Tanga. Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mlezi wa CCM Mkoa wa Tanga, Hemed Suleiman Abdullah amesema hawatabeba wanachama wachafu, ambao wanakiuka taratibu na kanuni za chama kwenye shughuli zao za kisiasa katika chaguzi zinazokuja.
Akizungumza na wanachama wa chama hicho kwenye ziara yake ya siku nne ya kuongea na wanachama wa CCM, kwenye wilaya tisa za kichama mkoa wa Tanga, amesema wao kama viongozi wanayo taarifa kuhusu wanaoharibu taratibu kwa makusudi kwa kuandaa wagombea wao.
Kadhalika amesema makundi hayo ya wanachama yanaandaa wenzao ambao kwa wakati mwingine wao kama viongozi wanawafuatilia au wamebaini ni wachafu, na hawawezi kupandishwa jukwaani na kunadiwa hivyo wanaofanya mipango hiyo waache.
“Msibebe mizigo isiyobebeka na sisi tuliokuwa madarakani tusiwe na hofu. Ukifanya vizuri CCM tutakubeba na ukifanya vibaya tunakuacha hii haina kunong’ona kama ni mchafu hatuwezi kukupandisha jukwaani,” amesema Abdullah.
Pia ameagiza viongozi waliopo kwenye nafasi zao kwa sasa, waachwe wafanye kazi kwani kuna taarifa amezisikia kuwa kuna watu wanaharibu utaratibu wa chama, kwa kuandaa viongozi wao wakati wenye nafasi hizo bado wapo madarakani.
Wanachama wa CCM wasivuruge taratibu kwa maslahi ya mtu na badala yake wahakikishe wanasimama na yule ambae yupo madarakani kwa utaratibu uliopo na atakayebainika anaharibu taratibu za chama atachukuliwa hatua.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Rajabu Abdulrahman amesema katika uchaguzi unaokuja wa wenyeviti wa serikali za mitaa na vijiji, hawatawarudisha wale wote ambao wamekuwa chanzo cha migogoro ya ardhi.
Amesema chama kimefuatilia na kubaini wapo baadhi ya viongozi hao kwa makusudi wameanzisha migogoro ya ardhi kwa manufaa yao na kwa sababu hizo, wale wote ambao watathibitishwa wamefanya hayo hawatarudishwa kwenye nafasi zao.
Mwenyekiti huyo amesema chama hakiwezi kuwabeba viongozi ambao badala ya kuwasaidia wananchi, wamekuwa ni chanzo cha kusababisha matatizo kwao.
Kwa upande wake, Mbunge wa Tanga Mjini, Ummy Mwalimu amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha Bandari ya Tanga ambapo zaidi ya Sh249 bilioni zimetumika katika kuiboresha bandari hiyo ambayo sasa imewezesha kuhudumia meli kubwa.