Dar es Salaam. Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha), umesema hivi sasa matukio ya ajali kazini yamepungua na badala yake yameibuka magonjwa kazi mahala pa kazi.
Umeyata magonjwa hayo kuwa ni ya misuli, viuno, shingo na mgongo kutokana na wafanyakazi kutumia vifaa visivyo sahihi na mtindo wa maisha kazini.
Akizungumza na wanachama wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari nchini (Jowuta) juzi, Mtendaji Mkuu wa Osha, Hadija Mwenda amesema ili kuondokana na changamoto hiyo, ni muhimu kuzingatiwa sheria, kanuni mahala pa kazi, ikiwamo wafanyakazi kutapiwa vifaa sahihi nao kuvitumia.
“Sasa hivi magonjwa ya misuli, viuno, migongo, shingo, ndio magonjwa yanayoitafuna dunia, takwimu zinaonyesha hivyo.
“Hivi sasa ajali mahala pa kazi zimepungua, lakini magonjwa kazi yamekuwa yakiongezeka kutokana na mtindo wa maisha ya wengi, hali ambayo imekuwa ikichangiwa na matumizi ya vifaa visivyo sahihi, mfano viti ambayo si rafiki hasa kwa wanaofanya kazi za kukaa kwa muda mrefu,” amesema na kuongeza;
“Jukumu la Osha ni kuhakikisha haya magonjwa hayatokei kwa kuweka mifumo mizuri ya kuwalinda wafanyakazi dhidi ya ajali na vinavyosababisha magonjwa na miundombinu iwe sahihi isiyoleta vifo sehemu ya kazi,” amesema.
Amesema hali hiyo inasababisha athari mbalimbali, ikiwemo za kiuchumi, kwani mtu aliyetakiwa kufanya kazi kwa siku tano, analazimika kutumia siku tatu kwenda hospitali, hivyo utendaji wake wa kazi kupungua.
Mtendaji huyo wa Osha amesema wamefanya tathmini na kubaini uelewa kwa jamii kuhusu usalama mahala pa kazi ni mdogo, hivyo wameamua kushirikiana na waandishi wa habari kusaidia kufikisha elimu hiyo kwa wananchi.
“Hakuna mazingira ya kazi ambayo hayana vihatarishi, lakini tunataka tahadhariu zichukuliwe ili mtu akistaafu asione ndiyo anakwenda kufa, lazima tutoe elimu kuhusu mtindo sahihi wa maisha sehemu za kazi,” amesema.
Kwa upande wake, Meneja wa Mafunzo na Uhamasishaji wa Osha, Shabani Mbaga amesema ili wananchi kuwa salama katika maeneo ya kazi lazima kufuata sheria za usalama wa afya kazini.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkufunzi wa huduma ya kwanza kutoka wakala hiyo, Moteswa Meda amesema kuna umuhimu jamii kupewa elimu jinsi ya kujikinga na vihatarishi mahala pa kazi.
Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi wa vyombo vya habari nchini (Jowuta) Musa Juma amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa waandishi wa habari kulingana na mazingira wanayofanyia kazi.