NOBODY can stop reggae! Hii ni ngoma matata iliyowahi kupigwa na kuimbwa na Lucky Dube. Gwiji huyo wa miondoko ya Reggae, kwa sasa ametangulia mbele ya haki, lakini ngoma yake inaendelea kutamba.
Si unajua Reggae haipigwi na wanyoa viduku. Miondoko hii inapigwa na kuimbwa na watu wenye rasta. Sasa unaambiwa pale Msimbazi, kuna kikosi cha Reggae Boys.
Mabingwa hao wa zamani na washindi wa tatu wa Ngao ya Jamii msimu huu, wana nyota karibu kikosi kizima cha wenye kufuga au kuwa na mtindo wa rasta, kuanzia kipa hadi eneo la ushambuliaji.
Ndio, katika dirisha la usajili lililofungwa Ijumaa, Simba imesajili mashine kadhaa ambazo zinafuga rasta na kuungana na wengine waliosalia katika kikosi kilichopita, kilichomaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Bara na hapa chini ni dondoo ya Reggae Boys hao wa Msimbazi ambao wanaweza kuanza na mfumo wa 3-5-2.
Hakuna ubishi Simba imefanya usajili wa aina yake safari hii kwa kupata kikosi cha wachezaji 11 ambao wote wana mitindo ya rasta kichwani, kuanzia kipa Moussa Camara ‘Spider’ aliyesajiliwa hivi karibuni akitoka AC Horoya ya Guinea.
Kipa huyo aliyeonyesha uwezo mkubwa katika mechi tatu alizocheza hadi sasa ikiwamo moja ya kirafiki ya Simba Day dhidi ya APR na mbili za Ngao ya Jamii, ameonyesha anaweza kumrahisishia kocha Fadlu Davids kutumia mfumo huo wa 3-5-2 akiwa na maana ya kuanza na mabeki watatu wa kati, viungo watano na kuwatumia washambuliaji wawili bila wasiwasi.
Licha ya kwamba atakuwa anamkosa beki wa kulia mwenye rasta, lakini ana wachezaji wa eneo la kiungo wanaoweza kusaidia ulinzi na mtu akapigwa nyingi tu kwani, Camara anaweza kuanza na mabeki Valentin Nouma, Chamou Karaboue na Che Fondoh Malone ambaye yupo na timu tangu msimu uliopita. Nouma anayecheza beki wa kushoto na Karaboue ni nyota wapya waliosajiliwa msimu huu, huku Malone akicheza msimu wa pili.
Msimu uliopita Malone alitengeneza ukuta mgumu na rasta mwingine aliyeondoka kikosini, Henock Inonga aliyepo FAR Rabat ya Morocco kwa sasa.
Ukiondoa eneo hilo la ulinzi, Reggae Boys wa Simba kwa eneo la kiungo, Fadlu anaweza kuwachezesha kwa pamoja Fabrice Ngoma, Augustine Okejepha, Debora Mavamba, Awesu Awesu na Kibu Denis ambao nao wana mitindo ya rasta kichwani.
Ngoma ambaye wakati mwingine uzifumua nywele zake na kuziweka katika mitindo wa kiduku pamoja na Kibu ni wachezaji waliokuwapo msimu uliopita, wakati Okejepha anayetokea Nigeria, Debora raia wa DR Congo na Awesu ni nyota wapya waliosajiliwa dirisha hili lililofungwa usiku wa jana Alhamisi.
Katika eneo la mbele, Fadlu ana mashine za mabao, Freddy Michael aliyesajiliwa katika dirisha dogo la msimu uliopita na aliyemaliza na jumla ya mabao 11, yakiwamo sita ya Ligi Kuu Bara na mengine ya Kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa Afrika, sambamba na Mganda Steven Mukwala aliyetua hivi karibuni.
Mukwala aliyesajiliwa kutoka Asante Kotoko ya Ghana, aliyoifungia mabao 14 hadi sasa ameifungia timu hiyo bao moja katika mechi sita ilizocheza Simba tangu ilipoenda kambini Ismailia, Misri na kurudi nchini.
Kama sio kuuzwa dakika za lala salama, huenda Simba huenda ingekuwa na mchezaji wa akiba wa kikosi cha reggae boys, Willy Onana kwani naye alikuwa ana mtindo wa rasta kichwani.
Licha ya safari hii Simba kuonyesha kama imekomoa kwa kusajili reggae boys, lakini hii sio mara ya kwanza kwani hapo awali iliwahi kuwa na wachezaji marasta akiwamo kina Amri Kiembe, Haruna Moshi ‘Boban’, Nurdin Bakari, Amir Maftah na Moses Odhiambo waliowahi pia kuichezea Yanga bila kumsahau Dan Sserunkuma na wote walikuwa na viwango vikubwa uwanjani, baadhi hivi sasa wakiwa wamestaafu soka la ushindani, huku Kiemba akigeukia uchambuzi na Maftah akisomea ukocha.
Mchezaji wa zamani wa Simba, Steven Mapunda ‘Garrincha’ alisema wachezaji hao (marasta) wakipata muda na kuzoeana huenda wakafanya makubwa ya kusaidia timu, kwani boli lipo miguuni mwao hata kama ni mapema mno kuanza kuwajadili.
“Mfano kiwango alichokionyesha Debora ni kikubwa, akiendelea nayaona mabao mengi kutoka kwake,” alisema Garrincha, huku kipa wa zamani wa Yanga, Benjamin Haule aliongezea kwa kusema;
“Nimewaona wachezaji hao katika mechi ya Simba Day, nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga na Coastal Union kusaka mshindi wa tatu, wanafanya kazi nzuri, isipokuwa Mukwala anahitaji utulivu ili kupata umakini wa kufunga. Pia hakuna asiyejua uwezo wa Awesu na Kibu, pia hata yule Mnigeria (Okejepha).”