Rombo. Katika Kijiji cha Kwalakamu, wilayani Rombo Mkoa wa Kilimanjaro, kijana mwenye umri wa miaka 14, James Efram licha ya kuwa na umri mdogo, amebeba mzigo mzito wa majukumu makubwa yanayozidi umri wake.
Ni mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi Mamonjo iliyo jirani na anapoishi. Hata hivyo, masomo kwake si kipaumbele tena, jukumu kubwa zaidi limekuwa malezi ya familia.
Anaishi na familia yake katika nyumba ya udongo iliyojaa matobo na paa linalovuja wakati wa mvua hivyo kuhatarisha maisha yao.
Hata hivyo, nyumba hii ndiyo kimbilio la familia hii, ambayo mama yake mzazi anapambana na tatizo la changamoto afya ya akili, akiwa hana uwezo wa kujitunza mwenyewe. Baba yao alifariki dunia mwaka 2011.
James akiwa mtoto wa pili ndiye katika familia, amelazimika kuwa nguzo kwa wadogo zake watano, ambao wote wanamtegemea, baada ya dada yeke kukimbia nyumbani kutokana na ugumu wa maisha.
Ili kutimiza majukumu haya, James hutumia muda mwingi kuombaomba kijiji hapo wakati mwingine akipokewa kwa maneno na kuitwa kwa majina yenye dharau.
Hata hivyo, James amesema hajakata tamaa, anajua kuwa familia yake inamtegemea.
Mwananchi imefika katika nyumba hiyo, ambako James anasema hawana kitanda wala godoro, hivyo hutandika nguo chini na kulala.
“Changamoto niliyonayo ni kubwa kwa kuwa sehemu ya kulala hatuna ni kama tunalala nje, chakula hatuna, wakati mwingine kwa kuwa mimi ndiye ninayetegemewa kwenye familia siendi shule nalazimika kuingia mtaani kuomba ili hawa wadogo zangu watano pamoja na mama waweze kupata chochote,” amesema.
“Nikitoka shuleni jioni nikiwa na sare zangu naenda kuomba msaada wa chakula mtaani wadogo zangu wasilale bila kula,” amesema.
Waliompokea kwa maneno ya faraja na kumsaidia, James anawashukuru, akiwamo mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda, ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kwa kushirikiana na wadau, amesema watasaidia kuboresha maisha ya familia hiyo.
Kati ya waungwana waliompokea na kumshika mkono ni walimu wake sita waliokubali kuchangia Sh5,000 kila mmoja kutoka kwenye mishahara yao.
Mwalimu mkuu wa shule anayosoma kijana huyu, Spensioza Kwayu, anasema walibaini changamoto zinazomkabili baada ya kutoonekana shuleni kwa wiki mbili.
Kupitia kwa mwalimu wake wa darasa na mwalimu wa nidhamu walienda nyumbani kwa kina James kujua kulikoni haonekani shuleni.
James alikutwa nyumbani akiwa na wenzake, katika hali ya unyonge alijieleza alikosa viatu vya shule na mahitaji mengine, kutokana na hali ya familia yake.
Mwalimu mkuu amesema baada ya kuelezwa yaliyojiri, aliitisha kikao cha walimu wakaridhia kumsaidia.
Waswahili husema chanda chema huvikwa pete, moyo wa huruma uliwaingia walimu hao si tu kutokana na hali ya maisha ya James, bali pia licha ya hali yake ngumu, bado anafanya vizuri darasani.
Kwa mujibu wa walimu wake, James tangu ajiunge na shule amekuwa akifanya vizuri darasani ikiwa ni pamoja na kushika nafasi ya kwanza kwenye mitihani.
Hata wakati alipokosa kuhudhuria shuleni kwa wiki mbili iliwalazimu kumfuatilia kujua kulikoni.
Profesa Mkenda anaungana na Taasisi ya Glad’s welfare iliyojitolea kumsaidia mwanafunzi huyo.
“Nitoe wito kwa Watanzania, hii kesi ni moja tu, lakini zipo nchi nzima, hivyo naomba iwe ni fundisho kwetu sisi sote tujitahidi kuangalia zile kaya ambazo zina changamoto kama hii, hivyo tuziibue ili tuwasaidie hawa watoto kurudi shuleni,” amesema Profesa Mkenda.
Glads Lyamuya, amesema waliguswa na changamoto ya mtoto huyo hivyo kupitia taasisi ya Glads welfare wameanza mchakato wa kuisadia familia hiyo kwa kuijengea nyumba.
Simulizi ya James imejaa uthubutu, uvumilivu, na upendo wa dhati kwa familia yake, licha ya changamoto nyingi.
Kwa umri wake, angetamani kuwa na maisha ya kawaida ya shule na michezo, lakini amejikuta katika nafasi ya kulea na kutunza wakati yeye mwenyewe bado anahitaji kulelewa.