu ambaye ni baba mzazi wa mshtakiwa Ally, amedai mwanae alimwambia anaenda mahakamani lakini hajui wakati huo alikuwa wapi.

Baada ya kauli hiyo, Wakili Titus alisema hata jana shauri hilo lilishindwa kitolewa hukumu kutoka na mshtakiwa huyo kushindwa kufika mahakama, hata alipopigiwa simu na baba yake alimweleza yupo njiani anakuja na baadaye alidai anaumwa.

Hakimu Kibona baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, aliamuru mdhamini huyo ambaye ni baba yake Ally akamatwe na kupelekwa rumande hadi hapo mshtakiwa atakapopatika.

“Kwa kuwa mshtakiwa hayupo, mahakama inaamuru mdhamini wake akamatwe na apelekwe rumande hadi hapo atakapopatikana mshtakiwa na kwamba mara tu mshtakiwa huyo atakapopatikana adhabu yake ya kutumikia kifungo hicho ndipo itaanza mara moja,” alisema Hakimu Kibona

Akichambua uamuzi huo, Hakimu Kibona alisema washtakiwa wanakabiliwa na kosa moja la kujihusisha na biashara ya nyara za Serikali kinyume na sheria.

Alisema kutokana na ushahidi uliotolewa pamoja na vielezo vilivyowasilishwa na upande wa mashtaka, haujaacha shaka kuwa washtakiwa hao walihusika na kosa hili.

“Hivyo mahakama inawatia hatiani kama mlivyoshtakiwa katika kesi hii” alisema hakimu Kibona.

Washtakiwa baada ya kukutwa na hatia, upande mashtaka uliomba mahakama itoe adhabu kali kwa mujibu wa sheria na iwe funzo kwa wengine wenye tamaa kama hiyo.

Kwa upande wake mshtakiwa Seif, yeye aliomba mahakama impunguzie adhabu akijielekeza kuwa amekaa ndani kwa muda mrefu na pia anategemewa na wazazi wake na familia yake na kwamba ana watoto wanaosoma, hivyo akifungwa watakosa huduma.

“Mheshimiwa hakimu, mimi nimekaa ndani muda mrefu tangu mwaka 2021 hivyo naomba unipunguzie adhabu,” aliomba Seif

Hakimu Kibona baada ya kusikiliza maombi ya mshtakiwa huyo, alisema amezingatia ombi la mshtakiwa kukaa muda mrefu ndani, hivyo mahakama imepunguzia miaka mitatu aliyokuwa rumande kutoka kifungo cha miaka 20 jela hadi kifungo cha miaka 17 jela.

Alisema kwa upande wa mshtakiwa Palupalu yeye atatumikia kifungo cha miaka 20 atakapopatikana.

“Haki ya kukata rufaa iko wazi iwapo washtakiwa hamjaridhika na hukumu iliyotolewa na mahakama,” alisema Hakimu.

Seif na Palupalu walikamatwa Machi 13, 2021 katika maeneo ya Gongo la Mboto, wilaya ya Ilala wakisafirisha vipande 8 vya meno ya tembo yenye thamani ya Sh87milioni.

Related Posts