Askofu KKKT ashinda rufaa kesi madai ya kashfa

Iringa. Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Ziwa Tanganyika ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambele Mwaipopo, ameshinda rufaa ya madai ya Sh250 milioni, iliyofunguliwa na mwanazuoni Dk Stephen Kimondo.

Hii ni baada ya Jaji Dunstan Ndunguru wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, kuitupa rufaa hiyo namba 9253 ya mwaka 2024 iliyofunguliwa na Dk Kimondo, akipinga hukumu ya kesi ya madai ya kashfa aliyoshindwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa.

Mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa, Dk Kimondo aliyekuwa Mhadhiri Mwandamizi Chuo Kikuu Iringa (UOI), alifungua kesi ya madai ya fidia ya Sh250 milioni, akidai Askofu Mwaipopo alikuwa ametoa tuhuma za uongo dhidi yake.

Katika kesi hiyo, Dk Kimondo alidai Juni 17, 2021, Askofu Mwaipopo alimwandikia barua Makamu Mkuu wa Chuo cha UOI, Profesa Ndeliliyo Urio, akieleza mhadhiri huyo alikuwa akimtongoza mmoja wa wanafunzi.

Katika barua ya Askofu Mwaipopo ambaye ni sehemu ya mwenendo wa kesi hiyo, kwenda kwa Profesa Ndeliliyo, alieleza kuwa mwanafunzi huyo aliyekuwa akisoma Stashada ya Thiolojia, amemshirikisha kuwa Dk Kimondo anamtaka kimapenzi.

“Huo ni unyanyasaji na kutokana na hali hiyo kama kiongozi wa KKKT Dayosisi ya Ziwa Tanganyika, na mlezi wa kiroho wa (jina limehifadhiwa) nasema wazi kwamba jambo hili halikubaliki,” alisema Askofu Mwaipopo katika barua hiyo.

Askofu Mwaipopo katika barua hiyo alinukuliwa akisema mwanafunzi huyo kukutana na vitendo kama hivyo ni kutweza na kudhalilisha utu wake, kufifisha wito na imani yake na imemfanya mwanafunzi huyo anyong’onyee.

Alieleza ni wazi kwamba baada ya mwanafunzi kukataa kufanya mapenzi na Dk Kimondo, usalama wake katika mazingira anamoishi na kimasomo yako shakani na kwamba, ana imani chuo hicho hakitafumbia macho kitendo hicho.

“Chuo Kikuu Iringa ni fahari ya KKKT na dayosisi zake. Wakati wote ni maombi yangu kuwa chuo hiki kiwe mfano bora wa kuigwa kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Vinapotokea vitendo ambavyo sivyo, vinapaswa kushughulikiwa ipasavyo,” alieleza katika barua hiyo.

Dk Kimondo alidai kutokana na tuhuma hizo, Profesa Ndeliliyo aliitisha kikao cha kamati na kumtaka yeye ahudhurie kwa ajili ya kuchunguza kitu ambacho hakina ukweli, hivyo akaomba Mahakama itamke kuwa askofu alikuwa amemkashifu.

Pia, aliomba Mahakama imwamuru askofu amlipe fidia ya jumla ya Sh250 milioni kwa kumkashifu, kulipa gharama za kuendesha kesi hiyo, na Mahakama iamuru apewe nafuu nyingine itakavyoona inafaa.

Askofu Mwaipopo alikanusha madai hayo na baada ya Mahakama kusikiliza shauri hilo, iliona Dk Kimondo alishindwa kuthibitisha madai yake na kuitupa kesi hiyo, jambo ambalo hakuridhika nalo.

Hoja za rufaa zilivyokuwa

Kutokana na hukumu hiyo, Dk Kimondo alikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa akiegemea sababu nne, ikiwamo hakimu alikosea kisheria kwa kushindwa kutafsiri vipengele muhimu vya kashfa na uwepo wa matamshi ya kashfa.

