Arusha. Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), imesema shughuli za utalii katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro zinaendelea na kuwahakikishia usalama watalii waliopanga safari kwenda hifadhini humo.
Hata hivyo taarifa hiyo imetolewa leo Jumapili Agosti 18, 2024 baada ya leo asubuhi kwenye mitandao ya kijamii, kuonekana picha mjongeo na picha mnato zikionyesha baadhi ya watu wa jamii wa Kimasai waishio Tarafa ya Ngorongoro wakiandamana.
Watu hao wanadai kukosa huduma za kijamii baada ya kugoma kuhama kwa hiari katika eneo hilo.
Katika maandamano yao, wananchi hao walidaiwa kuweka vizuizi barabara kuu na magari ya watalii kukwama.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Kaimu Meneja Kitengo cha Uhusiano kwa Umma (NCAA), Hamis Dambaya imesema shughuli za utalii katika eneo hilo zinaendelea vizuri licha ya uwepo wa baadhi ya wananchi waishio katika hifadhi hiyo kuandamana leo asubuhi.
Taarifa hiyo imeeleza watalii kutoka ndani na nje ya nchi wameendelea na safari zao za kushuhudia vivutio vya utalii ndani ya Hifadhi na Serikali inaendelea kuwahakikishia usalama wao.
“Maandamano yaliyoripotiwa kupitia baadhi ya mitandao ya kijamii yanaidhihirisha dunia na jumuiya za kimataifa, vyombo vya habari na asasi za kimataifa kwamba ndani ya hifadhi hiyo hakuna ukiukwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji wa wananchi,” imesema taarifa hiyo na kuongeza;
“Mamlaka inawahakikishia watalii wote waliopanga safari zao kuja Ngorongoro kuwa Serikali itaendelea kusimamia usalama wao wakati wote watakapokuwa ndani ya hifadhi.”