Singida Black Stars yaanza na moto  Ligi Kuu Bara

Singida Black Stars imeanza kwa kishindo msimu mpya wa Ligi Kuu Bara baada ya kuikaribisha na kipigo kizito, KenGold iliyopanda daraja kwa kuinyuka mabao 3-1 katika pambano tamu lililopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini hapa.

KenGold iliyopanda daraja sambamba na Pamba Jiji kutoka Ligi ya Championship, ilikumbana na kipigo hicho licha ya kucheza kwa dakika karibu 40 kwa nidhamu na kuwabana Singida, hata hivyo, umakini mdogo kabla ya mapumziko ilitoa mwanya wa kuruhusu bao la kuongoza la wageni.

Bao hilo la kuongoza la Singida, liliwekwa kimiani na Emmanuel Kayekeh dakika ya 41 kwa kufumua shuti la mbali akimchambua kipa Mussa Mussa, kabla ya kipindi cha pili, Elvis Rupia akaongeza la pili dakika ya 62 akiunganisha kwa kichwa mpira wa krosi ya Joseph Guede na wenyeji kucharuka na kupata bao la kufutia machozi lililowekwa kimiani na Joshua Ibrahim dakika ya 68.

Lakini wakati KenGold ikiamini huenda ingerudisha bao la pili, ikajikuta ikitunguliwa la tatu na Mohamed Kamara dakika ya 81 aliyeunganisha mpira wa kona iliyopigwa na Marouf Tchakei na kuifanya Singida kuvuna pointi tatu za kwanza msimu huu sawia na mabao matatu. 

Matokeo hayo yaliifanya Singida kuiengua Mashujaa iliyokuwa ikiongoza msimamo baada ya juzi kuifunga Dodoma Jiji kwa bao 1-0 na kukaa kileleni kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa (hii ni kabla ya mechi iliyofuata baadae jana jioni, kati ya Simba na Tabora United).

Kocha wa Kengold, Fikiri Elias alikiri walistahili kipigo kutokana na kuzidiwa na wapinzani wao, ambao wana wachezaji wazoefu na kwamba wanaenda kujipanga kwa mechi zijazo za ligi hiyo kwani itavaana na Fountain Gate kabla ya kuumana na Yanga wiki ijayo.

Kwa upande wa Patrick Aussems alisema timu yake ilikosa umakini kipindi cha kwanza licha ya kutengeneza nafasi nyingi iliambulia bao moja na alizungumza na wachezaji na kurudi kivingine kipindi cha pili na kupata ushindi huo ambao ameona ni mwanzo mzuri, japo anaenda kujipanga zaidi wa mechi zijazo.

Related Posts