Jiji la Dodoma hatarini kuwa eneo la makazi holela

Dodoma. Tangu Dodoma ilipotangazwa kuwa Jiji Aprili 2018, kumekuwa na kasi kubwa ya ongezeko la idadi ya watu na shughuli za kibinadamu zinazoathiri mifumo ya ikolojia hasa misitu na uoto wa asili.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi, idadi ya watu jijini humo imeongezeka kutoka 410,956 mwaka 2012 hadi 765,179 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 86.

Mbali na kutangazwa kuwa jiji, Serikali ya awamu ya tano ilihamishia rasmi makao makuu ya nchi mkoani humo.

Kutokana na ongezeko hilo, wadau wa mazingira wameshauri mamlaka za Serikali kuhakikisha jiji hilo linapangwa ili kuepuka uvamizi na ujenzi holela ulioathiri majiji mingine kama Dar es Salaam.

Katika Jukwaa la Maendeleo Endelevu 2024 lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi na kufanyika jijini Dodoma hivi karibuni, likiwa na kaulimbiu ya: “Kuhamasisha uwekezaji katika bustani za kijani kwa maendeleo endelevu Tanzania,” umuhimu wa kutunza maeneo ya wazi na bustani ulisisitizwa.

Akifungua kongamano hilo, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango licha ya kuagiza kuimarishwa kwa maeneo ya bustani nchini, ameutaka uongozi wa Jiji la Dodoma uanzishe bustani tatu kabla ya mwaka 2025.

“Ninafahamu mamlaka ya Jiji la Dodoma imetenga maeneo ya bustani hizo. Ninapenda kulishawishi Jiji kutangaza fursa za kuwekeza katika kuanzisha bustani hizo tangulizi.”

“Natoa wito kwa sekta binafsi kujitokeza kuanzisha bustani hizo ili pamoja na kutunza mazingira, tulifanye Jiji letu makao makuu ya Taifa letu kuwa la kupendeleza zaidi,” amesema Dk Mpango.

Katika bustani hizo, ameshauri jiji kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Misitu (Tafori) na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), bustani mbili ziwe ‘green parks’ (hifadhi za kijani) na moja iwe ya kibotaniki.

Mpango kabambe wa uendelezaji wa Jiji la Dodoma

Akitoa mada katika kongamano hilo, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Dodoma, Aziza Mumba amesema mapitio ya mwaka 2019 yamebainisha maeneo ya kuendeleza bustani za kijani (Land Scape Improvement Plan 2019 – 2039).

“Mpango unafafanua maeneo hayo yanapaswa kupandwa miti na kutunza uoto wa asili uliopo. Ili kupendezesha maeneo hayo, mpango ni kupanda miti na maua yenye kuvutia ili kulifanya Jiji la Dodoma kupendeza na kusaidia kusafisha hewa ya ukaa inayotokana na shughuli za kibinadamu.”

Alitaja maeneo yaliyopangwa kukijanishwa kuwa Mji wa Serikali ni maeneo ya wazi, pembezoni mwa barabara, vitovu vya huduma, stendi ya basi, kuzunguka eneo la kuhifadhi na kuteketeza taka ngumu, maeneo ya taasisi na ofisi.

Mengine ni maeneo tengefu ya kilimo (kilimo cha zabibu), eneo la katikati ya Mji wa Serikali na Ikulu, maeneo yanayozunguka mabwawa ya majitaka, kuzunguka mabwawa ya msimu na ya kudumu, maeneo ya viwanda na kupendezesha vilima.

Kuhusu matumizi ya jumla yaliyopendekezwa, Mumba alisema wanatarajia kutengeneza maeneo ya kupumzika, njia za kukimbia, njia za mashindano ya baiskeli, maeneo ya mazoezi, maeneo ya kuuza bidhaa za kitamaduni, maduka na bustani, sanamu za kumbukizi na mabwawa ya kutengeneza.

Matumizi mengine ya jumla yaliyopendekezwa ni mabwawa ya kutengeneza, kituo cha taarifa, maktaba ya wazi, duka la vitabu, sehemu ya vinywaji na viwanja vya michezo.

Hata hivyo, Mumba alisema kuna changamoto katika uendelezaji na usimamizi, akieleza kuna mahitaji makubwa ya rasilimali fedha katika kuanzisha na kusimamia bustani za kijani.

