Kazi imeanza Kizimkazi Festival | Mwanaspoti

NI michezo, burudani, uchumi na fursa mbalimbali za kijamii katika tamasha la nne la Kizimkazi linalofunguliwa leo Jumapili na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi huko Kizimkazi mkoa wa Kusini Unguja.

Tamasha hilo linatajwa kufungua fursa mbalimbali za kijamii, kimichezo na kiuchumi.

Katibu wa Kamati Kuu ya tamasha hilo lenye kauli mbiu ya Kizimkazi Imeitika, Ahmed Abdulhamid Hamis aliliambia Mwanaspoti kuwa, maandalizi yamekamilika na litawahusisha wadau mbalimbali na viongozi wa Serikali ya serikali ya Muungano na ile ya SMZ.

Hamis alisema katika tamasha hilo kutakuwa na mashindano ya soka, muziki wa Bongo Fleva na Zenji Flava.

“Pia kutakuwa na masuala ya utamadunia na asili ya vyakula vya Kizanzibar na mafunzo ya wajasiriamali ikiwamo kuwapa mikopo baadhi ya vikundi ili kujikwamua kiuchumi,” alisema

Alisema ufunguzi huo utatanguliwa na jogging itakayoanzia Uwanja wa Kizimkazi Dimbani hadi viwanja vya Kizimkazi Mkunguni kabla ya ufunguzi itakayoongozwa na Dk Mwinyi.

Akizungumzia matukio ya kimichezo, Naibu Katibu Mkuu wa Kamati, Hindi Juma Ramadhan alisema leo baada ya ufunguzi jioni ni bonanza maalumu litakalohusisha michezo ya bao, karata na soka ya ukufukweni.

Ratiba itaendelea kesho Jumatatu hadi siku ya kufungwa kutakuwa na mashindano kama ya mbio za baiskeli zitakazoanzia Uwanja wa Maisara hadi Makunduchi zikihusisha wapiga pedeli wa ushindani, wazee na walemavu, pia kutachezwa kabadi ambao Zanzibar imekuwa ikifanya vizuri katika nchi za Afrika Mashariki.

“Kutakuwa pia na mbio za ngalawa ambazo zitawapa fursa washindi kupewa boti za kisasa na pesa ili kuwafungulia fursa za kiuchumi na Agosti 24 itakuwa na fainali ya mechi ya soka ya timu za skuli ambazo mbili kati ya timu 16 za Visiwani Zanzibar zilizokuwa zikichuana zimetinga fainali,” alisema Hindi.

Tamasha hilo lilianza mwaka 2016 likijulikana kama Siku ya Samia (Samia Day) kabla ya kubadilishwa na kuwa Kizimkazi Day na miaka minne iliyopita lilibadilishwa jina na kuitwa Tamasha la Kizimkazi.

Related Posts