ONGEA NA AUNT BETTIE: Mdogo wangu anamsalandia mke wangu

Habari Aunt, naomba ushauri, mdogo wangu anaonekana wazi kumtaka shemeji yake (mke wangu). Nimesema hivyo kwa sababu naona utani usiokuwa na mipaka umezidi. Nashindwa kumkanya kwa sababu ni mdogo kwangu kiumri. Nifanyeje?

…..Unanishangaza, unashindwa kumkanya mdogo wako utamkanya nani tena!

Kwanza kabisa unapo pa kuanzia, anza kumkanya mkeo asikubali utani uliopitiliza na shemeji yake, kwa sababu mwishowe watakuwa hawaheshimiani kabisa na atakuwa akimweleza kitu hafanyi.

Ili kuwe na heshima kusiwe na utani kupita kiasi. Ukimkanya mkeo akiwa na mipaka ya utani na shemeji yake, utakuwa umemaliza jambo.
Kwa faida ya mdogo wako, ni vema ukamwambia kwa utulivu ili atambue kuwa huyo ni shemeji yake na anapaswa kumheshimu.

Kupitia somo kuhusu kuwa na mipaka ya utani na shemeji yake, utamsaidia popote atakapokuwa kuheshimu wanawake, hasa wake za watu. Kwani inaonekana wazi hana adabu na anahitaji kufundishwa.

Ila unapomkanya sema naye taratibu na umpe nafasi mara chache akueleze jambo kuhusu shutuma hizo, pengine anajua kumtania shemeji, kuwa naye karibu ndiyo kibinadamu.

Wengine huwa wagumu kufikiria mambo mara mbili, linalowajia ndilo wanalolifanya ilimradi kichwani kwao wanakuwa na nia madhubuti isiyokuwa na chembe ya shaka.

Hawajali wengine wanafikiria nini kuhusu wanayoyafanya, ninamaanisha pengine huyo mdogo wako hana hili wala lile kuhusu kumtamani shemeji yake.

Anajua utani kati ya mtu na shemeji yake ndiyo hasa mahali pake.
 

Kaingia mitini baada ya kunitolea barua ya uchumba

Nilikuwa na uhusiano na mwanaume, akanitolea barua akidai anataka tuoane. Lakini tangu afanye hivyo mawasiliano yetu yamekatika kabisa. Nachanganyikiwa na ninaona aibu.
Nifanyeje?

Pole. Usione aibu kwa sababu suala la barua lilihusisha familia kwa maana ya wazazi au jamaa zako kuipokea, hivyo washirikishe. Pia kwa kawaida suala la barua huhusisha mshenga, hivyo familia yako itawasiliana na mshenga kwa ajili ya kuuliza familia ya mchumba wako nini kimetokea.
Wao wanaweza kusaidia kujua kuna nini katika ukimya wake.

Jambo la muhimu kufanya ni kujiandaa kukubali majibu watakayokuja nayo, ikiwa ameamua kuahirisha kukuoa au vinginevyo.
Usifanye kitu kibaya, huwezi kujua, inawezekana Mungu kuna jambo amekuepusha nalo.

Iwapo kuna mahali ulikosea ukamkasirisha jitahidi mkae pamoja ili kumaliza tofauti zenu. Jambo la muhimu kama unaona hayupo tayari usimlazimishe ili usije kupata shida mbele ya safari.

Anaweza kukubali kuwa pamoja na wewe kwa ajili ya kuwaridhisha wazazi na jamaa zake, kumbe anajilaumu kuwa na wewe na amekata shauri kukuacha, ila kwa shinikizo amekurudia, hapo utateseka, maana atakuwa na wewe lakini hana mapenzi.

Kisha suala la kuoana ni la watu wawili, kama mmoja hayupo tayari hakuna haja ya kuona aibu.

Hao waja unaowaogopa kuwa watakucheka hawatakuwepo kwenye ndoa yenu.

Hivyo akikupa jibu la maana kubali na muendeleze safari mliyoianza, ukiona majibu na tabia zake hazieleweki amua vinginevyo, hakuna makaburi ya walioachwa kwamba wakiachwa wanakufa, kama maelewano hakuna busara ni kila mmoja kufanya mambo yake.

Sikushauri uachane naye, bali nakupa angalizo kuwa makini, iwapo atakuja sikiliza kila neno analolisema kuwa ndiyo sababu ya kuingia mitini, kabla ya kukurupuka kumkubalia, usipokuwa na msimamo sasa itakuwa ndiyo tabia yake akiamua anaondoka kisha anarudi anakulaghai maisha yanaendelea.

Related Posts