WAKALA wa Usajili , Ufilisi na Udhamini (RITA) imesema kuwa katika kipindi cha miezi miwili iliyopita imepokea jumla ya maombi 198,972 ya vyeti vya vizazi na vifo na kati ya maombi hayo jumla ya waombaji 195,771 ambayo ni sawa na asilimia 98.4 tayari wamepatiwa vyeti vyao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA Frank Kanyusi amesema kuwa kati ya maombi hayo, maombi 179,485 yalikuwa ni ya uhakiki wa vyeti vya kuzaliwa na maombi mengine 19,487 ni ya uhakiki wa vyeti vya vifo.
“Maombi mengine 18,341 yalikuwa ya mapungufu ya vyeti hivyo ambapo wahusika walirudishiwa kwa ajili ya kufanya marekebisho,” alisema Kanyusi na kuongeza kuwa maombi 562 yalikataliwa kwa sababu vyeti vilivyowasilishwa kwa uhakiki havikuwa halali.
Kwa mujibu wa Kanyusi maombi mengine 3,201 yanaendelea kufanyiwa kazi na yatakamilika ndani ya siku chache zijazo.
Amesema kumekuwa na changamoto kadhaa ambazo zilichangia zoezi hilo kulegalega kutokana na changamoto ya kimtandao iliyojitokeza, ambapo kikundi kazi cha taasisi hiyo kilichukua hatua za haraka kutatua changamoto hiyo.
“Licha ya changamoto hiyo ya kimtandao kumekuwa na changamoto tofauti tofauti kutoka kwa waombaji ambazo zimefanya baadhi ya waombaji kutokubaliwa kuhakiki vyeti vyao ikiwemo kuambatanishwa kwa nakala zisizosomeka ambazo maandishi yake yamefifia, hivyo kuwafanya wataalumu kushindwa kusoma,” alisema.
Kanyusi alisema kuambatanisha nyaraka isiyo sahihi, mfano cheti cha kuzaliwa badala ya cheti cha kizazi imefanya baadhi ya vyeti kushindwa kuhakikiwa na
pia kumekuwa na makosa ya baadhi ya nyaraka kuwekwa nywila (password), hivo wakala kushindwa kuzihakiki.
Akifafanua zaidi, Afisa Mtendaji Mkuu huyo amesema kumekuwa na makosa ya kutuma nakala ya vyeti vilivyotolewa nje ya nchi ambavyo RITA haina mamlaka ya kuvihakiki sambamba na wengine kushindwa kufuatilia majibu yao ya uhakiki katika akaunti walizofungua hivyo kuchangia ongezeko la malalamiko.
“Changamoto tulizokutana nazo zilikuwa ni nyingi lakini kwa kushirikiana na wataalamu wetu tuliendelea kuzitafutia ufumbuzi wa haraka. Kwamfano wapo baadhi ya waombaji wamekuwa wakichagua sababu ya kuomba uhakiki tofauti na inayotakiwa ya kuomba mkopo wa elimu ya juu,” alisema.
Kanyusi alisema RITA imeendelea kutoa elimu kwa baadhi yao wanaofika katika ofisi zake pamoja na kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii.
Mbali ya vyeti vya uzazi na vifo, amesema RITA pia hupokea mombi ya wanafunzi wanaoomba vyeti vya kuzaliwa kwa ajili ya kukidhi moja ya vigezo vilivyowekwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya kupata mkopo.
Kanyusi amewataka waombaji wa mikopo ya elimu ya juu kutumia vyema muda uliobaki kuhakiki vyeti vyao vya kuzaliwa na vifo ndani ya wakati ili waweze kuwa na sifa ya kupata mikopo hiyo.
Amesema zoezi la kupokea vyeti hivyo litafungwa siku chache zijazo na hivyo kuwataka wanafunzi hao kutuma maombi yao kupitia mitandao yao kijamii ya RITA ili waweze kujua vigezo vya kukidhi maombi yao.