PAZIA la michuano ya kimataifa inayoendeshwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ngazi ya klabu limefunguliwa rasmi wikiendi hii.
Klabu mbalimbali Afrika sasa zinapambana kuweka heshima kuanzia juzi Ijumaa na jana zilipigwa mechi nyingine kabla ya leo Jumapili kupigwa michezo mingine.
Kwa Tanzania timu za Yanga, Azam FC, Simba na Coastal Union zinawakilisha nchi. Simba pekee ndiyo haitaanzia raundi ya kwanza, ila wengine watano wanaanzia raundi ya kwanza, tatu zikishuka leo kibaruani.
Kwa msimu huu Yanga inatajwa katika orodha ya timu zinazopewa nafasi ya kufanya vizuri. Hii inatokana na kile ilichofanya mwaka jana na mwaka juzi katika michuano hiyo.
Mwaka juzi, Yanga ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Ikapoteza kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya sare ya mabao 2-2 na USM Alger ya Algeria.
Ilikuwa ni kiwango bora kwao. Nafasi ya juu zaidi waliyowahi kushika katika Kombe la Shirikisho kabla ya hapo ni kufika hatua ya makundi. Ilikuwa historia mpya.
Mwaka jana walitolewa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa mikwaju ya penalti, baada ya suluhu katika michezo miwili.
Yanga iliwaduwaza wengi kwa namna ilivyosimamishana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini. Hiyo imetosha kuwafanya wapewe nafasi kubwa mwaka huu.
Kwa Simba, mwaka huu inaikosa Ligi ya Mabingwa, lakini nayo inategemewa kufanya vizuri katika Kombe la Shirikisho.
Simba imefika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa mfululizo. Licha ya kushindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa miaka mitatu, katika mashindano ya CAF inafanya vizuri.
Mwaka jana ilitolewa na Al Ahly katika robo fainali. Ahly wakaenda kutwaa ubingwa huo.
Ndoto ya Simba imekuwa kufika nusu fainali ambapo mwaka huu itapambana tena kuona kama wanaweza kufikia rekodi hiyo. Wataweza? Ni jambo la kusubiri na kuona.
Coastal Union wanashiriki tena mashindano hayo baada ya miaka mingi. Watakuwa na jipya gani? Hawana presha kubwa. Hakuna watu wenye matarajio makubwa kutoka kwao. Watakachofanya itakuwa ni bonasi tu.
Sasa turudi kwa hawa Matajiri wa Chamazi, Azam. Wana deni kubwa katika mashindano ya Afrika. Hawajawahi kufanya lolote la maana tangu 2013. Wana kitu cha kufanya. Wana maswali ya kujibu.
Tangu Azam imeanza kushiriki mashindano ya Afrika haijawahi kufika hata makundi. Yaani imeshindwa hadi na Namungo iliyopata nafasi hiyo kwa mara ya kwanza hivi majuzi na kutinga hatua hiyo, japo nayo ilitia aibu kwa kucheza mechi zote sita za kundi ilililokuwapo bila kushinda wala kufunga bao. Si mchezo! Kwa Azam wengi wanajiuliza nini kinawashinda? Azam ina pesa. Inafanya usajili mkubwa. Inaajiri makocha wakubwa. Kwanini hawafanyi vizuri kwenye mashindano ya Afrika? Inafikirisha sana.
Hii ni mara ya pili inashiriki Ligi ya Mabingwa. Wamerudi baada ya miaka tisa. Mara ya kwanza ilikuwa 2015 ilipotolewa na chama la zamani la kipa wao wa sasa, Mohammed Mustafa yaani Al Merrikh ya Sudan.
Mwaka huu wana jambo la kufanya. Tunatazamia kuwaona wakifika makundi. Japo wana mtihani mzito. Wanaanza na APR ya Rwanda. Haina historia kubwa katika mashindano ya Afrika. Haijawahi pia kufika hatua ya makundi. Hivyo ni timu ambayo wanapaswa kuishinda. Sitaki sana kuzungumzia mtihani utakaofuata kwani muhimu kwao ni kuwatoa kwanza APR.
Mashabiki wana hamu na subira ya kuona Azam inafanya vyema kimataifa. Kama wanavyofanya Mamelodi Sundowns.
Na sasa ni wakati muafaka kwani wana timu bora. Wana kocha bora. Wenye timu wako mstari wa mbele. Tumeona juzi Yusuf Bakhresa alikwenda kuzungumza na wachezaji. Huwa inatokea mara chache. Ni morali tosha kwa wachezaji. Acha tusubiri tuone mwaka huu kama Azam FC itazima kiu yetu ya kuwaona wakifanya vizuri kimataifa.