Mbali na hoja hiyo, alisema hakimu aliyesikiliza shauri lake alikosea kisheria kwa kushindwa kuchambua ushahidi mzito alioutoa kortini na badala yake, akaegemea katika ushahidi dhaifu na unaojikanganya uliotolewa na mjibu rufani, yaani askofu.

Dk Kimondo akasema hakimu alikosea kisheria kwa kupuuzia kumpa tuzo ya fidia yenye thamani ya Sh250 milioni kwa kuwa, kwa heshima yake aliumizwa na matamshi hayo na pia alikosea aliposema ameshindwa kuthibitisha madai yake.

Kupitia kwa wakili wake, mwanazuoni huyo aliiomba Mahakama ikubali rufaa yake ingawa hata hivyo, katika hukumu iliyotolewa na Jaji Ndunguru Agosti 16, 2024 alisema baada ya kuchambua na kupima ushahidi, hakimu alikuwa sahihi.

Kupitia kwa wakili wake aliyetajwa kwa jina la Chengula kwenye nyaraka za hukumu, Dk Kimondo alisema hakuna ubishi kuwa mjibu rufaa (askofu) alichapisha matamshi yaliyokuwa na tuhuma nzito yakieleza alitaka kufanya ngono na mwanafunzi.

Alieleza katika kikao cha kamati kilichoitishwa chuoni hapo kuchunguza tuhuma hizo, mwanafunzi huyo alikanusha kufuatiliwa kimapenzi na mhadhiri huyo na kwamba, matamshi ya askofu yalimshushia heshima katika jamii.

Wakili huyo alieleza Askofu Mwaipopo hawezi kujitenga na mzigo huo kwa kuwa alichapisha maneno kutoka kwa mwanafunzi huyo ambayo yalikuwa ni ya kuambiwa na wala hakuiambia kamati kuwa alikuwa akimtongoza.

Majibu ya Askofu Mwaipopo

Kupitia kwa wakili wake ambaye naye alitajwa kwa jina moja la Nyato, Askofu Mwaipopo aliiambia Mahakama kuwa hakuchapisha maandishi ya kashfa dhidi ya Dk Kimondo kupitia kwa Profesa Ndeliliyo kama inavyodaiwa.

Badala yake alisema, Profesa Ndeliliyo ndiye alikuwa na wajibu wa kuchukua hatua dhidi ya utovu wa nidhamu wa mrufani kwa mwanafunzi wake aliyekuwa akisomea mafunzo ya dini au thiolojia.

Askofu alisema hatua ya mwanafunzi huyo kukataa mbele ya kamati kuwa alikuwa anafuatwa-fuatwa kimapenzi na mrufani, haikuwa na maana kwamba alikuwa amemkashifu na kwamba, Mahakama ilipima na kuona ameshindwa kuthibitisha.

Kulingana na hoja zake, Askofu Mwaipopo alisema maneno yaliyopo katika barua hiyo yalibeba maoni ya haki na kwamba, hakuna Mahakama ambayo kwa maneno hayo, ingeweza kushawishika na kuweka msimamo kuwa ni ya kashfa.

Alisema maneno yaliyomo katika barua yalikuwa ni mawasiliano kati ya taasisi na taasisi, ambazo kila moja ilikuwa na wajibu wa kuhakikisha mwanafunzi anamaliza masomo yake kwa manufaa ya kanisa na jamii nzima kama mchungaji.

Alieleza mwanafunzi huyo alitoa ushahidi kortini kwamba alikuwa tayari kukatisha masomo kutokana na vitendo vinavyokera vya mrufani na kwamba, alitoa taarifa hiyo kwa askofu wake ambaye pia ndiye mwajiri wake.

Wakili huyo alieleza maneno yanayodaiwa kuwa ya kashfa hayakusambazwa popote badala yake ni barua iliyotumwa kwa mamlaka ya chuo ambayo yana wajibu wa kutunza masomo kwa wanafunzi wanaosoma katika chuo hicho.

