CRDB Bank Marathon ilivyonoga Dar

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko ameipongeza taasisi ya CRDB Bank Foundation kwa kuendelea kuandaa mbio za CRDB Bank Marathon ambazo zimejielekeza katika kusaidia jitihada za serikali kuboresha sekta ya afya, kusaidia wenye uhitaji, pamoja na kukuza ustawi wa jamii.

Biteko ametoa pongezi hizo wakati wa kilele cha msimu wa tano wa CRDB Bank Marathon ambazo zimekusanya Sh350 million kwa ajili ya kusaidia watoto wenye uhitaji wa upasuaji wa moyo Taasisi ya Jakaya Kikwete (JKCI), huduma za afya kwa wakinamama wenye ujauzito hatarishi hospitali ya CCBRT, na uwezeshaji wa vijana.

“Niwapongeze kwa kuendelea kusaidia matibabu ya kinamama na watoto wetu.

“Kinamama ndio wamebeba uchumi wa Taifa letu piandio waangalizi wa familia zetu hususani watoto,” amesema.

Amesema ukiimarisha afya ya mama na mtoto umeimarisha afya ya Taifa.

Akizungumzia mbio hiyo, Waziri wa Sanaa, Utamaduni, na Michezo, Damas Ndumbaro amesema imesaidia kuchochea ari ya michezo nchini.

Amesema zimekuwa jukwaa muhimu kwa wanariadha nchini kuonyesha vipaji vyao katika jukwaa la kimataifa kwani mbio hizo zimesajiliwa kimataifa na Shirikisho la Upimaji Mbio Kimataifa (AIMS) na Shirikisho la Riadha Duniani (World Athletic).

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema katika fedha kilichokusanywa, Sh100 milioni zitasaidia watoto wenye uhitaji wa upasuaji wa moyo Taasisi ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Amesema kitita kingine kama hicho  kitasaidia huduma za afya kwa kinamama wenye ujauzito hatarishi hospitali ya CCBRT, na Sh150 milioni zitasaidia uwezeshwaji kwa vijana.

Akizungumzia mbio hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB Bank Foundation, Martin Warioba amesema zimeshirikisa wanamichezo zaidi ya 8,000.

Amesema washindi wamezawadiwa Sh98.7 milioni katika mbio za kilometa 42, 21, 10 na kilometa 5, pamoja na wa mbio za baiskeli za kilometa 65.

Amesema lengo la mwakani ni kupata washiriki 10,000 wa Tanzania, huku malengo ya washiriki wa Burundi na DR Congo yakiwa ni 3,000 kila nchi.

Katika mbio ya marathoni, Joyloyce Kemuma alishinda kwa wanawake wakati kwa wanaume, Moses Nengichi alishinda wote kutoka Kenya.

Katika mbio ya Kilometa 21 upande wa wanawake ni Sara Ramadhan na Joseph Panga wote Watanzania.

Kwenye kilometa 10, Hamida Nasoro wa Tanzania aliibuka mshindi na kwa upande wa wanaume, Mtanzania Mao Hindo Ako alishinda.

Kwenye mbio za baiskeli, Paul Lumoria alishinda na kufuatiwa na Richard Laizer na Joseph Thuku ambapo kwa upande wa wanawake mshindi alikuwa Jamila Abdallah na kufuatiwa na Monica Jelimo na Julia Miringu.

Related Posts