Kampuni ya siri nyuma ya mgogoro wa P-Square

NI miaka mingi sasa wanamuziki pacha Peter na Paul Okoye wanaounda kundi la P-Square kutoka Nigeria hawana maelewano na hivyo kila mmoja kushika njia yake kimuziki na kifamilia, lakini hiyo haijawa mwarobaini wa tofauti zao.

Kampuni ya siri ndiyo ipo nyuma ya mgogoro wao ambao umeshuhudiwa hivi karibani katika mitandao ya kijamii ikiwa ni matokeo ya kushindwa kutatua mizozo ya kibiashara iliyodumu kwa muda mrefu. 

P-Square, wakali wa miondoko ya Afrobeat, R&B na Dancehall walianza kuvuma baada ya kutoa wimbo wa Senorita (2003), kisha albamu ya pili Get Squared (2005) ambayo iliwapa nafasi ya kuwania tuzo za MTV Europe.

Kwa miaka zaidi ya 10 ya kufanya kazi pamoja walifanikiwa kutoa albamu sita ambazo ni Last Nite (2003), Get Squared (2005), Game Over (2007), Danger (2009), The Invasion (2011) na Double Trouble (2014).

Hadi sasa P-Square wanajulikana kila sehemu kwa nyimbo zao kali kama Temptation, Do Me, Bizzy Body, Personally, Chop My Money, Alingo, Beautiful Onyinye, Shekini, Bring it On, Gimme Dat, Roll It, Ifunanya na kadhalika.

Wakiwa wasanii wa kwanza Nigeria kuingia tano bora chati ya SNEP Ufaransa, P-Square walifanikiwa kuwania tuzo kubwa ikiwemo BET, Soul Train, MTV Europe na MOBO huku wakishinda tuzo za KORA, MTV Africa, Channel O na kadhalika.

Baada ya mafanikio makubwa kimuziki mambo yalianza kwenda mrama kwa kundi hilo. Mwaka 2015 dalili za awali zilionekana kuwa hali siyo shwari.

Hiyo ni kufuatia Paul kupitia mtandao wa X zamani Twitter kudai ameandika asilimia 90 ya nyimbo za P-Square, kauli ambayo kairejea hivi karibuni. Ingawa Peter hakujibu ila ukweli ni kwamba alihisi mchango wake umedharaulika.

Mwaka 2016 hali ilikuwa mbaya zaidi kwani migogoro ya kibiashara iliibuka na kusikika nje. Peter hakukubaliana na kaka yao mkubwa na aliyekuwa meneja wao, Jude Okoye kwa mambo mengi, hivyo alitoka hadharani na kutangaza kumfuta kazi.

Peter alimtuhumu Jude kwa usimamizi mbaya wa fedha na miradi yao, hivyo kutaka mabadiliko ya menejimenti. Wakati hayo yakijiri, Paul alimuunga mkono Jude kitendo kilichochochea mgogoro huo.

Baada ya miaka miwili ya mzozo huo, Peter alitangaza kujiondoa katika kundi la P-Square kwa sababu zake binafsi ila kwa nje wengi walifahamu uamuzi huo ulichangiwa na kutokuelewana kwao.

Septemba 2017, video ilisambaa mtandaoni ikiwaonyesha wakibishana vikali katika ofisi ya mwanasheria wao chanzo cha mabishano yao ni kutoelewana kuhusu suala la meneja wao, Jude.

Licha ya kumtuhumu Jude kwa usimamzi mbaya wa fedha zao, pia Peter alidai meneja huyo amekuwa akimpendelea Paul kwa vitu vingi ukilinganisha na yeye.

Hata hivyo, Paul alikanusha madai hayo ila huo ukawa mwanzo wa kila mmoja kufanya muziki peke yake ambapo Peter alitumia jina la Mr P huku Paul akijitambulisha kama Rudeboy.

Baada ya takribani mwaka mmoja wa utengano, Desemba 2018, P-Square walitumbuiza pamoja na kufufua matumaini huenda kundi hilo likarejea kufanya kazi kama ilivyokuwa awali, lakini haikuwa hivyo kisa kampuni ya siri.

Je, kampuni ya siri ni kitu gani hasa? Mapema wiki hii Peter kupitia mitandao ameandika barua ya wazi kwenda kwa Paul na kujibu madai yaliyotolewa na pacha mwenzake huyo hivi karibuni.

Ikumbukwe Paul akihojiwa na kituo kimoja cha redio huko Nigeria alidai Peter alimshtaki katika Tume ya Makosa ya Kiuchumi na Kifedha (EFCC) kwa madai ya kufuja fedha za mirabaha ya P-Square.

Ila katika barua yake Peter alikanusha hilo na kuibua kile alichoita kampuni ya siri, akisema waliunda kampuni iitwayo Northside Entertainment ili kukusanya mirabaha yao lakini akaja kugundua kuna kampuni nyingine ya siri, Northside Music inayofanya kazi hiyo.

Alisema uchunguzi wake ulibaini Northside Music imekuwa ikichukua fedha kutoka Northside Entertainment, na kibaya zaidi kampuni hiyo ya siri wakurugenzi wake ni Jude na mkewe ndipo akawaita EFCC na hakuna sehemu alipomtaja Paul kuhusika na jambo hilo.

“Kile kilichonikera zaidi ni kubaini kwamba kwa miaka mingi mamilioni ya dola yalikuwa yanapelekwa kwenda kwenye hii kampuni ya Northside Music kutoka kwenye kampuni yetu wenyewe ya Northside Entertainment,” alisema Peter.

“Nilipomfuata Paul kumuuliza mazungumzo yetu yaliishia kukasirishana, alisema ‘Peter nenda kafanye lolote baya unaloweza’. Katika hatua hii sikuwa na chaguo lolote zaidi ya kuripoti jambo hili katika mamlaka na kuchukua hatua za kisheria,” alisema.

Baada ya Peter kuripoti kwa EFCC kuhusu kampuni hiyo ya siri, Jude alikamatwa na kuhojiwa ikiwa ni pamoja na akaunti zake za benki kufungwa. Pia watu wengine akiwemo Paul ambaye hakutajwa walihojiwa.

“Upelelezi wa EFCC ulibaini kuwa Northside Music imekuwa ikikusanya mirabaha ya P-Square kwa miaka mingi. Mirabaha hii ilitumwa kwenye maduka ya kubadilishia fedha kisha kuhamishiwa kwenye akaunti binafsi ya Jude,” alisema. 

“Na kwa kuangalia taarifa za miamala ya Jude tukabaini kwamba baada ya fedha kuingia kwake kulikuwepo na miamala mingi ambayo ilikuwa inatumwa kwenda kwa Paul pasipo mimi kujua,” alisema Peter katika barua yake hiyo ya Agosti 12, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Peter, anachosubiri ni ripoti ya mwisho kutoka EFCC kisha kupeleka jambo hilo mahakamani kwa ajili ya hatua za kisheria zaidi. Na atakayeshtakiwa ni kaka yao mkubwa, Jude Okoye na mkewe ambao ndio wakurugenzi wa Northside Music, kampuni inayotajwa kuwa ya siri.

Related Posts