Fikiria uko jikoni ukiandaa chakula cha jioni. Watoto wako wawili wadogo Fred na Linda wanacheza sebuleni. Salome yuko mezani akifanya kazi za shule.
Mara unasikia mlio wa kitu kuvunjika sebuleni. Unapatwa na wasiwasi. Unakwenda haraka kujua kilichotokea. Maji yanatiririka sakafuni. Chupa ya chai imedondoka na kupasuka. Unakasirika.
Fred, mwanao mdogo, haonekani kuwa na wasiwasi. Haraka anamsemea mkubwa, ‘Sio mimi mama…ni Linda!’ Kwa hasira unamtazama Linda. Uso wake kweli unaonyesha wasiwasi. Kwa ukali unamuuliza, ‘Wewe ndo’ umevunja chupa?’
Anasita. Amejaa wasiwasi. ‘Nauliza ni wewe?’ unarudia. Kwa haraka anajibu huku akitikita na kichwa, ‘A-a-a! Sio mimi mama!’
‘Nani amevunja chupa?’ Unauliza kwa hasira kali. Mdogo anasisitiza, ‘Ni Linda!’ Unamshika mkono kwa ghadhabu kubwa huku ukilalamika, ‘Kwa nini umevunja chupa?’
Salome anaona aokoe jahazi. ‘Usimchape Linda mama. Aliyevunja chupa ni Fred!’ ‘Fred?’ Unakasirika kudanganywa na mtoto wa miaka miwili. Mbaya zaidi haonekani kujutia anachokifanya.
Kwa nyakati na sababu tofauti watoto hudanganya. Kudanganya ni kutoa habari zisizo za kweli. Tena, wakati mwingine, watoto hudanganya kama mbinu ya kumpendeza mzazi. Kuna mazingira, uongo hutumiwa kwa nia njema ya kutokumkatisha tamaa mzazi.
Hata hivyo, uongo, unaoanza kwa nia njema utotoni, ukiachwa ukomae ni hatari kwa mustakabali wa mtoto. Uongo huu mbeleni hubeba nia mbaya. Huumiza watu. Huharibu uhusiano na watu. Hufanya mtu asiaminike. Uongo pia ni dhambi. Dini zote zinakataza uongo.
Hatuzaliwi na tabia ya kudanganya. Tunajifunza. Fred tuliyemwona hapo juu kajifunza kudanganya. Fred ametumia uongo kukidhi matakwa ya mazingira ingawa kwa umri wake, hana uwezo wa kutunga uongo.
Ukimuelewa Fred utaona anachokifanya ni kumridhisha mama yake. Fred anajua kuvunja chupa ni kosa kwa sababu mama amekasirika. Hatamani kuwa upande wa kumuudhi mama yake.
Kwa sisi watu wazima Fred anadanganya. Lakini yeye haoni hivyo. Anatumia ‘uongo’ kusema matamanio yake. Anaposema, ‘Ni Linda amevunja’ maana yake anatamani kwa wakati huo angekuwa kama Linda. Hapendi hali aliyojikuta nayo.
Fred anatumia uongo kama namna ya kulinda uhusiano wake na mzazi. Kwa kuzingatia umuhimu wa uhusiano na mzazi, Fred anakuwa tayari kuulinda kwa gharama yoyote.
Fred anajua matokeo ya kukiri kosa ni kukaribisha adhabu. Ili awe salama lazima aseme kile anachojua ndicho mzazi anachokitarajia. Kudanganya ni kuepusha shari na mzazi wake.
Aidha, katika umri fulani, mtoto huweza kutumia uongo kama silaha ya mashambulizi. Hudanganya kama namna ya kumuumiza mtu mwingine. Inawezekana Fred analipiza kisasi kwa Linda. Huenda uongo unatumika kumwingiza mwenzake kwenye matatizo.
Tufanyeje kupunguza uwezekano wa watoto kudanganya? Kwanza, ni muhimu tusiweke mazingira ya kudanganywa. Badala ya kuomba kudanganywa kwa maswali ya uchokozi, kama alivyofanya mama yake Fred, shughulika na kosa moja kwa moja.
Lakini pia, ni muhimu kushughulikia uongo mapema. Kupuuza uongo ‘mdogo’ unaoubaini ni kukomaza tabia ya uongo wa makusudi mbeleni. Shughulika nao kila unapojitokeza.
Kadhalika, tuepuke mazingira ya kuonekana tunawaadhibu watoto kwa kusema ukweli. Ikiwa mtoto amekiri kuwa ndiye aliyevunja sahani kwa nini unamwadhibu? Ikiwa mtoto amekiri makosa na ameelewa, mpongeze kwa kuwa mkweli. Unapofanya hivyo hulei makosa yake, bali unampa motisha ya kuwa mkweli.
Mwisho, mfundishe mtoto kuwa mkweli kwa kuonyesha mfano. Mtoto hawezi kuwa tofauti na mzazi wake. Usipokuwa na tabia ya kusema ukweli hata katika mazingira magumu, unamfundisha mtoto kudanganya. Unapoahidi jambo kwa mwanao, tekeleza. Ikitokea umeshindwa kutekeleza, omba msamaha.
Usitumie uongo kufunika makosa yako. Anapouliza swali gumu, mpe maelezo rahisi ya kweli badala ya uongo ‘mzuri’ ambao, hata hivyo, anaweza kuugundua baadaye.
Kadhalika, usiwadanganye watu mbele yake. Usimpe mtu majibu ambayo mtoto atajua ni ya uongo. Mfano, uko nyumbani umepigiwa simu na mkuu wako wa kazi akiuliza uliko. Unaposema uko ofisini na mtoto anakusikia, mtoto ataona uongo ni sehemu ya maisha. Usishangae akikudanganya na wewe siku nyingine.