Mahakama yapigilia msumari adhabu ya kifo aliyekutwa na simu ya marehemu

Arusha. Mahakama ya Rufani, imebariki adhabu ya kunyongwa hadi kufa aliyohukumiwa Orestus Mbawala, ambaye alikutwa na hatia ya kumuua Mwalimu Christopher Ndimbo na kumuibia pikipiki yake.

Orestus na mtu mwingine ambaye hahusiki katika rufaa hiyo, Cosmas Mbena, walishtakiwa kwa tuhuma za mauaji kinyume na kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu.

Ilidaiwa Juni 14, 2016 katika eneo la Making’inda ndani ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Orestus na Cosmas walimuua Christopher Ndimbo, aliyekuwa mwalimu.

Rufaa hiyo inatokana na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea uliotolewa Septemba 28, 2022 ambayo ilitegemea zaidi kukiri kwa Orestus katika maelezo ya onyo pamoja na kukutwa na simu ya marehemu.

Mahakama ya Rufani iliyoketi Songea, ilitupilia mbali rufaa hiyo ya jinai namba 486 ya mwaka 2022 iliyokuwa imekatwa na Orestus, baada ya kujiridhisha upande wa mashitaka ulithibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka, na Orestus alikutwa na simu ya marehemu muda mfupi baada ya kifo chake.

Uamuzi huo wa mahakama ya rufaa ulitolewa Agosti 15, 2024 na majaji watatu ambao ni Augustine Mwarija, Rehema Kerefu na Omar Othman Makungu, na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama.

Katika kesi hiyo, upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi 12 na vielelezo 10. Baada ya kusikilizwa kwa kesi ya upande wa mashitaka uligundua umeshindwa kuthibitisha kesi dhidi ya Cosmas hivyo kumuachia huru.

Mahakama hiyo iliona kesi hiyo imethibitishwa dhidi ya Orestus bila kuacha shaka yoyote na kupatikana na hatia, na kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Ilidaiwa mahakamani Juni 11, 2016 saa tano usiku, marehemu alichukua pikipiki na kwenda kufanya biashara ya kusafirisha abiria, ila hakurejea nyumbani tarehe hiyo hivyo mkewe kwenda kutoa taarifa Polisi kufuatia simu yake ya mkononi kutopatikana.

Ilidaiwa laini ya simu ya marehemu ilikuwa imetolewa kwenye simu hiyo ila Polisi walifuatilia eneo ambalo simu hiyo ilikuwepo na siku kadhaa baadaye kufanikiwa kukuta mwili wa marehemu kwenye kichaka ukiwa umeoza  huku ukiwa na jeraha sehemu ya kichwani lililoonyesha alipigwa na kitu kizito.

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songea kwa ajili ya kuhifadhiwa na kufanyiwa uchunguzi, ambapo ilibaini alifariki dunia kutokana na jeraha la kichwa.

Baada ya kupatikana kwa mwili wa marehemu, Polisi waliendelea na uchunguzi na ufuatiliaji wa simu ya mkononi ya marehemu, ambayo ilibainika kutumika kwa namba nyingine na kusajiliwa kwa jina la mtu aliyekuwa Njombe.

Shahidi wa tano Ibrahimu Mtehule katika kesi hiyo, alidai akiwa kazini kwake kwenye mashine ya kusaga, Orestus alifika na kumweleza alikuwa akiuza simu na kwa siku hiyo alikuwa ametembelewa na shahidi wa tano ambaye aliinunua simu hiyo kwa Sh450,000, ambayo baadaye ilikutwa kwa Orestus akiitumia.

Aliyefanikisha kukamatwa kwa Orestus ni binti yake Pendo Orestus aliyekamatwa Songea ambapo alieleza simu hiyo ilikuwa ikitumiwa na baba yake na kuwapeleka Polisi nyumbani kwao Njombe alipokuwa anaishi baba na mama yake.

