Pamba Jiji yarudi Ligi Kuu na gundu

PAMBA Jiji juzi Ijumaa ilicheza kwa mara ya kwanza mechi ya Ligi Kuu Bara baada ya kupita miaka 23 tangu iliposhuka daraja mwaka 2001 na kuishia kutoka suluhu na Tanzania Prisons, lakini sare hiyo huenda ikaigharimu timu hiyo kwa kupigwa faini au  kunyang’anywa pointi kwa tuhuma za kudaiwa kuchezesha wachezaji wasiokuwa na leseni za uchezaji kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Mchezo huo wa ufunguzi wa msimu wa 2024/2025 ulipigwa Ijumaa iliyopita kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza na kumalizika bila timu hizo kufungana, lakini mra baada ya dakika 90 zilianza kuenea taarifa kwamba wenyeji iliwatumia wachezaji wasiokuwa na leseni kinyume na kanuni za ligi.

Wachezaji hao wanaodaiwa kucheza bila ya leseni za msimu huu ni Paulin Kisindi raia wa DR Kongo na Erick Okutu raia wa Ghana waliosajiliwa kutoka Tabora United, ambapo wakati mchezo ukiendelea baadhi ya wasimamizi wa mechi kutoka Bodi ya Ligi walionekana wakizungumza na benchi la ufundi la timu hiyo.

Baada ya mazungumzo hayo wachezaji ho hata hivyo wachezaji hao walitolewa kipindi cha pili, Kiungo Paulin Kisindi alitolewa dakika ya 55 na kuingia Samuel Atwi, huku mshambuliaji, Erick Okutu alitolewa dakika ya 79 na kuingia Robert Kouyara.

Baada ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Pamba Jiji, Goran Kopunovic alilitupia lawama TFF kwa kuharibu mpango wa mechi na kuwalazimisha kufumua kikosi mara tano kabla ya mchezo huo kuanza jambo ambalo lilichangia timu hiyo kutopata matokeo ya ushindi.

“Tumelazimika kufanya mabadiliko ya kikosi mara tano kabla ya mchezo kuanza kwa sababu za vibali na leseni, mamlaka za soka zimetuvurugia mpango wetu wa mchezo na wachezaji wamecheza kwa presha, hii hakubaliki,” alisema Goran na kuongeza;

“Sina tatizo na utimamu wa wachezaji wangu wala mbinu zangu lakini tumevurugwa na usumbufu tuliosababishiwa, wachezaji wangu walicheza kwa presha nina matumaini mechi ijayo nitawatumia wote na tutakuwa tayari kuonyesha ubora wetu, taratibu tutafanya vizuri kwa sababu suala la leo limechangia kuwatoa mchezoni.”

Msemaji wa Pamba Jiji, Moses William alisema wachezaji hao wawili na wengine wote wamesajiliwa katika mfumo wa usajili wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kwamba kilichotokea ni kuwa hawakuwa na kadi za mkononi (hard copy), huku klabu hiyo ikijipanga kutoa taarifa kuelezea sakata hilo.

“Hawa wachezaji wote wamesajiliwa katika mfumo, lakini mamlaka zinasema mchezaji asicheze kama hard copy ya kuthibitisha ila kwenye mfumo tayari TFF ilishawathibitisha. Menejimenti imekiona hiki kinachozungumzwa iko kwenye mchakato muda siyo mrefu watalitolea taarifa kamili kuondoa mkanganyiko,” alisema William, huku hakuna kiongozi wa TFF aliyepatikana kutolea ufafanuzi juu ya tukio hilo.

Related Posts