Kuna kubadilishwa kwa matumizi ya baadhi ya maeneo yaliyokuwa yametengwa kwenye Mpango Kabambe kama ya kukijanishwa na kuna shughuli za kibinadamu kama vile kilimo na ufugaji zinaathiri miti inayopandwa.

“Tunajipanga kuzingatia uwepo wa maeneo ya bustani za kijani wakati wa kuandaa Mpango Kabambe wa Jiji. Tutapima na kuyaandalia maeneo hayo hati ili yasivamiwe na wananchi kwa matumizi mengine,” alisema Mumba.

Ofisa Mipago Miji wa Jiji la Dodoma, Anna Paul amesema wakati uboreshaji wa jiji ukiendelea, kumekuwa na uvamizi wa hifadhi za barabara.

“Wafanyabiashara wanaweka gereji, wengine wanauza chipsi, matokeo yake wanachafua Jiji. Tumeshauri hifadhi hizo zipandwe miti na bustani za maua, kama ni biashara zifanywe kwenye maeneo husika,” amesema.

Akizungumza wakati wa mjadala katika kongamano hilo, Mkurugenzi wa Haki Ardhi, Cuthbert Tomito alisema kuna haja ya kudhibiti ukuaji wa miji kwa mfumo wa mlalo badala yake Serikali iweke sera na sheria ya kuwa na majengo mengi ambayo yanajengwa kwa mfumo wima.

“Hii itasaidia kupunguza spidi ya ukuaji wa miji ambao unasababisha ufyekaji wa miti na misitu mingi ili kujenga majengo,” amesema Tomito.

Pia, aliishauri Serikali kurejesha mfumo wa uwepo wa waangalizi wa ardhi maarufu ‘land rangers’ hasa katika maeneo ya mijini ili kulinda maeneo ya wazi yasivamiwe.

“Historia inatuonyesha hawa waangalizi walikuwepo wakati wa Serikali ya awamu ya kwanza na ya pili lakini baadaye waliondolewa na kusababisha uvamizi mkubwa wa maeneo haya ya wazi na watu binafsi na kujenga majengo ya makazi na biashara,” amesema Tomito.

Ameshauri pia kuwe na udhibiti wa upandaji wa miti hasa kwenye ardhi za vijiji, kwa kuwa wakati mwingine upandaji wa miti kwenye ardhi za kilimo unasababisha uhaba wa chakula.

“Miti iliyopandwa ambayo ukuaji wake mpaka ivunwe unachukua kati ya miaka 10 hadi 15 hali inayosababisha uhaba wa chakula kwenye baadhi ya familia,” amesema.

Akieleza changamoto za kisheria, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Charles Meshack amesema, mara nyingi miji inapopanuka, maeneo yaliyotengwa kisheria kwa ajili ya misitu, hubadilishwa matumizi.

“Eneo likishapandishwa hadi kwa mfano kuwa manispaa, hawautambui tena msitu uliohifadhiwa kisheria, badala yake wanaita ni pori na kulipangia matumizi mengine, kwa sababu sheria hazisomani,” amesema Meshack.

Akizungumzia changamoto ya maji, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alisema kwa idadi ya watu zaidi milioni 3.07 maji yanayozalishwa ni asilimia 42 ya mahitaji ambayo ni mita za ujazo milioni 132.

“Serikali imechukua hatua, kwanza kuna uchimbaji wa visima virefu eneo la Nzuguni utakaoongeza asilimia 11 ya mahitaji, pia kuna miradi mingine ya visima virefu katika maeneo ya Zuzu, Nala na Duwasa pia wamepewa mapendekezo ya kuchimba maeneo mengine,” amesema Shekimweri.

Ametaja mipango mingine ya muda mrefu kuwa ni kusubiri mradi wa maji ya Ziwa Victoria na ujenzi wa Bwawa la Farkwa.

Kuhusu maeneo ya wazi aliwataka viongozi wa Serikali za Mitaa kufuatilia maeneo hayo na kuyalinda.

“Kwenye maeneo ya wazi yaliyovamiwa ni kwa sababu ya masilahi ya kisiasa, kibiashara na kiuchumi,” amesema Shekimweri.

Amesema mkoa huo una jumla ya maeneo ya wazi 150 na zaidi ya maeneo 20 yamevamiwa.

Related Posts