Katika hukumu aliyoitoa Agosti 16, 2024, Jaji alisema amepitia kwa umakini hoja za pande zote mbili lakini kwa kuwa ndiyo Mahakama ya kwanza ya rufaa, atachambua ushahidi wa Mahakama ya chini na kuja na hitimisho lake.

Jaji alisema ushahidi uliopo katika kumbukumbu za Mahakama ni kuwa matamshi ya kashfa yanayolalamikiwa yapo katika barua ya askofu ya Juni 17, 2021 ambayo aliiandika kwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Iringa na akainukuu barua hiyo.

Alieleza ni ukweli barua iliandikwa na mjibu maombi (askofu) na ilitumwa kwa mtu wa tatu lakini ilimhusu mrufani katika rufaa hiyo na swali kuu ambalo Mahakama inajiuliza ni kama maneno yaliyomo katika barua hiyo ni ya uongo.

Jaji alisema kwa ushahidi wa mwanafunzi, mrufani na mawasilisho ya mawakili, matamshi hayo yanadaiwa kuwa ni ya uongo kwa sababu tu mwanafunzi alipoitwa kwenye kamati, hakuiambia Dk Kimondo alikuwa akimtaka kimapenzi.

“Kwa hiyo maneno ya mjibu rufaa ilikuwa ni uongo. Siyo hiyo tu, lakini sababu ya pili ni kwamba mrufani anaona maneno hayo ni ya uongo kwa kuwa mjibu maombi hakushuhudia kile ambacho mrufani alidaiwa kukifanya,” alisema Jaji Ndunguru.

Tofauti na msimamo huo,  mwanafunzi mwenyewe alitoa ushahidi kwamba mrufani alikuwa akimtaka kimapenzi na kwamba alimripoti kwa mjibu maombi kama askofu wake, mfadhili wake na pia akatoa taarifa kwa mumewe.

Jaji alisema askofu alieleza aliandika kile alichoelezwa na mwanafunzi huyo.

Kwa mtizamo huo, Jaji alisema ana maoni kuwa maneno yaliyosemwa na mjibu maombi (askofu) hayakuwa ya uongo kwa kuwa aliandika kile ambacho alielezwa na mwanafunzi huyo na kwamba, hakuwa na dhamira ya kumkashifu mrufani.

“Tuchukulie maneno yale ni uongo kama ilivyoelezwa, mjibu maombi alichukulia kile alichoelezwa kuwa ni kweli,” alisema Jaji na kuongeza:

“Hata kama haikuwa kweli, lakini kwa kuwa mrufani ameshindwa kuthibitisha dhamira mbaya ya mjibu rufaa wakati mjibu rufaa ametoa ushahidi kujenga kuwa alifanya hayo kwa uaminifu bila nia mbaya, mjibu rufaa anakingwa na sheria.”

Jaji alisema ushahidi kuwa Mwaipopo ni Askofu wa Dayosisi ya Tanganyika na mwanafunzi ni wa dayosisi hiyo aliyekuwa akisoma Iringa, akifadhiliwa na dayosisi ambayo ni askofu, yeye kama kiongozi ana wajibu wa kufanya mawasiliano.

Alieleza mawasiliano hayo yalifanyika kutokana na wajibu aliokuwa nao kwa jamii ambao unahusiana na tabia za wafanyakazi na masuala ya siri, pia na mawasiliano hayo yanafanyika kwa lengo la kulinda kama ilivyo katika kesi hiyo.

Jaji alisema baada ya kuchambua ushahidi huo, ni tafakari yake thabiti kuwa Mahakama ya chini iliyosikiliza shauri hilo ilichambua vyema vigezo vya madai ya kashfa, kuvipima na kuchambua ushahidi hivyo anabariki uamuzi wa Mahakama.

Related Posts