Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimefanya uteuzi wa makatibu wa kanda nne wa chama hicho.
Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi 17 Agosti,2024 na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema, imezitaja kanda hizo kuwa ni Magharibi, Serengeti, Victoria na Nyassa.
Mrema amesema uteuzi wa makatibu hao umethibitishwa na Kamati Kuu ya Chama iliyoketi katika kikao chake cha kawaida kuanzia Agosti 8 hadi 10,2024 jijini Dar es Salaam.
“Kamati Kuu ya chama iliyoketi katika kikao chake cha kawaida tarehe 8-10 Agosti,2024 pamoja na maamuzi mengine mbalimbali ilithibitisha uteuzi wa makatibu wa kanda za Magharibi, Serengeti, Victoria na Nyassa, hilo ni kwa mujibu wa Katiba ibara ya 7.7.16(c),” imeandika sehemu ya taarifa hiyo.
Imewataja walioteuliwa kwa kanda ya Magharibi ni Meshack Buhahagare ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa ofisa mwandamizi makao makuu.
Mwingine ni Grace Shio, aliyeteuliwa kuwa Katibu Kanda ya Nyassa ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa mweka hazina wa kanda hiyo.
Kanda ya Serengeti aliyeteuliwa ni Jackson Mnyawami, ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Katibu wa kanda hiyo, huku Kanda ya Victoria akiteuliwa Zacharia Obad ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa katibu wa kanda hiyo.