Gaza. Israel imetoa amri nyingine ya kuwataka wakazi wa Maghazi kuhama maeneo yao, wakati huu ikilenga vitongoji vya kambi ya wakimbizi ya Maghazi katikati mwa Gaza.
Msemaji wa Israel, Avichay Adraee, alitoa tangazo hilo kupitia chapisho kwenye mitandao ya kijamii, akiorodhesha maeneo ya Maghazi na vitongoji kadhaa vya kusini mwa Gaza, ambavyo wakazi wanapaswa kuondoka.
Amesema Hamas ilifyatua makombora kutoka maeneo hayo na Jeshi la Israel litajibu kwa nguvu kubwa.
“Kwa usalama wenu, hameni mara moja,” amesema Adraee akizungumza kwa Kiarabu.
Hii ni mara ya tatu kwa Israel kuamuru wakazi wa vitongoji vipya ndani ya Gaza kuhama katika siku chache zilizopita, na kusababisha makumi ya maelfu ya watu kuyakimbia makazi yao.
Wakati huohuo, Wizara ya Afya ya Lebanon imethibitisha kuwa watu tisa wameuawa katika shambulio la Israeli usiku wa kuamkia leo Agosti 17, 2024.
Wizara hiyo imesema watu tisa waliuawa katika shambulio la usiku wa manane lililofanywa na Israeli katika eneo la Jiji la Nabatieh kusini mwa nchi hiyo.
Taarifa ya wizara hiyo imesema miongoni mwa waliouawa ni mwanamke na watoto wake wawili, huku watu wengine watano wakijeruhiwa, wawili kati yao wakiwa mahututi.
Wizara hiyo imesema jengo la makazi lilishambuliwa katika jiji hilo, wakati Jeshi la Israeli likidai hivi karibuni kuwa lilishambulia ghala la silaha la Hezbollah.