Orestus na mke wake walikuwa na mpango wa kutoroka ambapo alikamatwa na Polisi akiwa amejificha kwenye kichaka huku mkewe akiwa amelala kwenye nyumba ya wageni, baada ya kukamatwa na kuandika maelezo ya onyo, alikiri kutenda kosa hilo.

Orestus katika utetezi wake, alidai kukamatwa Juni 20, 2016 katika Kituo cha mabasi Njombe akiwa anakwenda mkoani Mbeya na kudai alitakiwa kuonyesha alipokuwa ameficha pikipiki na kuwa akiwa katika Kituo cha Polisi cha Kibena aliteswa na kutakiwa kukiri aliwakuta watu kadhaa na kuwaibia mali zao.

Katika kumtia hatiani mrufani, Jaji aliyesikiliza kesi hiyo aliegemea Orestus alikutwa na simu ya mkononi ya marehemu pamoja na kukiri katika maelezo yake ya onyo.

Miongoni mwa sababu za rufaa za Orestus ni kuwa Mahakama ilikosea kisheria kwa kutegemea vielelezo viwili kumtia hatiani, huku vielelezo hivyo vikikubaliwa bila utaratibu.

Pia  Mahakama kukosea kisheria kuufanyia kazi ushahidi wa shahidi wa nne ambaye ushahidi wake haukuwa wa kuaminika.

Nyingine ni Jaji aliyesikiliza kesi hiyo alikosea kisheria na kusema kwamba, upande wa mashitaka umethibitisha kesi yake bila shaka na kukosea kisheria kutegemea kielelezo cha nane ambacho ni simu ya mkononi ya marehemu kumtia hatiani mrufani, huku mlolongo wa ulinzi wa kielelezo hicho ukiwa haujaanzishwa.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili jopo la majaji hao kupitia kumbukumbu na maelezo ya pande zote mbili ilitupilia mbali sababu zote za rufaa hiyo kwa kuwa hazikuwa na mashiko.

Jaji Mwarija alisema kuhusu uhalali wa ripoti ya uchunguzi wa baada ya kifo na taarifa ya mrufani iliyoonywa, wana maoni kwamba madai hayo hayana uhalali.

Amesema kuhusu malalamiko kwamba ripoti ya uchunguzi wa mwili haielezi chanzo cha kifo ni  msimamo sahihi lakini kwa mujibu wa ushahidi wa shahidi wa nne, alieleza kifo hicho kilitokana na jeraha la kichwa.

Jaji Mwarija alieleza kutokana na ushahidi wa kumbukumbu, Orestus aliwaongoza Polisi hadi eneo la tukio ambapo awali, mwili huo ulikutwa na jeraha linaloonekana kwenye sehemu ya kichwani, kwa hiyo kutokuwepo taarifa kwenye ripoti hiyo hakubatilishi.

Jaji Mwarija amesema kuhusu hoja za maelezo ya onyo ya Orestus ni kweli, katika ushahidi wake wa utetezi, alikataa maelezo hayo na kukana kutenda kosa hilo na kuwa katika hali kama hiyo ushahidi huo ulihitaji uthibitisho kabla ya kufanyiwa kazi.

“Jaji alizingatia ushahidi wote na kubaini kuwa, maelezo yaliyoonywa yalithibitishwa na ushahidi kuwa Orestus alikutwa na simu ya marehemu muda mfupi baada ya kifo chake na ushahidi unaonyesha kuwa simu hiyo ilikuwa ikitumiwa na laini ya mrufani,” alieleza.

“Hivyo basi, tunakubaliana na Jaji wa Mahakama hiyo kwamba, ushahidi wa maelezo ya mrufani ulithibitishwa kwa hiyo malalamiko yaliyotokana na hitaji hilo hayana mashiko.” Kwa msingi wa sababu zilizotajwa hapo juu, tunaona kwamba rufaa imeletwa bila sababu za kutosha, hivyo inakataliwa,” amesema Jaji Mwarija

Related Posts