NDIO IPO KIZIMKAZI HALAFU KUNA KIZIMKAZI YA SAMIA

Na Said Mwishehe,Michuzi TV -Kizimkazi

NIMETAMANI kukaa kimya lakini nimeshindwa acha nisime japo kidogo angalau moyo uwe huru.

Nafahamu kazi kubwa ya moyo ni kusukuma damu lakini chakushangaza moyo wangu eti umeamua kujipa na jukumu la kuhifadhi mambo na matukio.

Nisipokuwa makini moyo utaanza kujihusisha na mambo ambayo sio ya kwake.Ni bora niseme moyo uwe huru.Kwani shida iko wapi?

Iko hivi huu ni ule msimu wa tukio kubwa la tamasha la Kizimkazi maarufu Kizimkazi Festival.Inategemea tu unataka kutamka Kiswahili kwa lugha ya akina Wayne Rooney wa Uingereza.Lugha ya Malkia Elizabeth.Usinicheke swahiba.

Basi bwana kama unavyojua ninapozungumza Kizimkazi uwe unanielewa.Kizimkazi ndiko anakotoka mama yetu,mpendwa wetu ,rafiki na Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan a.k.a Mama wa R4.Nakupenda Rais wangu.

Tamasha la Kizimkazi kuwa Kizimkazi anakotoka Rais hata ingekuwa wewe unakaaje kimya, unanyamaza ili iweje? Ingekuwa mimi ni shabiki wa Yanga ningekuuliza KWANI WE HUOGOP lakini mimi ni shabiki wa Simba Yaaani UBAYA UBWELA.

Nimeamua kufunga safari kutoka Dar es Salaam kuja Zanzibar kushuhudia mechi ya kisasi ya mashabiki wa Simba na Yanga .Mechi hiyo ni sehemu ya matukio ya kuelekea katika Kizimkazi Festival.

Ni mechi inayohusisha mashabiki wa Simba na Yanga walioko Zanzibar na hasa Kimzikazi anakotoka Rais Samia.Kwa kugha nyinyine wajuu wa mama leo watakuwa uwanjani.

Acha tuone nani ataibuka kidedea kisha achukue milioni tano maisha yaendeleee.Mwaka jana hakupatikana mshindi,si Simba ,si Yanga.Leo tutajua nani mbabe.

Kwa utamu wa mechi ya leo, na mchezo wenyewe unakofanyika nakaaje Dar? Nakaaje kimya? Yaani niuchune? Nisiwaambie hata washikaji zangu?Nisiwaambe Wana? Nisiwaambie masela? Nisiwaambie wadau? Hapana lazima niseme tena kwa herufi kubwa…

JAMANI MWENZENU niko Kizimkazi nyumbani kwa Rais kushuhudia game ya kibabe ,game ya Simba na Yanga(mashabiki).

Neno Kizimkazi hakikisha linabakia kichwani kwako hata kama mengine utasahau.Ndiko ambako Rais Samia anatokea lakini ndiko tamasha la Kizimkazi linafanyika.

Ni tamasha ambalo limeandaliwa na Taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation chini ya Mwenyekiti wake Wanu Hafidh Ameir ambaye pia ni Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.Kwa kukumbusha tu dada Wanu ni mtoto wa Rais Samia, hivyo ni dada yetu na wengine ni mdogo wetu.Ni mtoto wa Mama.

Kwa wale ambao wanataka kufika Kizimkazi ni rahisi tu, ukiwa katika bandari ya Zanzibar kutoka hapo hadi Kizimkazi ni kilometa 41 tu.Kwa wale wanaotumia usafiri wa gari binafsi wakitumia spidi 80 basi watatumia muda wa saa moja na nusu.Wale watakaokwenda kwa spidi 100 basi watatumia saa moja.

Sehemu ambayo watatembea spidi ndogo ni pale katika Ikulu ya Tunguu kwa kuwa hapo unapaswa kutembea mwendo mdogo wa spidi kati ya 40 hadi 20 na itakuchukua kama dakika moja na nusu au mbili utarejea katika spidi ya 80 au 100.

Kwa wanaotaka kutumia usafiri wa bajaji na bodaboda nao upo tena wa uhakika.Hapo mchawi mapatano tu .Mchawi hela tu lakini ukiona vipi daladala zipo nauli Sh.2000 tu .

Ukiwa njiani macho yatakuwa yanashuhudia uzuri wa aridhi ya Zanzibar,aridhi ya Rais Dk.Hussein Ali Mwinyi.Ukienda enda utakutana na Msitu wa Jozani wenye wanyama adimu ambao hawapatikani kokote zaidi ya Jozani kwenyewe.

Njoo Zanzibar,njoo Kizimkazi,njoo kwenye tamasha kubwa la Kizimkazi,leo tunaanza na mechi ya Simba na Yanga.

Sifa kubwa ya wananchi wa Kizimkazi ni wakarimu,wapole,wacheshi na wenye kupenda wageni.Ukitaka kujua wanafananaje angalia ukarimu wa Rais Samia,angalia upendo wake,angalie unyenyekevu wake hapo utakuwa umepata picha halisi ya wananchi wa Kizimkazi.

Unaweza kusema nazidisha chumvi ,hapana kama unataka ushahidi muulize Rais Samia atakuthibitishia.Kama huna namba yake niambie nikupe Ila kwenye namba hapo tafuta mwenyewe.Mi naitoa wapi ?

Pamoja na hayo niwapongeze Mwanamke Initiative Foundation wakiongozwa na Wanu Hafidh Ameir Kwa kuandaa tamasha la Kizimkazi.Tamasha ambalo limekuwa chachu katika kuhamasisha maendeleo ya wananchi.

Tamasha ambalo limekuwa chachu katika kuhamasisha michezo Zanzibar na Tanzania Bara.Hakika tamasha hili limekuwa mwanga wa maendeleo.

Halafu nikwambie kitu jamaa yangu juzi kati nilibahatika kuwa Makunduchi ya huku huku Kizimkazi bwana nilikutana na machungwa matamu hatari.Ya Tanga cha mtoto.

Inatosha nisikuchoshe wala usinichoshe acha nisubirie mechi ya watani.Uwe na Jumamosi njema na anayetaka ubuyu wa Babu Issa aseme mapema.

Related Posts