Dar/Mbeya. Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), imesema bado haijafikishiwa jalada la kesi ya vijana watano wanaotuhumiwa kutekeleza tukio la ubakaji na ulawiti wa binti anayedaiwa kuwa mkazi wa Yombo Dovya, Mkoa wa Dar es Salaam.
Picha jongefu (video) kuhusu tukio hilo zilisambaa Jumapili ya Agosti 4, mwaka huu kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha vijana watano wakimbaka na kumwingilia msichana huyo kinyume cha maumbile.
Katika video nyingine watuhumiwa hao wanasikika wakimhoji binti huyo na kumshurutisha amwombe radhi mtu aliyetajwa kwa jina la afande, naye alifanya hivyo.
Hata hivyo, katika taarifa aliyoitoa kwa umma Agosti 9, 2024, Msemaji wa Jeshi hilo, David Misime alisema uchunguzi umewezesha kubaini tukio hilo lilifanyika Mei 2024 katika eneo la Swaswa jijini Dodoma.
Aliwataja vijana waliokamatwa kwa kosa la kumlawiti na kumbaka binti huyo ni Clinton Damas jina maarufu Nyundo, Praygod Mushi, Amini Lema na Nikson Jakson.
Misime alisema watuhumiwa hao walikamatwa mkoani Dodoma na Mkoa wa Pwani na Jeshi hilo linaendelea kuwatafuta watuhumiwa wawili ambao walikuwa hawajapatikana mpaka wakati huo.
Mwananchi leo Jumapili Agosti 18, 2024 limezungumza na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Sylvester Mwakitalu kuhusiana na hatua iliyofikiwa katika uchunguzi wa sakata hilo na kipi kinaendelea.
Mwakitalu amesema jalada la tukio hilo bado halijamfikia mezani kwake kwa kuwa bado linaendelea kuchunguzwa na Jeshi la Polisi.
“Bado upelelezi unaendelea na likifika kwangu ni kukamilisha upelelezi tu, isipokuwa kwa sasa bado jeshi linaendelea na upelelezi,”amesema DPP Mwakitalu.
Alipoulizwa kuhusu mwenendo wa uchunguzi wa tukio hilo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Ramadhan Kingai amesema aulizwe Kamanda wa Mkoa wa Dodoma na Msemaji wa Jeshi la Polisi watakuwa na majibu sahihi.
“Suala hilo mtafute Kamanda wa Polisi Dodoma au Msemaji wa Jeshi la Polisi watakueleza hatua za tukio hilo lilipofikia,”amesema Kingai
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, SACP Theopista Mallya amesema jalada la tuhuma hizo limekamilika na kwamba kesho Jumatatu Agosti 19, 2024 atafuatilia kama litapelekwa mahakamani.
Amesema katika uchunguzi, Jeshi la Polisi limebaini vijana hao waliotuhumiwa kwa madai ya kutumwa, walikiri kutoagizwa na askari kama ilivyoelezwa.
“Kilichobainika vijana hao hawakutumwa na askari, walikuwa kama walevi na wavuta bangi tu, lakini yule dada alikuwa kama anajiuza ‘kahaba’.
“Neno askari ni General (jumla) kwa kuwa hata mgambo ni askari, hivyo hatuwezi kulifafanua zaidi kwa kuwa haikubainishwa wazi na tunaliacha hivyo” amesema kamanda huyo.
Hata hivyo, Mwananchi ilimtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi, Misime kutaka kujua kama watuhumiwa wengine wawili waliobakia kati ya sita wanaotuhumiwa hakupokea simu na alipotumiwa ujumbe kwa whatsapp aliousoma lakini hakujibu chochote.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.